Sunday, November 28, 2010

Jaribu kuwa rafiki bora uibadili Dunia.



Na Hafidh kido

Dunia imegubikwa na maudhiko mengi sana, asilimia kubwa ya maudhiko hayo husababishwa na aina ya marafiki tulio nao. Ni ngumu sana kujua yupi ni rafiki wa kweli na yupi si rafiki wa kweli, kwa maana hawajapigwa chapa usoni kuonyesha tabia zao za ndani.
Ubinafsi huchochea urafiki mbaya, waovu wengi huunguzwa na choyo, kujipendelea wao kwanza na chuki ya maendeleo ya jirani yake. Kukoma mambo hayo ni ngumu kama ardhi na mbingu kukutana.

Ajabu ya dunia huwezi kuepuka marafiki; kamwe haliwezekani hilo. Lakini ni vema kuchagua yupi rafiki na yupi ni mwandani wako. Angalia kwa makini maneno hayo mawili, rafiki na mwandani. Kuna fotauti kubwa sana kati ya hatua hizo za maisha.

Watu tumeumbwa ili tuishi katika jamii ya watu wengi, nafsi zetu ni dhaifu, ila Mungu muumba kila ajabu amejaalia nguvu fulani ikujiayo kila unapodhuriwa na urafiki mbaya. Nguvu hiyo huitwa SUBIRA; naam kusubiri ni ibada njema sana katika dunia ya ghanima nyingi, ina msaada wa ajabu usiomithilika.

Marafiki ni watu wa karibu tunaoishi nao katika jamii ama mkusanyiko wa watu. Inaweza  mmezawa  kijiji kimoja, mnasoma shule moja ama mnafanya kazi afisi moja. Wote ni marafiki zako, huwezi kuwaepuka hata kidogo. Lakini katika lundo hilo la marafiki lazima utakua na mmoja tu ama wawili ambao ni wandani wako, walipo wao ndipo ulipo wewe, wafanyalo wao ndilo ufanyalo wewe hamuepukani.

Mwandani wako ni kama ndugu, hamuachani na kila akengeukapo maadili si wewe tena unaemrekebisha bali jamii ndiyo inayomrekebisha kwa kumkumbusha ‘tazama mwenzako alivyo, tofauti na wewe umebadilika kabisa. Kwanini hufanyi kama afanyavyo rafiki yako?’ Nadhani umenielewa.

Tazama tunazawa sehemu mbali na kukulia sehemu mbali, tunasoma shule ya msingi hapa, na tunasoma sekondari sehemu yingine. Ama tunamaliza chuo kikuu sehemu moja na kufanya kazi sehemu nyingine. Kote huko unapoondoka unaacha lundo la marafiki, na huwezi kuwaepuka hata kidogo wamekuganda na ima watakuja kukusaidia au wao watahitaji msaada kwako. Ndivyo dunia ilivyo maajabu na vizugumkuti ni vitu vya kawaida sana.

Marafiki ni watu wazuri sana kuwa nao, kadhalika ni wabaya sana unaposhindwa kufaya wanachotaka. Siku zote wao wapo sahihi, hawakosei wala hawahitaji kurekebishwa; ukifanya lenye heri nao utasifiwa mpaka kizazi chako cha ishirini kilichopita, na ukiwakosea utatukanwa na kukumbushiwa maovu yako ya tangu utotoni. Ndivyo dunia inavyowatesa wanaadamu, ama inavyofanya wanaadamu watesane wao kwa wao.

Wapo marafiki ambao wanakujua pindi uwapo na shida, hao ni wazuri sana. Wapo marafiki wanaokuonya pindi unapopotea, wakumbatie sana marafiki hao usiwaache, wapo marafiki wanaokuvuta utoke kwenye shimo la hatari, wapende sana na ikiwezekana kawatambulishe kwenu.

