Sunday, November 7, 2010

ujana tuutumie vizuri



Na Hafidh Kido

Ujana ni kitu azizi sana, walipata kusema washairi wa zamani. Unaonaje mwanaadamu aliejawa siha, sura jamali na kiwiliwili kilichoshikamana kwa afya na furaha ya uzima; maradhi huwa ni kitu kigeni katika jumba la mwili wa kijana huyo. Ajabu akidi.
Lakini ujana hulemaza akili mwanadamu akasahau lengo la kuumbwa, ile furaha ya kuchekewa na kupendwa kila apitapo humpumbaza kijana akadhani dunia ni yeye na hakuna mwengine; makosa makubwa ajabu.

Tazama mzee aliepinda mgongo kwa kula chumvi nyingi namna anavyotamani kurudisha siku nyuma na kutenda matendo mema ili uzee wake upungue mashaka. Hudhani hata yeye alikua kijana kama wewe na sasa mate yamekuwa machungu na macho kufanya kiwi hajui tofauti ya mchana na usiku. Kama ni mwanamke zile nywele alizokuwa akizitunza kwa gharama kuu sasa ni kama mkonge uliokosa rutuba katika konde dhaifu la kichwa cha kizee huyu..

Mtu aliekuwa akiitwa na vijana wenye uchu na ubazazi kutokana na uzuri wake lakini leo hii hata kutazamwa hatamaniki; hudhani ni huzuni ya nafsi yako kuwa katika hali hii ikiwa sababu ni kuutumia vibaya ujana wako?

Jiulize ni mara ngapi umepata kukutana na mtu wa makamo mwenye umri mkubwa tofauti na muonekano wake. Jibu unalopata ni kuwa alijitunza vema alipokuwa kijana, fahari iliyoje hii. Huoni haya kujidhuru mwili kwa furaha ya muda mfupi hali utakuja kutaabika kwa muda mrefu pindi upindukapo miaka hamsini tena bila ya msaada wa ndugu wala watoto uliowazaa mwenyewe na kuwalea kwa taabu kuu.

Mawe!! Hakuna jibu muafaka la maswali yote hayo bali kuwa makini kwa kila nukta ya tamko litokalo kinywani mwako, kuzingatia kila angalio la ubaya ama uzuri kwa jirani au mtu baki, kuwa mbali na chuki na kila dhiki uzibebeshazo moyo mteke wa kiumbe cha Mungu. Hakuna tahadhari njema kama kuulinda moyo wako na mabalaa ya dunia; macho hutazama, ulimi hutamka na miguu ikafuata, ila balaa lolote litakalosababishwa na viungo vyote hivyo mbebaji ni moyo.

Chunguza kisigino kinapopata ajali ya kudungwa na nyigu au msumari, lakini maumivu hupenya mpaka kwenye moyo pakatokea mpasuko wa uchungu kama radi isiyoambatana na mvua. Moyo huzeeka haraka na ukajiinamia kutokana na rabsha za dunia wewe mmiliki uutwishwazo, ni adhabu ya kijinga uupao moyo kwa tamaa za muda mfupi na upungufu wa tahadhari.

Husemwa kwa mwerevu huenda kilio, lakini kinyume chake ni kicheko, hudhani kilio hudumu muda mwingi kuliko kicheko? Kwanini usichague kicheko ili uache kuwa na huzuni kwa muda mwingi? Maana huzuni hutafuna mwili mithili ya panzi atafunavyo jani la mbono.
Najaribu kuwavuta vijana ili wawe pamoja nami katika makala haya kwa lengo la kuondoa chuki na hashuo la kukurupuka kulaumu pasi na kuelewa mada na mwandishi kalenga nini katika maandiko yake.

Wamasai husema ‘ukiona simba kazeeka ujue amekwepa mishale mingi’ na ndivyo ilivyo kwa mwanadamu, ukiona kijana amezeeka vizuri ujue alijilinda na kukwepa majaribu mengi katika ujana wake. Huamki tu kutoka usingizini na ukajikuta u mzee wa siha na furaha nyingi, mara nyingi wazee hutuhumiwa uendawazimu na matusi kila namna kwa kuwa tu hawapendezi tena katika jamii.

