Saturday, December 11, 2010

Hatutakua huru mpaka siku moja tutakapoamua kuwa huru.


 
Na Hafidh kido

Taaluma ya uandishi wa habari ni kama dini mpya inayojiamualia mambo yake na kuishi katika dunia watu waso fikira njema kutofika. Yanaweza kuwa ni maneno mabaya lakini yana maana kubwa kwa wale waliopata kuhudhuria darasa la taaluma ya uandishi wa habari.

Huo ndiwo msingi wake, unapoamua kuwa mwandishi hasa wa habari ni lazima ujivue katika imani yoyote; ikibidi hata familia yako uikane pale panapostahiki kuandikwa ukweli kuhusu jambo fulani.

Na ndiyo maana katika taaluma hii kuna neno la kimombo linasemwa ‘ethical dilemma’ au ‘conflict of interest;’ hivi ni vitu vinavyoogopwa sana na mwandishi aliekula kiapo kuwa msafi.

Kwa muda mrefu tangu kuingia mfumo wa vyama vingi ile ladha ya uandishi wa hakika imeonekana kupungua nchini. Waandishi shupavu na wanaosimamia haki wamepungua ama hawapo tena. Na hata aina ya magazeti tuliyonayo hayana hadhi ya kuitwa magazeti yenye kupasha habari. Unafiki mtupu.

Najua nitapata taabu nyingi baada ya kuandika haya, maneno kama ‘silijui nilitendalo, sijakomaa katika taaluma ya habari ama nimetumwa,’ yatakuwa mengi sana. Ni bora nikose kupendwa lakini niandike kile ninachoamini; ili siku nikifa nisigeukegeuke kaburini kwa kutamani kurudi duniani kufanya hiki nikifanyacho sasa. Kuandika ukweli.

Inahitaji muhariri mwenye moyo wa kutojali mwajiri wake atasema nini ili kuweza kuruhusu makala kama haya kuchapwa katika kurasa zake. Lakini hilo si lengo la makala haya, tujali kilichotuleta humu.

Mimi nipo Uganda kimasomo, lakini taaluma yangu ya uandishi haikomi kwa kuwa nje ya mipaka ya nchi yangu, ule udakuzi wa kutaka kujua kila kinachotokea nyumbani umenifanya kusoma mengi na kuona vita vingi vya waandishi wakongwe wenye kutajika katika tasnia ya habari hapa nchini.  

Kwa kipindi fulani nimekuwa nikifuatilia mabishano hayo, na mengi yalikuwa yakitoka nje ya taaluma hii, taaluma iliyotokea kuogopewa sana na jamii bila kuheshimiwa. 

Ndiyo! Tunaogopewa kwa maana kila tunapoona jambo limeenda mrama tunasema, na hatuheshimiwi kwa kuwa tukinunuliwa kidogo tunafunga midomo yetu na kalamu zinakoma kuandika.

Nimeliona hilo, japo ni mchanga katika taaluma: haimithiliki kwa muandishi kuchagua gazeti la kupeleka habari yake baada ya kuiandika. Maneno kama ‘aahahaa usipeleke makala hayo katika gazeti fulani, hawatoitoa,’ ni aibu sana kufikia hapo.

Kwa maana taaluma ya uandishi habari imekuwa inabadilika misingi na maadili yake kila unapotoka gazeti moja kwenda jingine. Kifupi uandishi wa habari umekuwa ni biashara za kulinda maovu ya watu fulani na kuwakomoa watu fulani kwa sababu tu mmiliki wa gazeti lako haivi na mtu huyo.

Mwandishi wa habari hawakilishi mawazo yake, ni kinyume na mafundisho kutumia neno ‘mimi.’ Bali huandika alichokiona na chenye ukweli, hakandamizwi mtu bali dunia hutaka kujua kinachoendelea kiwe kibaya ama kizuri. Lakini lazima ufuate taratibu.

