Saturday, March 26, 2011

Mfanye ndugu yako kuwa rafiki, maisha yatakuwa mazuri sana na yenye furaha tele.

Maisha yana maonevu mengi, kukasirikiana na magomvi yasiyo maana baina ya ndugu hurudisha nyuma maendeleo na kusababisha maradhi.

Husemwa ndugu wakigombana tafuta jembe ukalime, na wakipatana nenda ukavune. Lakini hayo yote hayawezi kutokea ikiwa hakuna upendo kati yenu. Umeshawahi kuwaona ndugu wa baba mmoja mama mbalimbali hawasemani? ama baba mbalimbali mama mmoja pia hawasemani? Tafakari.

Dawa pekee ya kufanya udugu ukashamiri ni kumfanya ndugu yako kuwa rafiki, kiswahili cha sasa: awe zaidi ya ndugu. Maisha yatakuwa rahisi kuishi. Mtacheka na kufurahia uhai pamoja pasi kujali tofauti zenu.

Kugombana ni ada ya mwanaadamu, ila ugomvi wa ndugu huchelewa kuisha ingawa haufanyi udugu ukaisha, ila ugomvi wa marafiki hudumu kwa muda mchache sana kwa maana tabia huvutana kuwa pamoja tena.

Umeshawahi kuona mtu anakuwa mkali hasikizani na ndugu zake, utasikia watu wakisema 'kamuiteni fulani ndie anaemuweza huyu'. Na huyo fulani anakuwa ni rafiki tu, hudhani ni kichekesho? Ndugu wote wameshindwa kumtuliza ila rafiki ameweza. Huoni ipo haja ya kuokoa muda na kumfanya ndugu yako kuwa rafiki? Fikiri hili kwa makini.

Nalo liwe neno la leo...

No comments:

Post a Comment