Lakini wapo marafiki ambao wanasubiri upotee ndipo wakuseme, kaa mbali nao ila usiwatenge maana si kosa lao bali hawajiamini. Wapo marafiki ambao ukiwaambia ukweli hukasirika na pengine huiambia jamii wewe ndie mbaya maana unamzulia mambo asiyo nayo, rafiki huyo muepuke baki kumpa salamu tu lakini si siri zako. Wapo marafiki ambao hukufata pindi wawapo na shida tu, ni vema wasaidie, ila unapogundua wewe ukiwa na shida wanakuepuka huna budi kuwaepuka nao.

Msomaji usione hawa marafiki ni ni watu waishio dunia ya peke yao, bali tumo nao humuhumu pengine mmoja wao ukiwa wewe au mimi mwandishi. Maana kama tukisema kuna marafiki wabaya kila mmoja atasema mimi si mmbaya, husemwa nyani haoni kundule.
Ukimnyooshea mtu kidole kimoja jua vilivyobaki hukurejelea wewe, hakuna wa kumfunga paka kengele ila muandishi anajaribu kuiasa jamii tuwe marafiki wema kwa marafiki zetu.

Wewe ukiwa mwema na Yule akipendezewa na wema wako basi dunia itakua ni mahala salama na bora pa kuishi. Lakini kila mmoja akisema Yule ndie mmbaya, basi sote tutakua wabaya. Ikiwa unamnyooshea Yule hata nae anamnyooshea Yule ambae ni wewe. Umeona mkanganyiko huo?  

Anza kubadilika sasa, kuwa rafiki mwema ili rafiki yako nae awe mwema. Maana urafiki mmbaya huzaa chuki, magomvi na hasada kubwa katika dunia. Ulimwengu umeshakinai vurugu zisababishwazo na urafiki mbaya, ardhi imeelemewa na damu imwagwayo kwa urafiki mmbaya. 

Huoni kidole chako ukikitumia vyema kuziba tundu imwagayo damu  kwa urafiki mbaya itasaidia kizazi chetu kiishi katika mazingira bora?kuliko kidole hicho kukitumia kuwanyooshea marafiki wabaya, ambapo bila kutazamia hata wewe hunyooshewa.  Badilika, anza sasa kumkumbatia rafiki uliekosana nae.

Neno dogo sana la kuomba radhi huweza kubadilisha jambo kuu kama dharau, chuki na hasada. Hukuchukua sekunde chache sana kusema ‘SAMAHANI’ lakini bila ya kutambua itakuchukua miaka mingi sana kuhuzunika, kutaabika na kukosa amani kwa kushindwa kuzitumia hizo sekunde chache za kusema samahani ama kuomba radhi. Naomba kuwasilisha…

mapenzi ni maonevu?

Na Hafidh Kido

Tumekuwa walalamishi wakubwa juu ya wapenzi wetu kutukosea adabu, tunalaumu kuwa ni wenye kutoka nje ya makubaliano. Mara nyingi sababu huwa ni sisi kutozingatia alama za nyakati na namna tulivyokutana na mwenzi wetu.

Kuzingatia mazingira mliyokutana na mwenzi wako ni jambo muhimu katika mahusiano na mustakabali wenu; lakini wanaadamu tumekuwa tukilalamika kuwa hali imekua mbaya sasa tofauti na zamani, hali zamani ndiyo iliyokuharibia sasa. Mapenzi hupangwa mustakabali wake siku ya kwanza tu mnapoanza mahusiano, kinachosubiriwa ni hatma na sababu ya kuachana ama kugombana.

Tumekuwa tukitembelea wataalamu wa saikolojia juu ya mafarakano yetu, lakini husemwa mapenzi hayana ufundi. Hivyo ni vema kutafuta ufumbuzi wewe na mwenzio ima kwa kuuliza waliokuzidi umri, elimu au unaweza kuvuka mipaka ukaenda kumuuliza mpenzi wa zamani wa mwenza wako, usione wivu wala haya. Maana unaweza kugundua hata yeye alimpata baada ya kumkuta akigombana na mtu mwingine aliekua mpenzi wake, labda ndiyo hulka yake.

