Wednesday, November 3, 2010

fahari ya jioni inapoingia.


Na Hafidh Kido

Adhuhuri huchechemeza duara la jua na kuikaribisha alasiri yenye miali hafifu ya jua na burudiko la mchanganyiko wa joto na upepo mwanana kulingana na hali ya hewa  siku hiyo.
Jioni huingia baada ya mchekecho na mabishano mafupi baina ya jua na mbingu kuwa nani atawale wakati. Na ndiyo maana jioni inapoingia mawingu hutoa kilio na kuacha uwekundu uliosababishwa na athari ya kilizi cha jua kushindwa pale linapoamua kuondoka katika upande mmoja wa dunia.

Hali hiyo ya mabishano hutoa faraja kubwa kwa mwanadamu anaefuatilia kwa makini kitali hicho; hakika ni burudani isiyo kifani kushuhudia kuzama kwa jua. Macho hufanya nuru inayoakisiwa kutoka katika mbingu; rangi ya samawati iliyochanganyika na zari ipendezayo angani humaanisha kuisha kwa siku.

Waumini wa dini ya kiislamu wakati huo hushughulika kushika udhu ili kuingia katika sala ya magharibi kwa kumtukuza Muumba wa maajabu yote hayo. Shukurani nyingi humuendea muandisi wa ajabu hiyo ya kupendeza.

Mara nyingine watu hutoa viti vya uvivu nje  wakiwa  na vikombe vya kahawa wakishuhudia mandhari hayo mazuri ya kupendeza macho na kupumbaza akili, baada ya hangaiko la siku nzima katika jua kali la kutesa ngozi. Huwa ni kama sherehe ya kuliaga jua ili kuukaribisha mwezi na nyota zake wakia pulizo la upepo likizidisha raha hiyo ya magharibi.

Magharibi ni wakati muafaka kwa wapendanao kuandaa mandari yao au kwa wanagenzi wa mambo ya mahaba kuomba kutoka kwa kinywaji  au mlo wa pamoja na wawapendao. Nyakati hizi huwa kama uchawi namna zinavyopumbaza akili za watu. Maajabu mengi hutendeka.

Magharibi huvuta watu katika migahawa na masikani zenye mwanga hafifu mfano wa sumaku ivutavyo uchafu wa chuma na vitu namna hiyo. Utaona watu wamesimama wawiliwawili katika vipembe vya mitaa na viguzo vya umeme au visiki vya miti; hilo hudhihirisha ni namna gani wanadamu hunufaika na kiza. Maana mengi yashindikanayo kufanyika mchana huvugumizwa katika nyakati hizi.

Fahari ya magharibu hudhihirika pale mwanadamu anapozigugumia pesa zake alizozivuna kwa siku nzima. Wengine hunena ‘ponda mali kufa kwaja,’ lakini itaonekana ni msemo wa kipumbavu kabisa ikiwa unatumia usichoweza kukiingiza; ama unatumia nusu na robo ya ulichokichuma hali saa chache kutakucha na misukosuko ya kilimwengu itaanza upya usahau kama kulikuwa na magharibi usiku wa jana.

Ni jambo la kuchunga sana namna tuitazamavyo magharibi, maana ni wakati wenye ghiliba nyingi na vishawishi vya ajabu sana. Mara zote huwafanya watu wajute saa chache baada ya kuitumia vibaya magharibi yao; ujukuu wa majuto hudhihirika pale tu uamkapo kitandani huna senti hata moja hali mchana wa jana ulihangaika chini ya jua ukiitafuta hiyo shilingi kwa matusi, kedi na kila namna ya dharau za waajiri wabaya.

Chumo bora hupaswa kutumika vema na kwa uangalifu mzuri sana, ni faraja na fahari iliyoje kuweka akiba yako kwa manufaa ya baadae. Ni ushujaa mkuu kuipitisha magharibi kwa kinywaji kidogo ima ukiwa na familia au wenza wema watakaokushauri kurudi nyumbani kupumzika baada ya kukuona umeanza kupoteza utimamu katika maamuzi. Ama ni vema kuipitisha magharibi ukiwa nyumbani huku umeshikilia kikombe cha chai ukizungumza na mtoto wako mkiulizana habari za masomo na kumsaidia kazi za shule.

