Friday, March 4, 2011

Bob Marley alikuwa mvuta bangi, lakini nidhamu imemfanya aheshimike duniani.

NIDHAMU
 
 
NIDHAMU


By Hafidh kido
Kaka yangu Maggid Mjengwa, katika maandiko yake humu facebook, alipata kuandika utaratibu wake wa maisha kila anapoamka asubuhi. Nilivutiwa sana na muda ambao hufanya mazoezi ya kukimbia ‘jogging;’ niliandika kumuonea ngowa au wivu juu ya kufanya kwake mazoezi muda wa asubuhi.

Kwa maana kama unachelewa kulala, lazima utachelewa kuamka; hivyo kwa sisi tulio vyuoni na wengine walio makazini muda wa asubuhi huwa ni wa kujiandaa kutoka. Na mara nyingi huwa umechelewa. Sasa ikiwa kuna watu walio na shughuli nyingi kama kina Mjengwa, wanapata wasaa wa kufanya mazoezi, inastaajabisha kidogo.

Nilionyesha kuyatamani maisha yake, naye kwa busara alinijibu neno moja tu ambalo lilininyima raha siku nzima mpaka nilipopata wasaa wa kukaa chini na kuliandikia kurasa hizi kutoka katika neno hilo moja.

Alinambia bwana Hafidh, unaweza kuwa kama mimi unachotakiwa ni ‘nidhamu,’ lile neno nidhamu ndilo lililonisisimua. Nikakaa na kujiuliza neno dogo kama hili mbona limeushtua sana moyo wangu na kukosa raha siku nzima? Lina nini ndani yake mpaka likanipa mzigo mkuu namna hii.

Naam, nidhamu ni chachu ya maendeleo. Na ndiyo maana mungu amehubiri nidhamu katika matendo yake, huchukia sana watu wasio na nidhamu.

Nilijaribu kutafuta kamusi ya Kiswahili kwa Kiswahili ili kujua maana ya neno nidhamu limeelezwaji kwa kirefu. Sikubahatika kuipata, ila kwa ufahamu wangu mdogo wa lugha ya Kiswahili nidhamu ni adabu, maadili au mfumo wa maisha ambao unamfanya mtu afuate taratibu zilizopangwa bila ya kukengeuka.

Wanajeshi somo la kwanza baada ya kujiunga na jeshi ni nidhamu, huwezi kuwa mwanajeshi , mwanausalama au polisi kama huna nidhamu. Ni amri moja tu mdogo kwa mkubwa; Nidhamu.

Ukiamua unaamka saa kumi na moja ya asubuhi, unasali, unafanya mazoezi, unasoma magazeti, unaoga na kuelekea kazini, chuoni ama shuleni; utaratibu huo wa maisha unahitaji nidhamu kuweza kuufuata. Kama huna nidhamu lazima utakuwa mvivu wa kuamka na kutekeleza yote hayo.

Nidhamu hukufanya kukumbuka wajibu, hukulazimisha kutenda  kitakiwacho wakati huo bila kuchelewa wala kukosa. Kifupi hukujengea kufuata utaratibu na kuepuka njia za mkato ama uzembe.

Kutokana na neno hili moja ‘nidhamu’ lililotoka katika kinywa cha mwanajamii Mjengwa, nimegundua jamii inakosa maendeleo kwa kupungua nidhamu ya uwajibikaji; watu wanaanguka mitihani darasani kwa kukosa nidhamu ya kuzingatia wanachofunzwa, biashara hazileti faida kwa kukosa nidhamu ya mapato na matumizi, mashirika yanafilisika kwa kukosa nidhamu ya kazi. Hata ndoa zinavunjika kwa kukosa nidhamu.

Cha ajabu jeshi linaheshimika na kuogopewa katika jamii, unadhani ni nini kinawatisha? kwasababu jeshini kuna nidhamu. Mtu asie na nidhamu hafai kuwa mstari wa mbele.

Hivyo nimegundua hakuna kinachoshindikana katika uso wa dunia ikiwa kutakuwa na utaratibu wa kuwa na nidhamu, mtu yeyote duniani akitaka kuwa sawa katika maamuzi na jamii imuheshimu hana budi kuwa na nidhamu.
Nimejifunza kitu kipya kutoka kwa mzee wa neno la leo mwenzangu, nacho ni nidhamu.
Naomba kuwasilisha.

No comments:

Post a Comment