Mfano: inawezekana siku ya kwanza kuonana nae alikua anagombana na mpezi wake wa zamani, hivyo ili kumtia uchungu na kumdhihirishia kuwa yeye akiona ni wa nini wenzake wanajiuliza watampata lini anaamua kuwa na mahusiano na wewe. Akifanikiwa kumtia uchungu mpenzi wake kwa kuwa nawe fahuwa, lakini akiona kuendelea kuwa nawe hakumshitui kitu bibi au bwana Yule jiandae kuachwa ama kuandamwa na magomvi.

Watafiti wa masuala ya mapenzi duniani wanasema asilimia kubwa ya wanandoa hawana furaha na ndoa zao, wengi wakikumbuka siku waliyokula kiapo cha kuishi kwa raha na shida, hutamani siku zirudi nyuma akatalie palepale kanisani ama msikitini.

Sababu zipo nyingi, wengi huishi katika ndoa kwa kuwa mwenza wake ni chaguo la mama ama jamaa zake. Wengine wanaamua kuendelea kuwa katika ndoa ngumu kwasababu  wameshazaa na watoto  ni wadogo, kuwaacha wachague kati ya baba na mama itakuwa ukiwa mkubwa kwa watoto. Na mengi kadha wa kadha ambayo yanafichwa na viwambaza vya nyumba.

Tunaishi katika dunia ya kila mtu kujiamulia mambo yake, tofauti na zamani baba ndie muamuzi wa masuala ya nyumbani. Hivyo inakuwa ngumu kwa wanandoa kusikizana ama kuwa na nidhamu, kwa maana mafahali wawili hawakai zizi moja.

Tatizo ni nani awe myonge kwa mwenzie, mke anataka kudhihirisha kuwa sauti yake lazima iheshimike, na mume ana yale mazoea aliyorithi kwa mababu zake kuwa mume ndie mwenye sauti ya mwisho. Balaa ndipo linapoanzia hapo; na mbaya zaidi kila mmoja anafanya kazi na kuingiza kipato katika familia hakuna wa kumnyanyasa mwenzie kwa hali yoyote.

Elimu, nyote mmesoma na tena labda chuo kimoja na mkahitimu siku moja maana ndiyo mambo ya sasa hayo. Pesa, nyote mnafanya kazi na mna noti kichele za pesa katika kanzi au wazungu wanaita bank. Umri, mara nyingine mke ndie amekupita, tofauti na zamani mke lazima awe mdogo kwa mume ili apate kumuheshimu.

Hayo yote yanafanya ndoa za sasa kukosa nidhamu na umri huwa mchache kwa magombano ya kila siku. Adabu katika nyumba ikikosekana hata mapenzi hupungua. Hakuna uchawi mzuri katika mapenzi kama kusikilizana, kubali kuwa mjinga ila hakikisha msimamo wako unaeleweka.

Zamani wazee wetu walikua wakigombana na wake zao waliwatuma kijijini wakasalimu wazee,  mantiki yake ilikua ni kumlani shetani. Na mke akisharudi ana hamu na mumewe husahau yote yaliyopita. Ila kwa sasa huwezi kumtuma mke kijijini akakae tu, kwa hali ya maisha ilivyobadilika Watu wanafanya kazi sasa mke na mume, utamtuma kijijini na kazi amuachie nani?

Nilichotaka kueleza hapa ni namna ya wake zetu tunavyoonana nao katika siku za awali za mapenzi yetu, mfano mkeo umeanza kuonana nae katika kilabu cha pombe, ama ulimkuta nusu uchi ndipo ukapenda mwili wake kwanza; hivyo hali itakapobadilika na kurudi kama zamani ulivyomkuta usishangae.