Ni ushujaa ulioje kuipitisha magharibi yako ukiwa jikoni na mumeo ama mkeo huku mkisaidiana kuandaa chajio kwa furaha na vicheko  mkitaniana. Huoni ni jambo jema kuonekana na watoto wenu mkiwa pamoja mkifurahi, maana hata wao hufarijika kuwaona wazazi wao katika hali hiyo.

Akili ya kawaida tu inatosha kufahamu kuwa mchana ulipita nyumba ikiwa tupu na kimya kama ganjo wakati wewe ukiwa kazini na watoto wakiwa shuleni; magharibi ama jioni imefanya tas-hila na msaada mkubwa kuweza kuwaweka pamoja watoto na wazazi, hivyo si busara baba kuiacha familia yako ikiwa pweke nawe ukatokomea kusikojulikana halafu baada ya saa nyingi unarejea nyumbai ukiwa umelewa, watoto wameshalala, mama amechoka kwa kukusubiri, chakula kimepoa na nyumba imepoteza nuru ya mkusanyiko wa familia. Si hali nzuri, hakika husikitisha.

Muumba ardhi na mbingu amezigawa nyakati na matukio ili iwe rahisi kwa wanaadamu kufanya mambo yao kwa ufanisi na utaratibu mkuu.

Asubuhi ni ya kujiandaa kulijenga taifa na watoto huenda shule ili kujizoeza kutenda matendo bora ya baadae na kujua mambo mapya ambayo ima walikuwa wakiyasikia lakini hawana uhakika nayo au ni mapya kwa maana ya upya, huyajua kwa mara ya kwanza ili yaje kuwasaidia katika umri uliobakia.

Mchana huwa ni wa kupumzisha akili baada ya kuisumbua kuanzia asubuhi ima kwa kazi ngumu au masomo yanayohitaji akili imara. Na ifikapo alasiri huwa ni wakati wa kurudi nyumbani na kuandaa ya magharibi.

Wengi huitumia alasiri kwa kusoma majarida, vitabu, kutembelea wagonjwa, ndugu au jamaa waliopotelewa na mtu kwa kuifariki dunia. Vijana wengi huenda pwani ya mito au bahari ili kuikabili kurasa nyeupe ya maji yaliyotuama. Ama hutembelea mabustani ya maua yenye harufu nzuri na laini kwa nyoyo zilizokufa;  Kufanya hivyo huwaburudisha nafsi na kupata akili mpya. 

Magharibi huwa ni wakati wa kurudi yumbani na kukaa na familia, kula au kunywa pamoja huku mkitazama luninga. Wengine ambao hawana familia huitumia magharibi kwa kutembelea sehemu za burudani ama hukaa tu na marafiki wakipiga soga.
Usiku unapoifunika dunia ni wakati wa kulala na kupata nguvu mpya ya kuikabili asubuhi yenye mikiki na vishindo vingi vya walimwengu.

Ni busara sana kulala mapema na kuamka mapema, na ni ukatili wa afya yako kuchelewa kulala na kuchelewa kuamka ama kuchelewa kulala na kuwahi kuamka. Kwa maana mwanaadamu amepangiwa saa za kila shughuli anayoifanya katika siku yake. Na kulala kumetengewa saa kumi katika saa ishirini na nne za siku nzima. 

Maana ikiwa tunashauriwa kulala mchana kwa saa mbili, na usiku kuanzia saa nne tuwe tumeshalala na asubihi ikifika saa kumi na mbili tuwe tumeshaamka. Sasa ukichanganya utagundua katika saa 24 tunapaswa kulala saa kumi. Na hizo saa kumi na nne zilizobaki tunatakiwa kuzitumia kwa ibada, kazi na kukutana na jamaa ima kwa kutembelea wagonjwa au kusaidia wahitajio msaada au kufunza na kujifunza vitu vipya katika dunia.
                                                     

No comments:

Post a Comment