Monday, April 4, 2011

Kuna tofauti gani kati ya Elimu na Hekima?


Na Hafidh Kido

Dunia imefanywa kuwa uwanja mkubwa wa kila nakama na amali zinazosaidia maisha kuendelea ima kwa taabu au mafanikio. Mungu akaamua kuwapa wanaadamu maarifa ya kuweza kuyamudu mazingira ya kidunia baada ya baba yetu kuasi huko mbinguni na kutupwa ardhini kutiwa adabu.

Maisha yana changamoto nyingi sana, baba yetu Adam, ndie anaesadikiwa kuwa ni kiumbe pekee aliepata kuishi duniani na kuwa na elimu nyingi akifatiwa na nabii Hidhri alietajwa katika visa vya Mtume Mussa.

Nae nabii Suleiman, anasadikiwa kuwa ndie mwanaadamu aliepata kuwa na hekima sana. Lakini umeshawahi kujiuliza tofauti ya hekima na elimu ama ufanano wao?

Mungu, mwingi wa rehema baada ya kugundua maisha ya duniani ni magumu kuishi, na kumtuma kwake mwanaadamu kuja kuishi duniani ingekuwa ni hatari na taabu aliamua kumpa maarifa ili aweze kuitawala dunia. 

Kwa kuwa awali hakukuwa na utaratibu wa elimu tuliyonayo sasa Mungu alishusha ‘ilhaam’ ama maono kwa wateule wachache na kuwaamuru wasambaze elimu ama hekima hiyo aliyowapatia.

Leo tuna vyuo vingi, shahada na mavyeti ya kila taaluma yanatolewa kwa wasomi wetu; lakini dunia imekuwa mahala pagumu kuishi kuliko zama ambazo hakukuwa na vyuo hivi vinavyosadikiwa kutoa elimu. Kuna kitu kinakosekana. Hekima.

Naam tuna wasomi wengi lakini hawana hekima juu ya usomi wao, matokeo yake hawazitumii elimu zao kusaidia kuondoa matatizo katika jamii zilizowazunguka na hata majirani zao.

Tofauti ya elimu na hekima ni kuwa elimu unaipata darasani ama kwa kukaa karibu na mwenye elimu ukaiga aina ya maisha anayoishi ama kwa kusoma maandiko yake. Lakini hekima haipatikani darasani wala kwa kusoma maandiko, bali hekima hutoka kwa Mungu ama kwa kukaa karibu na mwenye hekima akakukuza katika mwenendo huo.

Na ndiyo maana ukiona mtu anafanya mambo ya ajabu yasiyokubalika katika jamii, ni mara moja mtu kuuliza huyu ametoka wapi, wa ukoo gani huyu, kabila lake ama wazazi wake ni watu wa wapi, na vitu kama hivyo. Na baada ya hapo ndipo yanapokuja masuala kama kiwango cha elimu na aina ya kazi ama kipato, ingawa vina uhusiano mdogo sana na tabia ya mtu ama hekima.

Elimu ni neno la kiarabu lililochopolewa na kuingizwa katika lugha ya Kiswahili: msingi wake ni neno ‘Ilmu’kwa lugha ya kiarabu. Ikimaanisha ufahamu wa kuyajua mazingira ama utaalamu juu ya suala fulani la kijamii.

Mtaalamu ni neno pia lililotokana na lugha ya kiarabu lenye maana mtu alieelimika ‘ataalim’ alieelimika. ‘El- alaamaa’ mwenye elimu kuu ama mkufunzi.

Hivyo uwiano wa elimu na hekima ni wa karibu sana, na ndiyo maana katika dini ya kiislamu hekima ni muhimu kwa wanazuoni. Huwezi kuwa mkufunzi wa masuala ya dini ya kiislamu kama hauna hekima.

Hekima pia ni neno lililotokana na lugha ya kiarabu lenye maana ya mtu mwenye kujua hukumu ya mambo. Wale watu waliosoma ‘fiqhi’ ama maulamaa wenye kuweza kutoa fatwa ‘hukumu’ ni lazima wawe na hekima.

Hivyo ili uitwe mwenye elimu ‘ataalim’ ni lazima uambatane na hekima. Na ndiyo maana wasomi wa shahada ya uzamivu (PHD) ‘Doctor of Philosophy’ ni lazima watunukiwe cheo cha heshima cha ‘professor’ pale anapoonyesha hekima ya hali ya juu katika taaluma yake.

Ama kiongozi wa kijamii kama Rais, Waziri ama mtu yeyote anaefanya maamuzi yake ya kuisaidia jamii kwa kutumia hekima, vyuo vikuu huamua kumtunukia shahada ya uzamivu (PHD), kama ishara ya kutambua hekima yake aliyoitumia katika kutatua matatizo ambayo wao kama wasomi yalikuwa yakiwasumbua na walishindwa kuyatatua.

Hapa pia naomba niweke wazi: kuna tofauti kubwa kati ya msomi na mwenye elimu. Msomi ni Yule ambae anajishughulisha kutafuta elimu- anaweza aipate hiyo elimu ama laa. Anaweza pia kuwa alishahitimu vyuo kadha kwa kusoma, lakini hawezi kuwa ni mwenye elimu.

Ila mwenye elimu: ni Yule ambae ameshasoma ama bado anasoma lakini athari zake katika jamii zinaonekana. Anaweza kutoa maamuzi ambayo jamii nzima yananufaika kwayo. Lakini msomi anaweza kuwa mtu yeyote tu ambae amepitia vyuoni na kutunukiwa vyeti lukuki.

Mfano mzuri katika vyuo vikuu vyetu vya sasa, tunao wasomi maelfu kwa malaki, ambao wanahitimu na ambao bado wanaendelea kusoma. Lakini wameisaidia vipi jamii kwa usomi wao. Mara nyingine hata hawajaelewa walichokuwa wakikisomea kwa maana walitaka jamii tu ijue kuwa nao wapo vyuoni.

Ila wenye elimu ni wachache, ambao wanajitahidi kuzitumia elimu zao kufundisha wengine ama kufanya mambo yatakayosaidia jamii zao kupiga hatua.

Je, tunaweza kutofautisha baina ya elimu na hekima? Nadhani ni sawa na kusema gari na mafuta, ni vitu ambavyo havikimbiani vinategemeana kila kimoja kinamuhitaji mwenzie.
Naomba kuwasilisha.

No comments:

Post a Comment