Hivi utajisikiaje unamkanya mkeo asinywe pombe na amrudie Mungu au unamshauri asitiri mwili wake kwa kuvaa hijab au buibui, na anakujibu ‘kwani wewe uliponiona kwa mara ya kwanza nilikua msikitini au ulinikuta na buibui?’ eeeennnhhh!!? Utajisikiaje? 

Tafakari, chukua hatua kijana wa kike na kiume. Usikubali kuvutwa na matamanio ya nafsi yako, bali isikilize sauti ya Mungu anavyoshauri namna ya kumpata mume au mke bora. Naomba kuwasilisha.
 

Thursday, November 25, 2010

karibuni makaadi waugwana kwa idadi.


Na Hafidh Kido

Mwandishi Hafidh Athumani kido, ni mswahili aliezaliwa uswahilini na mwingi wa kufurahia ladha ya lugha adhimu ya kiswahili. Blogu hii ni ya kiswahili na mwandishi hufikiri namna dunia inavyokwenda. 

Kila uchao kuna mambo mapya yanayobangua vichwa vya wanaadamu. Ni fedheha sana kwa muungwana kushindwa kuidhibiti mihemko yake. Jina la ukurasa huu limeitwa 'picha na maneno,' kwa maana lugha zote duniani zinawakilishwa na vitu viwili, picha na maneno.

Mara zote tumekuwa ni watu wa kushindwa na mabadiliko ya kilimwegu. Mambo mengi hutokea kwa lengo la kututahini; lakini ni kweli kuwa tumeamua kuishi maisha ya walioshindwa? Jibu ni hapana, kwa kila mwenye kufikiri.

Najua sijapata wasaa wa kukukaribisha rasmi katika blogu hii yenye kuisadifu dunia na mambo yake, blogu yenye ladha ya Kiswahili kitamu kikwanguacho ndimi zetu laini. Karibu tafadhali ufaidi uhondo huu. 

Andamana nami katika ukurasa huu ili uweze kupata mafafanuzi ya mambo kadha yanayoonekana kutushinda kuyapatia maamuzi, aidha kwa uchache wa elimu ya dunia au uvivu wa kufikiri. Ahsante mswahili mwenzangu. 

Karibu ukaribie, ulo nayo unambie
Hofu tusizikimbie, nyufa tuzizibie
Kaburi tuwachimbie, waoga kina babie
Hekima jengo la busara, tuandamane nayo kwanza

umeshawahi kutamani kurudi nyumbani?










Na Hafidh Kido

Dunia imefanya maonevu makubwa kwa wanadamu kufarakana na jamaa zao, kwasababu ya kuhangaikia maisha mepesi kuishi. Kila mtu ameshughulika na upande wake kiasi hadiriki hata kumtembelea jamaa wa karibu, japo kumjulia hali katika kitanda chake cha ugonjwa.

Namna hii polepole bila kujitambua tunazitenga tamaduni zetu na kukumbatia matamanio ya dunia; tunasahau tulipotoka na kujinasibisha na tulipo sasa, mradi tunapata tonge siku zinasonga. Dhuluma iliyoje kwa nafsi zetu wanaadamu, dharau isiyomithilika kurudi chini ya mchanga mikono mitupu; tazama jamii iliyokukuza imekutenga na Mola mwingi wa usamehevu pia amekukasirikia, kwasababu tu Dunia ilikutia upofu ukakumbatia hadaa zake.

Wengi tupo mbali ya ardhi tulizozikia vitovu vyetu; namaanisha bara, nchi, mikoa na wilaya tulizozawa na mama zetu, badala yake tupo mbali huko tukihangaikia maisha mepesi ama kazi nzuri. Lakini tunasahau kuwa kazi ama mshahara mzuri kwa mwanaadamu ni kutimiza malengo yaliyokufanya uje duniani.