Kama mtu amekwenda kinyume na maadili fanya nae mahojiano, sikiliza upande wa pili unasema nini, oanisha na tazama haki iko wapi. Usiandike habari kumkomoa mtu, bali toa taarifa kwa manufaa ya umma. Lakini wakati huohuo mhariri hana haki kuzuia habari kwa kuwa tu alieandikwa ana maslahi nae, ni shoga yake ama ndie anaemuweka mjini, ingawa ni kweli amekosa.

Kuna muhariri nguli wa gazeti maarufu nchini, baada ya kutokea sakata fulani la kiuandishi (mgogoro wa kupinga kutaka kuteuliwa waziri fulani wa zamani) alitoa maneno mazuri ambayo nimeyapenda na nikaamua kuyaandikia makala haya unayosoma. Alisema ‘hatutakuwa huru mpaka siku moja tutakapoamua kuwa huru.’ 

Ni kweli waandishi hawataki kuwa huru? Hiyo siku ya kuamuwa kuwa huru itakuja lini kama wasipoamua sasa. Tambua mwandishi unalalamika huthaminiwi katika jamii, lakini huwezi kuthaminika mpaka uanze kujithamini mwenyewe kwanza. 

Mfano ulio hai waandishi wengi wanaishi bila ya mishahara, wanalipwa posho kwa jina la ‘retainer’ ni vibarua, mwajiri ‘atakuretain’ mpaka lini? Waandishi wengi hawana ajira kwa miaka hata kumi katika kampuni na bado wanaendelea kuinufaisha kampuni. 

Tena ukimkuta katika kusaka habari ndani ya gari la kampuni ameweka sambusa (kisugudi) nje, tabasamu kuubwa. Unafurahia nini, au kuwapo mmoja wa vibarua wa gazeti fulani? Inasikitisha.
Lakini akisikia kuna wafanyakazi katika taasisi fulani wamegoma kwa mshahara kiduchu, au wanataka ajira wamechoka kuwa vibarua; waandishi ndiyo wa kwanza kukimbilia na vikamera vyao, hao hao mbio mbio kuandika makala nzito nzito na habari ‘front page.’ 

Ila akirudi ofisini hana mshahara mpaka ‘stori’ yake itoke apewe elfu tatu au tano, au makala apewe elfu kumi au elfu kumi na tano.  Mpaka lini?

Na hautosikia muandishi anaandika makala au habari inayohusu waandishi wenzie kuwatetea haki zao. Anaogopa makala hayo yakionekana kitumbua chake kitaingia mchanga. Tunakwenda wapi na tutafika lini..

Kuna dhana kuwa viongozi wengi wa vyama si CCM, CHADEMA na CUF  tu, bali vyama vyote vya siasa, asilimia kubwa wanamiliki vyombo vya habari, au kuna chombo cha habari wana mkono wao. Lengo likiwa ni kuficha maovu yao na kulipua maovu ya wapinzani wao kisiasa ama kiitikadi. Lakini ikumbukwe si wao wanaoandika habari hizo, bali ni waandishi wa habari ndiwo watumikao kama mbuzi wa sadaka kutimiza malengo ya mabwana wakubwa.

Kuuza taaluma ni sawa na kuuza utu wako, hilo halihitaji shahada ya chuo kikuu kulitambua. Lakini leo hii wafufuke wale waandishi wa zamani waliopata kubobea katika fani hii, na waulize ‘uwapi ule ujasiri waliokuwa nao waandishi wa zamani’ mtajibu nini?

Hatutakuwa huru mpaka siku moja tutakapoamua kuwa huru. 

Angalia ujanja wa walanguzi wa taaluma za watu, kibopa baada ya kukwapua fedha za umma anaanzisha gazeti ama redio, ananunua kampuni kubwa iliyokuwa imara katika kutoa habari zenye hoja nzito. Makampuni ya habari yaliyokuwa mwiba kwa mafisadi na wakengeuka maadili katika jamii.

Baada ya kununua kampuni haishii hapo, ananunua na waandishi. Kichekesho: ati muandishi nae ananunuliwa, na baada ya muandishi kununuliwa nae anajiuza kwa bei rahisi kwa kuandika anachoambiwa na si anachoona.

