Na Hafidh kido
Dunia imegubikwa na maudhiko mengi sana, asilimia kubwa ya maudhiko hayo husababishwa na aina ya marafiki tulio nao. Ni ngumu sana kujua yupi ni rafiki wa kweli na yupi si rafiki wa kweli, kwa maana hawajapigwa chapa usoni kuonyesha tabia zao za ndani.
Ubinafsi huchochea urafiki mbaya, waovu wengi huunguzwa na choyo, kujipendelea wao kwanza na chuki ya maendeleo ya jirani yake. Kukoma mambo hayo ni ngumu kama ardhi na mbingu kukutana.
Ajabu ya dunia huwezi kuepuka marafiki; kamwe haliwezekani hilo. Lakini ni vema kuchagua yupi rafiki na yupi ni mwandani wako. Angalia kwa makini maneno hayo mawili, rafiki na mwandani. Kuna fotauti kubwa sana kati ya hatua hizo za maisha.
Watu tumeumbwa ili tuishi katika jamii ya watu wengi, nafsi zetu ni dhaifu, ila Mungu muumba kila ajabu amejaalia nguvu fulani ikujiayo kila unapodhuriwa na urafiki mbaya. Nguvu hiyo huitwa SUBIRA; naam kusubiri ni ibada njema sana katika dunia ya ghanima nyingi, ina msaada wa ajabu usiomithilika.
Marafiki ni watu wa karibu tunaoishi nao katika jamii ama mkusanyiko wa watu. Inaweza mmezawa kijiji kimoja, mnasoma shule moja ama mnafanya kazi afisi moja. Wote ni marafiki zako, huwezi kuwaepuka hata kidogo. Lakini katika lundo hilo la marafiki lazima utakua na mmoja tu ama wawili ambao ni wandani wako, walipo wao ndipo ulipo wewe, wafanyalo wao ndilo ufanyalo wewe hamuepukani.
Mwandani wako ni kama ndugu, hamuachani na kila akengeukapo maadili si wewe tena unaemrekebisha bali jamii ndiyo inayomrekebisha kwa kumkumbusha ‘tazama mwenzako alivyo, tofauti na wewe umebadilika kabisa. Kwanini hufanyi kama afanyavyo rafiki yako?’ Nadhani umenielewa.
Tazama tunazawa sehemu mbali na kukulia sehemu mbali, tunasoma shule ya msingi hapa, na tunasoma sekondari sehemu yingine. Ama tunamaliza chuo kikuu sehemu moja na kufanya kazi sehemu nyingine. Kote huko unapoondoka unaacha lundo la marafiki, na huwezi kuwaepuka hata kidogo wamekuganda na ima watakuja kukusaidia au wao watahitaji msaada kwako. Ndivyo dunia ilivyo maajabu na vizugumkuti ni vitu vya kawaida sana.
Marafiki ni watu wazuri sana kuwa nao, kadhalika ni wabaya sana unaposhindwa kufaya wanachotaka. Siku zote wao wapo sahihi, hawakosei wala hawahitaji kurekebishwa; ukifanya lenye heri nao utasifiwa mpaka kizazi chako cha ishirini kilichopita, na ukiwakosea utatukanwa na kukumbushiwa maovu yako ya tangu utotoni. Ndivyo dunia inavyowatesa wanaadamu, ama inavyofanya wanaadamu watesane wao kwa wao.
Wapo marafiki ambao wanakujua pindi uwapo na shida, hao ni wazuri sana. Wapo marafiki wanaokuonya pindi unapopotea, wakumbatie sana marafiki hao usiwaache, wapo marafiki wanaokuvuta utoke kwenye shimo la hatari, wapende sana na ikiwezekana kawatambulishe kwenu.
Lakini wapo marafiki ambao wanasubiri upotee ndipo wakuseme, kaa mbali nao ila usiwatenge maana si kosa lao bali hawajiamini. Wapo marafiki ambao ukiwaambia ukweli hukasirika na pengine huiambia jamii wewe ndie mbaya maana unamzulia mambo asiyo nayo, rafiki huyo muepuke baki kumpa salamu tu lakini si siri zako. Wapo marafiki ambao hukufata pindi wawapo na shida tu, ni vema wasaidie, ila unapogundua wewe ukiwa na shida wanakuepuka huna budi kuwaepuka nao.
Msomaji usione hawa marafiki ni ni watu waishio dunia ya peke yao, bali tumo nao humuhumu pengine mmoja wao ukiwa wewe au mimi mwandishi. Maana kama tukisema kuna marafiki wabaya kila mmoja atasema mimi si mmbaya, husemwa nyani haoni kundule.
Ukimnyooshea mtu kidole kimoja jua vilivyobaki hukurejelea wewe, hakuna wa kumfunga paka kengele ila muandishi anajaribu kuiasa jamii tuwe marafiki wema kwa marafiki zetu.
Wewe ukiwa mwema na Yule akipendezewa na wema wako basi dunia itakua ni mahala salama na bora pa kuishi. Lakini kila mmoja akisema Yule ndie mmbaya, basi sote tutakua wabaya. Ikiwa unamnyooshea Yule hata nae anamnyooshea Yule ambae ni wewe. Umeona mkanganyiko huo?
Anza kubadilika sasa, kuwa rafiki mwema ili rafiki yako nae awe mwema. Maana urafiki mmbaya huzaa chuki, magomvi na hasada kubwa katika dunia. Ulimwengu umeshakinai vurugu zisababishwazo na urafiki mbaya, ardhi imeelemewa na damu imwagwayo kwa urafiki mmbaya.
Huoni kidole chako ukikitumia vyema kuziba tundu imwagayo damu kwa urafiki mbaya itasaidia kizazi chetu kiishi katika mazingira bora?kuliko kidole hicho kukitumia kuwanyooshea marafiki wabaya, ambapo bila kutazamia hata wewe hunyooshewa. Badilika, anza sasa kumkumbatia rafiki uliekosana nae.
Neno dogo sana la kuomba radhi huweza kubadilisha jambo kuu kama dharau, chuki na hasada. Hukuchukua sekunde chache sana kusema ‘SAMAHANI’ lakini bila ya kutambua itakuchukua miaka mingi sana kuhuzunika, kutaabika na kukosa amani kwa kushindwa kuzitumia hizo sekunde chache za kusema samahani ama kuomba radhi. Naomba kuwasilisha…
No comments:
Post a Comment