Na Hafidh Kido
Unapotaja neno hasira kitu kinachokuja kwanza katika fikira ni maudhi na ukakasi wa hali awayo mtu anapokarahishwa na tukio, neno au hali fulani katika maisha tuishiyo ya karaha taabu na raha kidogo.
Hufurahisha kuona mtu anaweza kuhimili hasira zake, lakini pia simlaumu mtu anaeshindwa kuzuia hasira zake bali humuhurumia mtu namna hiyo. Kwa maana mpaka mja huamsha hisia zake za hasira inaonyesha ni namna gani ameshindwa kuvumilia kwa alilolishuhudia ama kulisikia dhidi yake.
Lakini husemwa jemedari ni Yule awezae kushinda kitali cha kupigana na moyo wake dhidi ya maudhi ya wanaadamu. Ikumbukwe kuwa tunaishi katika dunia ya mchanganyiko wa tabia na historia tofauti za maisha; hivyo kuudhiwa ama kutoelewana katika dunia ni kitu cha kawaida sana haifai kubeba kila uonacho na kukihifadhi moyoni kwa chuki na maudhiko.
Mara nyingine watu huona raha tu kukujaribu na kuona ni namna gani unaweza kughilibika na nafsi yako dhidi ya utani mdogo tu unaokera moyo; ni kawaida ya wanaadamu kufurahishwa na sura ya kutisha ya mtu alieudhika.
Ni busara kuhimili hasira zako ili watu wasione udhaifu ulionao pindi uudhikapo, nasema hivi kwa maana hasira humfanya mtu mwenye hadhi kuongea maneno mabaya yaliyo nje ya maadili mema katika jamii na kuiharibu heshima aliyoihangaikia kwa miaka mingi; pengine nusu ya maisha yake.
Marehemu Shaaban Bin Robert, alipata kusema kuwa ‘mtu anapoudhiwa ni vema ahesabu moja mpaka kumi,’ maana ya usemi huu ni kuwa unapoudhiwa usifanye papara ya kuwajibu wabaya wako au kutaka kuwaonyesha kuwa wewe ni nani kwao. Bali vuta subira. Na mara nyingi hasira ina tabia ya kupungua ipitapo kipindi fulani bila ya kutamka ama kutenda kitu.
Mambo mengi huharibika kwa kutendwa huku mtendaji akiongozwa na hasira ama chuki dhini ya nafsi yake. Ndiyo! mtu mwenye chuki hachukii ila huichukia nafsi yake.
Wanaadamu tumejiaminisha kuwa tunawachukia waliotutedea kinyume na tupendavyo, lakini bila kufahamu tunaudhika kiasi tunajidhuru wenyewe kwa kupata maradhi ya moyo; je huoni kuwa unaemchukia unazidi kumpa ushindi badala ya kumfanya ajutie alichotenda dhidi yako?
Angalia dereva alieudhiwa na mke wake nyumbani, huamua kuendesha kwa fujo akidhani anamkomoa aliemuudhi; matokeo yake huishia kuangusha gari ama kumpiga dafrau mpita njia na kupata hasara ya kumlipa mpita njia huyo. Badala ya kutatua tatizo moja bila ya kufahamu anaongeza matatizi juu ya tatizo moja ambalo lingemalizwa kwa kukaa chini na mkewe kumweleza namna alivyomkosea na kumtaka asirudie makosa hayo kwa maana hapendezewi nayo.
Naona unajiuliza ni namna gani utaweza kukaa mbali na hasira; ni rahisi.
Baada ya kuudhiwa na mtu awaye yeyote mdogo, mkubwa, rafiki au mtu baki, kitu cha kwanza kufanya ni kujiuliza kwa kuudhiwa huko maisha yako yatabadilika namna gani? Kitu gani kitapungua katika kipato, heshima au ukaribu na mtu aliekuudhi. Ukiona kipo kitakachopungua hakuna haja ya kumghadhibikia mja huyo bali ni busara kumuuliza ni kwanini ameamua kukufanyia hivyo hali anajua si jambo jema kwenu nyote.
Akikosa jibu muafaka la kukupa na bado akisisitiza kuwa alichotenda ni sahihi, basi kitu chema kufanya ni kutafuta watu ambao muovu huyo anawaheshimu ima kwa kuwa ni wakubwa wake kiumri au kicheo. Kwa kufanya hivyo utamsaidia yeye kujirekebisha ikiwa ni muungwana.
Lakini ukiona maudhi utakayopata hayatokuwa na madhara yoyote kwako ni vema kumuepuka muovu huyo kwa maana hakuna badiliko lolote litakalokupata kwa kumuepuka mtu huyo aso maana.
Waungwana husema ukimya ni silaha ishindayo mara zote. Hivyo inashauriwa kuitumia silaha hiyo mara nyingi iwezekanavyo.
Hivyo ni vema kujiweka mbali na hasira, kwa maana hakuna tunachonufaika kutokana nazo zaidi ya hasara ya kuharibu mahusiano na kazi zetu ama kudharaulika katika jamii.
No comments:
Post a Comment