Mwandishi anaweza kuulizwa na mwajiri wake, ‘tazama pale unaona nini?’ Atajibu ‘nimeona pikipiki inapita,’ basi ataambiwa ‘sasa nakutaka uandike ni gari ndiyo iliyokuwa inapita sawa?’ nae ataandika vilevile alivyoambiwa na bwana mkubwa, ingawa bwana mkubwa huyo hajui hata kuandika ‘lead’ ya habari. Ama hajui hata ‘5W na 1H’ zina maana gani katika habari.

Hajui hata ‘balanced story’ ni kidubwasha gani katika taaluma ya habari. Na bado anakuamulia cha kuandika, huoni haya?
Ifike wakati waandishi nao wanapoingia katika shughuli maalum waheshimike, watambulike uwepo wao. Wajulikane tena kwa majina kama wanavyotambulika madakitari, wahandisi na wanasheria.

Lakini hawawezi kufika huko mpaka jamii iwathamini kutokana na kazi zao zenye haki, mnapoandika kitu kiwe na maslahi katika jamii. Kisilenge kumchafua mtu wala kufurahisha kundi fulani katika jamii au serikali.

Elimu nayo hurudisha nyuma waandishi, hawasomi mpaka wawekewe sheria kwamba mwandishi haajiriwi mpaka awe na shahada. Ni aibu mwandishi una stashahada ama astashahada halafu unafanya mahojiano na mtu mwenye shahada ya uzamivu (Phd) au ni profesa.

Utaona tu hamlingani katika mawazo na aina ya maswali unayouliza hayatokuwa na mantiki wala kuhitaji majibu ya kiuchambuzi.

Na ndiyo maana Rais mstaafu Benjamin Mkapa, amenukuliwa mara kwa mara akiwaponda waandishi wa habari wa Tanzania. Hata mwaka jana  katika maadhimisho ya miaka hamsini ya kampuni kubwa ya habari Afrika Mashariki ‘National Media Group’ jijini Nairobi Kenya, alirudia maneno yake kuwa haturuhusu mwandishi asie na shahada kufanya nae mahojiano.

Hapa naomba niweke wazi, hoja yangu sisemi kuwa waandishi wasio na elimu si waandishi, la hasha. Tena unaweza ukakuta mwandishi ana cheti tu, lakini anaweza kukuandikia habari mpaka ukasikia raha, na mwandishi mwenye shahada akashindwa hata kuandika ‘lead’ au anaweza kuingia chumba cha habari kutoka mtaani lakini hata hajui ‘source’ wake alizungumza nini ambacho ni habari.

Lakini tutambue dunia ya sasa inabadilika, kusoma ni kila kitu. Ukiwa na elimu utajua mambo mengi, na hata ukikutana na watu wenye maringo kwa kuwa tu wamesoma wakigundua wewe umesoma zaidi yao au una uelewa mpana kuliko wao, hakika watakuheshimu na wataufyata mkia.

Cha ajabu mwandishi akishaamua kusoma akipata shahada yake iwe ya siasa, uongozi ama uchumi, basi huihama taaluma na kutafuta kazi mahala kwegine. Kwanini usiendelee kuwa mwandishi uliebobea katika masuala ya uchumi, siasa au jamii kulingana na shahada yako? 

Kwa kuikimbia taaluma yako kisa u msomi tafsiri yake ni kuwa uandishi habari ni wa ‘vilaza’ watu wasiosoma. Kamwe hilo sikubaliani nalo, tubadilike.

Hatutakuwa huru mpaka siku moja tutakapoamua kuwa huru. Nalo liwe neno la leo.
mwisho

Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi wa shahada ya mawasiliano ya umma. Kampala International University. Kampala Uganda. hafidhkido@yahoo.com +256 791848055 au +255 713593894.


Hatuna ujanja lazima tule. Umelizingatia hili?



Na Hafidh Kido

Wanaadamu tumekuwa na viburi vingi kutokana na neema alizotujaalia muumba ardhi na mbingu, bila ya fahamu kuwa viburi hivyo huturudia wenywe pale tufikapo kikomo.