Utajisikiaje leo nawe unakuwa kama Yule kizee anaepita mitaani na kopo akiomba senti ya kula huku ngozi yake imesinyaa kama dagaa la ziwani, nguo zake zimefubaa kwa kukosa maji muda mrefu huku amepinda mgogo kwa machovu. Hutumia saa nzima kukatiza uwanja wa mpira kwa namna anavyopiga hatua fupi za machozu ya mzigo wa uzee, unadhani hana ndugu?

Nani amekwambia uzee ni adhabu; hatuzeeki ili tudharaulike katika jamii wala kupoteza mazuri yote tuliyoyafanya wakati wa ujana. Bali ni sisi wenyewe ndiwo tuandaao uzee wa mashaka kwa kutojali kesho yetu. Tuache kuishi leo, tukumbuke kuwa kuna  kesho na keshokutwa.

Uraibu tuutumiao sasa ni sumu ijirundikayo mwilini na huchamka pindi tuzeekapo. Ugoro, mirungi, pombe na zinaa ni sumu kali sana kwa afya za wanaadamu. Hasa vijana.
Tupunguze kulala sana kwani mwili uliozoea kukaa kaa huchoka haraka. Tuzidishe kufanya kazi ili tuwe na akiba itakayotufaa uzeeni, ndugu watuchukiao pindi tunapozeeka hali tu maskini ndiwo haohao wanaotutumia kwa ushauri na kutusikiliza kila tusemacho pindi tuzeekapo hali tuna kipato.

Hujapata kusikia watu huwaita wazee dawa? Lakini mara hiyohiyo jamii huwatusi wazee kwa kuwaambia wanazeeka vibaya na hawahitaji ushauri wao. Lakini inaaminika wazi kuwa  ukiutumia vibaya ujana wako kwa matumizi yasiyo na nidhamu hakika utazeeka masikini na jamii itakosa kukuheshimu.

Kitu kingine cha kuzingatia  ni aina ya vyakula tunavyokula, ni hatari sana kula sukari kwa wingi, mafuta na nyama kwa wingi huharibu siha. Kwa sasa utaona ni tamu na huleta hadhi, ila kwa baadae bohari ya maradhi utakayokutana nayo hakuna wa kumlaumu ila ni nafsi yako.

Mazoezi ni kitu muhimu sana kwa mwili wa kijana, kujibweteka tu ni mbaya sana; Misuli na moyo vinahitaji kushughulishwa ili vipate kufanya kazi kwa bidii na kuacha kufubaa.
Ushauri wa bure kwa vijana wenzangu ni kuzingatia kuwa uzee ni aibu pindi ukikujia wakati uliutumia vibaya ujana wako ima kwa kutojiandaa kifedha, kiafya na kielimu. Maana ni vema kuwa na elimu ili vijana wa baadae wapate msaada mkubwa toka kwako.

Tazama mzee alielala kitandani hana afya wala fedha, lakini ni aalimu mkubwa katika masuala ya utabibu, historia ama sanaa. Watu hupanga misururu ya mstari ili kumuona na kuvuna chochote toka kwake. Furaha iliyoje hii kuthaminika hata katika kitanda chako cha uzee unasubiri kifo.

Mfano mzuri ni hayati Mwalimu Nyerere, hakuwa na fedha wala afya katika kitanda chake cha kifo, lakini angalia msururu wa wasomi na watu wakubwa duniani namna walivyomuandama ili kupata chochote katika taaluma ya uongozi ili nao wanufaike kwacho.

Tujue ujana ni dhamana itaondoka baada ya miongo michache ya kujifaragua na majigambo. Na tutaishi katika dhiki na kukimbiwa hata na damu zetu tulizozizaa na kuzihangaikia kwa taabu nyingi. Hujasikia mtu anasuswa na watoto wake mwenyewe? Tena kwa kuitwa mzee wa nongwa……


No comments:

Post a Comment