Haina maana kujitesa na kujidhuru mwili kwa kukaa nchi za baridi ama joto kali, ukaacha kwenu kuliko na upepo mwanana na miti mingi itoayo harufu tamu ya utomvu wa matunda machanga ama maua ya kuburudisha mboni za macho na pua;  badala yake kujifutika mahala ambapo kuna msongamano wa magari, watu na majumba yaso mpangilio wa ramani.

Karaha ya moshi wa magari na kelele za viwanda zote hizo huzibua masikio yaliyozoea milio laini ya ndege waimbao kwa sauti za kupokezana. Lakini tunavumilia kukaa mahali pasipokubaliana na afya zetu, kwa maana Mola ni mwingi wa hekima kwa kuwaumba kila watu na hali zao za hewa.
Lakini tunadiriki kukaa sehemu ambazo hazikubaliani na maumbile yetu na wakati huohuo hatufuati kilichotupeleka huko. Tunaanza kusahau nyumbani na tamaduni zetu zilizotulea, tunatumia hovyo tunachokipata bila kukumbuka wazazi na ndugu tuliowaacha nyumbani kwa hadaa tu za kipato. Haipendezi katu.

Kama hiyo haitoshi tunabadili maisha yetu na kujinasibisha na uzungu, uhindi ama uarabu kulingana na bara tulilokuwapo, tamaduni zetu za upole, kusaidiana na kuoneana huruma zinapotea kama theluji katika mahali wazi; inanikera sana.

Haivutii hata kidogo kuona mtanzania anakaa ulaya miongo mitatu, hafikirii hata kurudi nyumbani na kufanya maendeleo. Mbaya zaidi hata watoto atakaowazaa hataki kuwapa majina ya nyumbani, hawazungumzishi lugha ya nyumbani wala hafikirii kuwatembeza mahali alipozaliwa hata siku moja.

Hata  fikira ndogo ya kibinaadamu ambayo haihitaji usomi wa chuo kikuu ni kuwa, tumekimbia maisha mabaya nyumbani na sasa tumeshayapata, je umewahi kufikiria kuisaidia jamii yako nao waondokane na dhiki uliyoikimbia? Ama unataka nao wakimbie kama wewe na jamii yenu ifutike kama zamani.. hapana hilo haliwezekani, ni upuuzi usiomithilika.

Katika historia nchi ya Australia na Marekani kuna watu ambao asili zao ni nchi hizo, lakini leo hii zinakaliwa na wazungu na watu wamesahau kabisa uwepo wa waanzilishi wa nchi hizo. Mfano Aboriginal ni watu weusi na ndiwo wenye nchi ya Australia, ila ukoloni umeshtadi katika nchi hiyo ukatafua uwepo wa watu hao ‘waaboriginal,’  mpaka sasa wamepotea; inaonekana  hawakua na mapenzi kwa nchi yao hata kutominyana kubaki nchini mwao. Tazama leo msomaji unashituka kusikia jina la Aboriginal kama watu wenyeji wa Australia,  wamepotea kabisa na kubaki katika vitabu vya kumbukumbu na majumba ya historia.

Kadhalika nchi ya Marekani wenyewe ni wahindi wekundu, lakini Christopher Columbus, ameigeuza historia ya watu hao na sasa imebaki kwenye vitabu na majumba ya historia tu kuwa wahindi wekundu ndiwo wenye Marekani. Na hii ni sababu ya kukosa uzalendo na asili zetu.  

Mwandishi anajaribu kucheza na maneno ili wanaadamu wajenge utamaduni wa kuthamini tamaduni zao na kukumbuka walipotoka. 

Inasemwa kuwa mtu asie na historia ni mtumwa,  hathaminiki. Leo hii wahindi wekundu wamekimbilia msitu wa Amazon, lakini wazungu wamefanya kila jitihada za kuwatumia kama nembo ya Marekani ila haisaidii kitu;  kwani walishaamua kuitupa nchi yao na kuwaachia wazungu, hivyo itabaki tu katika vitabu vya historia kuwa wahindi wekundu ndiwo wakazi halali wa Marekani lakini kimantiki haipo tena akilini.