Hatujui tulitendalo! linaweza kuwa jibu la haraka kwa wale wavivu wa kufikiri. Lakini nakataa kuwa ni hivyo, kwa maana viburi tuvifanyavyo huazimia kabisa na mara nyingine tunatenda mchana kweupeee!!

Leo nimeamua kutoa mfano mdogo kabisa juu ya uwezo wa Mungu na udhaifu wa mwanaadamu. Kula: Naam hatuna ujanja katika hilo, juu ya viburi vyetu vyote na haraka ya kuhangaikia maisha lakini lazima tutafute kula. 

Husemwa njaa haina mjanja wala mwamba. Lakini tumejifunza nini katika tukio hilo ambalo tunaonekana kulizoea tu kuwa lazima tule; umepata kujiuliza halafu ya kula ni nini, kulala? Ama kuzidisha maasi kwa Mungu aliekujaalia baraka ya kupata kula.

Tazama, unaweza kuwepo katika shughuli iwe harusi au msiba, lazima katika ratiba kutakuwepo muda wa kula. Hudhani wanaadamu ni dhaifu kwa alietuumba na ndiyo maana hatuwezi kujizuia kula? Mpaka sasa umechukua uamuzi gani kumshukuru muumba wako kwa kukujaalia neema hiyo ya kupata kula.

Kwa maana nusu ya maisha yetu tunayatumia kutafuta kula. Madhambi mengi yanasababishwa na harakati za kutafuta kula. Magomvi na usaliti husababishwa na harakati ya kutafuta tonge. Umepata kutenga muda na kufikiri kuhusu hili?

Tumeamrishwa na dini kufanya ibada, lakini ibada yenye utulivu ni ile ifanywayo na kiumbe alieshiba, kwa maana huaminika katika dini kuwa kiumbe alieshiba ana utulivu wa nafsi. Mungu anasema ‘kuleni na kunyweni kisha mumuabudu aliewaumba.’

Hudhani kula pia ni ibada. Lakini tunakula kwa ibada kweli? Mimi na wewe tunapaswa kulijibu swali hili kwa mifano ya maisha halisi tunayoishi. Je tunakula ili tuishi ama tunaishi ili tule.

Dini iliyo na ukamilifu ya kiislamu inasema, mja anapokula hapaswi kushiba sana bali kiwiliwili chake kinapaswa kipate nguvu tu. Kwani kushiba sana huleta uvivu na maradhi; na pia haifai kulakula kila wakati kwani nako huleta maradhi na uvivu. Umelizingatia hilo?

Nchi zilizoendelea sasa zinapigana na ulafi usio na msingi, maana wananchi wake wamevimbiana na miili kupata maradhi ya mara kwa mara. Sukari, moyo, cholesterol, shinikizo la damu na saratani yamekuwa ni maradhi yaletwayo na kula hovyo. Umelizingatia hili?

Hatuwezi kuepuka kula, hata tuwe na nguvu kiasi gani. Hapa pana hekima kubwa sana na mazingatio kwa wenye akili. Umelizingatia hili?
 

Friday, December 10, 2010

Kuna walioumiza vichwa kuleta UHURU, tusiubeze.



Na Hafidh Kido

Kila ifikapo tarehe kenda ya mwezi Disemba, tunasherehekea uhuru wa Tanganyika, uliopatikanwa mwaka 1961, kutoka kwa waingereza. 

Wengi tuliozaliwa baada ya uhuru tumekosa dhana ya kupiganiwa uhuru, hatulewi maana ya uhuru, hatujui thamani yake. Kifupi wengine hutamani ukoloni ungerudi.

Nadhani hii hutokana na madhila ya maisha mabaya yanayodhaniwa kuwepo baada ya wazungu kuihama ardhi yetu takatifu. Elimu duni, huduma mbaya za afya sambamba na maradhi yasiyoisha bila kusahau umasikini uliokithiri.

