Saturday, March 19, 2011

Tunavitumiaje vipaji vya utotoni kutuokoa na ukali wa maisha?

Na Hafidh Kido
Tunapokuwa wadogo tunakuwa na muda mwingi sana wa kuzitumia akili zetu kwa kila tunachodhani kitatupa furaha. Suala hilo hutufanya tuwe na uvumbuzi na uga mpana wa kufanya mambo.

Imegundulika kuwa wanaadamu wanashindwa kuendelea kwa kukosa uthubutu. Maana wengi huogopa matokeo mabaya ya majaribio yao. Bila ya kuzingatia kuwa mavumbuzi ya vitu kama ndege na magari yalipitia majaribio mengi ya hatari na kukatisha tama, mpaka kufanikiwa.

Chunguza tunapokuwa wadogo tunataka kujaribu kila tunachokifikiri ama kukiona kwa wenzetu. Jiulize ulifanya vitu vingapi ambavyo havikuleta matokeo mazuri, lakini kitu gani kilichokuathiri? 

Tulijenga nyumba za udongo, zipo zilizopendeza na zipo zilizokuwa mbaya, tulijenga magari, yapo yaliyokuwa mazuri na yapo yaliyokuwa mabaya, tulichora picha za watu na vitu, kadhalika zipo zilizovutia wenzetu na zipo zilizochekesha. Lakini hatukukata tamaa mpaka tulipopata kilicho bora.

Tukiwa wakubwa tunasahau yale yote yaliyotufanya tusifiwe na kujulikana nayo pindi tulipokuwa wadogo. Na hili linatokana na kutopata msukumo kutoka kwa waliotuzunguka ama jamii ilitudangaya kuwa kipaji tulichonacho hakitoleta faida yoyote.

Jiulize katika umri huo wa utu uzima, unawakumbuka marafiki wangapi ambao utotoni walikuwa na vipaji kama kusakata kabumbu, kuchora, kuogelea, kuimba  ama kukimbia mbio fupi na ndefu; kiasi mtaani walijulikana kwa vipaji hivyo kuliko kwa majina yao. Lakini sasa ukikutana nao hawana hata moja katika vipaji hivyo, na la kusikitisha zaidi atakwambia maisha ni magumu na kazi hazipatikani.

Kupuuzwa kwa vipaji vya utotoni kunatokana na mambo mawili katika mengi: moja ni kukosa msukumo kutoka kwa wazazi ama walezi. Hili hufanya watoto waone wanachokifanya hakina faida kwao na kwa jamii. Katika hili mzazi, mlezi ama jamii inaweza kumkataza mtoto kucheza mchezo fulani kwa madai ni mchezo wa hatari.

Kwa mfano, mtoto anaweza kuwa na kipaji cha kuogelea, kuruka sarakasi ama kucheza soka, badala ya kutafutiwa utaratibu wa kuendeleza kipaji hicho matokeo yake hukatazwa kabisa na hata kufikia wakati akionekana anacheza hupewa adhabu.

Wakati huohuo mtoto anaweza kutoroka masomo kwa kuendekeza kipaji chake cha kuimba, kucheza mpira wa miguu, magongo au kikapu. Lakini kwa mzazi mwenye busara atakaa na mtoto wake amtafutie shule ambayo inakuza vipaji aina yake. Hivyo mtoto atakuwa anapata shule na anaendeleza kipaji alichochagua.

Jambo la pili linalosababisha kupuuzwa kwa vipaji vya watoto ni kukatishwa tama; wazazi wanaweza kukukubalia kipaji chako na kukupa msaada wa hali na mali. Tena inafika wakati ukipitisha muda wa kuenda mazoezini wazazi ndiwo wanaokukumbusha.

Lakini jamii inaweza kukukatisha tamaa kwa kukujaza maneno kuhusiana na kipaji chako; hii hutokana na aina ya mchezo au kipaji ulichonacho namna jamii iliyokuzunguka inavyokichukulia.

 Kwa mfano kijana anaeimba mziki jamii inamchukulia kama muhuni na mtovu wa maadili. Mtu anaejihusisha na mbio za magari atachukuliwa kama anahatarisha maisha yake. Hivyo jamii itaweza kukaa na kijana na kumkatisha tamaa kiasi atauchukia mchezo ule.

Ifike wakati serikali ione umuhimu wa kuangalia vipaji vya watoto tangu wakiwa shule za msingi, nakumbuka miaka ya tisini shule za msigi zilikuwa na somo la sanaa; wanafunzi tuliagizwa kutengeneza mafagio, magari, nyumba za maboksi na kila kile ambacho mwanafunzi alidhani kipo ndani ya uwezo wake.

Kitendo hicho kilifanya waalimu kutambua vipaji vya watoto, na baadhi ya wanafunzi ambao walionyesha uwezo mkubwa katika vitu walivyotengeneza waliwekwa pembeni na kupelekwa katika shule za jirani na kushindanishwa. Kulikuwa na mashindano ya kata, wilaya, mkoa kanda mpaka taifa na hata kimataifa.

Sijui kama utaratibu huu unaendelea ama la.. lakini ni utaratibu mzuri sana ambao umeweza kuinua vipaji vya watoto wengi ambao leo hii ni maarufu katika mambo waliyochagua.

Wapo wachoraji katika magazeti na vitabu, wapo wanasoka, wacheza kikapu, wakimbiaji, waimbaji na hata waogeleaji ambao wamepata mafanikio kutokana na utaratibu ule.
Michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA ilisaidia sana kuibua vipaji vya wachezaji wakubwa katika ligi za Tanzania katika kikapu na soka. Ipo haja kwa serikali kulifikiria hili kwa upana wake.

Wenzetu weupe wanathamini sana kuendeleza vipaji vya watoto, kwa maana wanaamini watoto ndiwo watakaokuwepo baada ya wao kuondoka; ikiwa watadharau kuwarithisha vipaji walivyonavyo na ujuzi waliojaaliwa na Mungu, maana yake wanaandaa taifa la watu walio watupu.

Naomba kuwasilisha..   

No comments:

Post a Comment