Hushangai mji kama Dar es salaam, wenyeji wamekua ni wachaga, wadigo, wahaya na makabila mengine toka bara. Uroho wa fedha na kutothamini nyumbani kumefanya wakaazi halisi wa Dar es salaam kukimbilia mbali au kuhama mji kabisa. Haivutii..

Tazama ugomvi wa Palestina na Israel, waisrael walikuapo katika ardhi ile kwa miaka ya nyuma kabisa ila wakahama. Walikimbilia ulaya kutafuta maisha rahisi.

Nao  baada ya kufurumushwa na Adolf Hitler wa Ujerumani, waliamua kurudu kwao ila hawakua na pa kufikizia, ndipo walipoamua kununua ardhi kutoka kwa waarabu wa palestina.

Kilichotokea ni waarabu nao kufanya kosa lile lile walilofanya waisrael kwa kuthamini fedha kuliko ardhi na utamaduni wao, waliwauzia kwa fujo  bila kujua ardhi husogea upande wa waisrael kama maji yanavyokupwa na kujaa baharini; wamekumbuka shuka kumekucha wanaanza kuwafukuza katika mpaka wa Gaza wakidai wanaingiliwa katika mipaka bila kujua walikua wakiuza miliki yao kwa tamaa ya fedha. Sasa wanajuta. 

Ni vema kuanza kujithamini ukupenda ulipotoka ndipo watu wako wa karibu wataanza kukuthamini na kukuheshimu. kwa  maana heshima ya mtu huanzia kwake.

Anza sasa kutembelea kijiji ulichozaliwa na kama upo nchi za mbali jaribu kuweka katika ratiba zako  uende kwenu ukasalimie, kama umebahatika kupata mke na watoto usione haya kumuonyesha mkeo mahali ulipozaliwa hata kuwe kubaya namna gani.

Hivi huoni ngowa kupata kumbukumbu ya harufu ya maembe mabichi ulizokua ukipopoa na wenzio wakati mkirejea toka shule? Huoni ni fahari kumuonyesha mkeo, mumeo ama watoto wako kuwa mto huu ndiwo nilikua nikivuka kuenda na kurudi shule, ama katika nyumba hii inayotaka kuanguka ndipo nilipozaliwa na kukua mpaka hivi nimekuoa ama nimeolewa na wewe tukazaa watoto hawa… hutamani?

Hebu jaribu kuliweka hilo akilini, nina hakika litakusaidia katika kulinda na kuheshimu utamaduni uliokukolea, kadhalika itakusaidia kujivua na utumwa ulionao. Najua kuna fundo limekukaa kwa muda mrefu namna utakavyorudi ulipozaliwa ila unazuiwa na maisha ya kigeni yanayokufanya uone haya kuujulisha umma kuwa hivi nilivyo chimbuko langu ni hapa. Jaribu kufuta mawazo hayo na uanze upya.  Ishi wewe na si watakavyo wao.

dhana haifai katika maisha


Tuache kuishi katika dunia ya dhana.