Utaona ni afadhali tungeendelea kutawaliwa. Ila hilo ni wazo la kijinga kabisa kwa mwenye akili, laiti ungepata bahati ya kuzaliwa miaka mia moja iliyopita na kuona namna waafrika walivyonyanyasika katika ardhi yao sijui kama mawazo yako yangefanana na ya sasa. Sijui kama ungetamani hata kuwaona hawa watu weupe na macho yao makali kama mwanga wa tochi; hawakuwa na huruma hata kidogo.

Nakumbuka bibi yangu aliefariki miaka ishirini iliyopita mimi nikiwa mdogo, ukitaja wazungu hasa wajerumani, alificha kichwa chake kifuani huku akilaani kwa lahaja yake ya kimtang’ata ‘kawatajwa hao jamani msiwatajeeee!! Kwani mwawataja kina kingi joji?’ alilaani vikali.

Unadhani ni nini kilichomfanya kulaani na kuogopa? Ni namna wazungu walivyowanyanyasa waafrika katika ardhi yao wenyewe. Hakika hata mimi sitamani wazungu warudi tena ingawa nimezaliwa miaka ya thamanini.

Mwalimu wangu wa ‘Photo Journalism’ Ramadhan Tonge, alipata kuniasa nisiwe na mawazo kama hayo ya kutamani uhuru usingepatikana. Alinambia kipindi chao huduma muhimu kama elimu, afya lishe na usafiri zilitolewa kwa ubaguzi. Kuna baadhi ya maeneo nchini ambayo wazungu walikaa, waafrika hawakuruhusiwa kufika; ukipita tu unakamatwa ama kufunguliwa mbwa.

Sasa kijana mwenzangu tafakari, ndani ya nchi yako mgeni anakuchagulia maeneo ya kupita, darasa la kukaa, zahanati ya kuenda ama huduma nyingine muhimu? Mgeni akuamulie mustakabali wa maisha halafu unasema bora hivyo wazungu wangekuwapo kuliko sasa tupo huru, lazima kichwani kutakuwa na mushkeli.

Turudi katika historia kidogo, bwana C.M.F Lwoga, katika kitabu ‘Uhuru wa bendera,’ ukurasa wa saba anasema, “Ukoloni ambao ni utawala wa mabavu ulioikumba Afrika…. Kiini chake kilikuwa ni ubeberu wa mataifa ya Ulaya.”

Mwandishi anaendelea kueleza “Kuvamiwa na kutawaliwa kwa nchi za kikoloni kulitokana na nchi hizo za Ulaya kutafuta malighafi kwa ajili ya viwanda vyao. Vilevile makoloni yalikuwa ni masoko ya kuuzia bidhaa zilizokuwa zikitengenezwa katika viwanda vyao nchi hizo za Ulaya.”

Hapa muandishi anajaribu kufichua siri ya ukoloni, kwa wale waliosoma historia hawapati tabu kuling’amua hili. Kwa maana wazungu walikuwa masikini na sisi matajiri, tatizo hatukuwa tukijua kuutumia utajiri wetu; na hata sasa hivyo ndivyo ilivyo. Walichofanya ni kuja kutughilibu na kufanya mabadilishano. Sasa sisi tunaonekana masikini na wao matajiri.

Badala ya kuamua inatosha kunyanyasika na tuwawajibishe viongozi walafi wanaoturudisha nyuma, Mtanzania mwenye shahada ya chuo kikuu anatamani kutawaliwa na mzungu. Hataki kuwa huru. Hapa pana shaka. 

Nchi yetu ni ya kijamaa, na katiba inatamka hivyo; kwanini tusitumie Azimio la Arusha kuwabana viongozi wetu ili tufaidi matunda ya uhuru badala ya kuendelea kutamani kutawaliwa na wazungu huku tukiubeza UHURU?

Hayati Mwalimu Nyerere, alipokuwa akizungumzia Ujamaa na dhana ya uhuru aliandika “Wakati tunapoyakataa mawazo ya kibepari yaliyoletwa katika Afrika na ukoloni, lazima vilevile tukatae na utaratibu wa kibepari ulioleta mawazo hayo……… sisi waafrika ardhi siku zote ilijulikana kuwa mali ya umma.
“Kila mtu katika kijiji alikuwa na haki ya kutumia ardhi, maana bila ya hivyo hakuwa na njia ya kupata riziki yake; na haiwezekani mtu awe na haki ya kuishi bila ya kuwa na haki ya kupata njia za kutafuta riziki.” (Ujamaa, Julius K. Nyerere, uk 6-7).

Hapa Mwalimu, alikuwa anajaribu kuwafungua masikio vijana wasomi na viongozi waliokuwa wakiukumbatia ubepari ambao ni moja ya mazao ya ukoloni. Uhuru wetu uliandamana na misemo mingi, miongoni mwao ni ‘Uhuru na kazi’. Vijana wa sasa wanalalamika sana kuwa uhuru haujawanufaisha lakini ukiwauliza wamezifanyia nini nafsi zao, si nchi! maana watakujibu si kazi yao; nafsi yake tu ameshindwa kuitendea haki. Sasa utamsaidiaje mtu huyo?

Mwalimu anaendelea kuasa katika kitabu cha Ujamaa, ukurasa wa 3-4, “Ujamaa ni kuhakikisha kwamba wale wanaopanda wanavuna mavuno ya haki ya yale wanayopanda.”

“kujilimbikizia mali kwa sababu ya kujipatia mamlaka au hadhi si mawazo ya ujamaa. Katika nchi ya namna hiyo mali inawaharibu mioyo wale wanaoipata. Mali inawapa hamu ya kuishi kwa raha zaidi kuliko wenzao,” anasisitiza.

Lazima viongozi wetu wafuate ahadi za viapo vyao vya kuilinda katiba ambayo ndani yake inaamini katika ujamaa. Hii itasaidia nchi yetu kufaidi utajiri tulionao na kurudisha imani ya vijana ambao walio wengi hawajui taabu na matatizo waliyopata mababu zetu kwa kutawaliwa. Ni hali mbaya sana kufikia mwanaadamu kutamani kutawaliwa.

Jambo muhimu katika suala la mabepari kutafuta mali ghafi katika makoloni ieleweke kuwa mali ghafi hiyo ilibidi ipatikane kwa gharama ndogo ili kuwawezesha  kujipatia faida kubwa. Waafrika walilazimishwa kufanya kazi kwa mabepari wakilipwa ujira mdogo, au kuwalazimisha walime mazao ya biashara ambayo yalinunuliwa kwa bei ndogo.

Kwa maana nyingine sisi tulinyonywa, hatukupewa elimu, huduma za afya wala miundo mbinu kwa faida yetu kama Tanganyika huru ifanyavyo sasa. Ingawa maisha ni mabaya, lakini tupo huru. Usipofanya kazi huli; ila kipindi cha ukoloni usipofanya kazi unakamatwa kwa kutolipa kodi ya kichwa.

Barabara, reli na bandari vilijengwa ili kupata urahisi wa kusafirisha malighafi ulaya, na wao kupata urahisi wa kuitembea Tanganyika. Huduma za kiafya hazikuwa za kutunufaisha sisi, bali ni wao wenyewe; utakumbuka hata wale manamba waliokuwa wakilima mikonge walipoumia kazini hawakupelekwa kwenye hospitali za wazungu. 

Huduma za elimu zilitolewa kwa lengo la kumfanya mwafrika ajue kuandika na kusoma; haikuwa kumwamsha toka ujingani.Na ndiyo maana majengo ya shule yalitofautiana. Shule na Hospitali ziligaiwa wazungu peke yao, wahindi peke yao na waafrika waliwekwa na waarabu. Matabaka haya tutayakubali sisi tunaokebehi uhuru?

Mwandishi Lwoga,wa kitabu ‘Uhuru wa bendera’ anaeleza, “Matokeo ya kuvamiwa kwa nchi na kutawaliwa na wakoloni ni kuwa nchi hizo zilizotawaliwa zilipoteza kitu muhimu sana katika historia ya maendeleo ya binadamu. Kitu hicho ni UHURU.” Uk. 6.