Na Hafidh Kido
Dhana ni kitu kibaya kabisa kwa dunia ya sasa iliyojaa kila namna ya taaluma na utitiri wa wataalamu wa fani mbalimbali. Huonekana ni jambo lililozoeleka kwa wanaadamu kudhania mambo tu na kukubali kupelekwa kibubusa; tunaridhika haraka kwa uchovu wa kufikiri.
Tumekuwa wavivu wa kuamua, hakika hainiridhishi hata kidogo. Jambo dogo linapodharauliwa linaweza kugeuka gharika ya matukio mabaya usiyoweza kutarajiwa katika maisha. Si vema kudharau kitu pale unapoona kitakuja kukudhuru.
Husemwa tone hujaza kiganja na kufanya bwawa la maji, na chembe ya mchanga hufanya tofali pakatokea nyumba; ndivyo hivyo hivyo ujinga mmoja huzaa matatizo katika jamii pakatokea mabahauu.
Tukirudi katika mada yetu, dhana imefanywa kitabu cha kukaririwa na kila mja mvivu. Si ajabu kumkuta kijana wako hakwenda shule, unapomuuliza anakujibu ‘nadhani leo shule hakuna kitu cha maana, hivyo nimeamua kubaki nyumbani na nitakweda kesho Mungu akipenda.’ Ni jibu la kipuuzi kabisa.
Kwanini udhani, kwanini huna majibu ya moja kwa moja yasiyoambatana na dhana? Ni hatari sana kauli ya kudhani ikachukuliwa kama dharura ama sababu ya kukimbia ukweli, bali bila kujua tunageuka mbuni kwa kuficha vichwa vyetu mchangani ili tusimuone adui au hatari ituepuke. Tunajidanganya.
Dhana, neno hili linaweza kutumika katika mwanzo wa sentesi yenye shaka, sentesi ya mtu anaeuliza ama kuhitaji ufafanuzi wa jambo kadha, hiyo imewafikiwa na watu wa lugha. Lakini dhana inapotumika katika sentensi sahihi na yenye kuonyesha ushupavu wa muongeaji, hapo ndipo mashaka yanapoanzia.
Mfano: mtu anaweza kusema ‘nadhani tunahitaji mwalimu wa kutuelekeza somo hili.’ Hiyo imekaa vizuri, neno dhana hapo limetumika kama kiulizo. Lakini mtu anaposema ‘nadhani mvua itanyesha, hivyo leo sitokwenda shambani kulima.’ Hiyo ni dhana ya kipuuzi kabisa na yenye kurudisha nyuma maendeleo. 
Kwanini udhani kitu ambacho huna uhakika nacho? Na nimegundua mara nyingi wavivu ndiwo wepesi sana wa kudhani vitu vya ajabu ajabu kama ajali, mvua na mambo ya kumzuia au kumkatisha tamaa mtu kufanya jambo la maendeleo.
‘Nadhani kesho sitokuja, hivyo kazi yetu itaendelea keshokutwa,’ tazama wavivu wanavyojua kukwepa kazi. Kwanini hutoi sababu kamili ya kutokuja kwako na badala yake utumbukize neno ‘nadhani’ kama sababu ya msingi?
Tukumbuke tunaishi katika dunia ya kiminyano cha maisha, si vema kuchelewesha kazi kwa uvivu tu, punguza kudhani bali fanya utafiti upate sababu njema ya kutokamilisha jambo.
Mtu anaweza kuwa hana ufahamu na jambo kadha, badala ya kuuliza wanaojua ama kufaya matafiti juu ya suala hilo, matokeo yake hukwambia anadhani jambo hilo hufanyika kadha au halipo kwa maana halijui. ‘Nadhani hili haliwezekani, kwa maana hiki kimekaa hivi na hakipaswi kuwa hivi.’ Epuka sana kauli hizo za dhana.
Mitandao ya intaneti, magazeti, vitabu na kila namna ya taaluma katika redio na luninga; bado tu tunaamua kuishi katika dhana? Tubadilike japo kidogo, tujitahidi kubadili matamshi yetu na kuipa dhana muda mdogo wa matumizi katika matamshi ya siku nzima.
Unaonaje kuzungumza na wanafunzi au wafanyakazi wenzio huku ukitumia kauli za kujiamini, kutoa maelekezo na ufafanuzi kwa kila jambo linaloonekana kikwazo katika masomo au kazi? Hakika ni jambo la kuvutia sana kujiamini.
Umalizapo kusoma makala haya nataka ule yamini ya kutotumia neno ‘nadhani’ kwa siku nzima tangu kusoma makala haya. Baada ya hapo tazama nafsi yako ina furaha ama kuna majuto kwa kukosa kulitumia tamko hilo dhalili.