Sasa ninachojaribu kuieleza jamii ni kuwa, hapa hatutetei serikali za kiafrika kwa unyonge wanaowasababishia wananchi wake mpaka wakatamani kutawaliwa na weupe. Ila ni kutaka kuiondoa ile dhana ya kuwa uhuru hauna faida yoyote, hakika hiyo ni laana na kukosa hekima. Ni sawa na mfungwa anaeachiwa huru na kuamua kuwaaga wafungwa wenzie kuwa ‘kirago hiki asilalie mtu nitarudi muda si mrefu’ na kweli baada ya wiki anaiba tena anarudishwa gerezani.

Haipendezi kuwa na fikra mgando namna hiyo, lazima ionekane tofauti ya binaadamu na mnyama. Tufikiri kuwa huru, na baada ya hapo tutafute namna za kutoa huduma katika nchi yetu ili uhuru ulete maana.

Tufahamu kuwa hata hizi fikra tulizonazo za kusema heri tusingepata uhuru, au mtu anasema tunashereheKea uhuru gani hali nchi ipo gizani, maji ya taabu na mafisadi wamejaa. Lakini haya yote ni mazao ya kutawaliwa, hatujiamini tena ule ukomavu waliokuwa nao mababu zetu kama kinjekitile Ngwale, chifu Mkwawa na chifu wa Kiyao, Machemba aliewaandikia barua wajerumani kuwajibu ujinga wao, ushujaa huo hatunao tena. Bali tunalalamika tu, madomo kaya.

Chifu Machemba, wa Uyao mnamo mwaka 1899 alimwandikia barua Wissman, aliekuwa Gavana wa Ujerumani, Tanganyika. Alimjibu baada ya Wissman kumtaka Machemba ajisalimishe kwa utawala wa kijerumani.

Majibu ya Chifu Machemba yalikuwa kama ifuatavyo:

“Sioni sababu yoyote ile ya kukutii wewe. Iwapo nia yako ni kutaka urafiki, vema niko tayari, leo na siku zote. Lakini kamwe sikubali kuwa chini ya himaya yako. Iwapo nia yako ni kupigana, vema pia, niko tayari. Lakini siwezi kamwe kuwa raia wako. Mimi ni Sultani katika nchi yangu hii, na wewe ni Sultani huko kwenu ulikotoka. Lakini sijakuambia kuwa unitii mimi, kwa sababu nafahamu kuwa wewe ni mtu huru. Sitakuja huko, kama una nguvu, hebu njoo basi unichukue.”

Hayo ni majibu ya mwafrika halisi mwenye fahari ya kuwa huru na kuwa tayari kuulinda uhuru hata mbele ya silaha kali. Lakini sisi tunataka kujirudisha katika ukoloni kilaini kama mbuzi amuonapo chatu.

Hivyo kama hukuchangia kupatikana kwa uhuru, tafadhali ulinde uhuru wako kwa vitendo na maneno ya kishujaa. Tusibweteke kwa kulalamika, tufanye kazi ili kuonyesha nia ya kuendelea. Wazungu hawana nia ya kutusaidia bali wanataka kutunyonya tena. Wanatutamani kutupata kama leo.


Wednesday, December 8, 2010

hakuna roho kongwe, kila mmoja anataka kupendeza.

katiak maisha usikate tamaa. nani alijua kikwete atakua Rais?

fitina


Fitina husumu mwili, viwili kuwa kimoja
Tena hudhuru akili, ukajawa na mauja
Siijui yake asili, ya kuondoka na kuja
Ila fitina si rafiki, iepuke kama njaa

Fitina jumba la magomvi, na kila namna balaa
Mazao yake uchimvi, na midomo kushupaa
Wengi wapenda ujuvi, fitina ndo yao idhaa
Ila fitina si rafiki, iepuke kama njaa
 Hafidh Kido (toto la bakungwi)