Saturday, November 20, 2010
Sunday, November 7, 2010
ujana tuutumie vizuri
Na Hafidh Kido
Ujana ni kitu azizi sana, walipata kusema washairi wa zamani. Unaonaje mwanaadamu aliejawa siha, sura jamali na kiwiliwili kilichoshikamana kwa afya na furaha ya uzima; maradhi huwa ni kitu kigeni katika jumba la mwili wa kijana huyo. Ajabu akidi.
Lakini ujana hulemaza akili mwanadamu akasahau lengo la kuumbwa, ile furaha ya kuchekewa na kupendwa kila apitapo humpumbaza kijana akadhani dunia ni yeye na hakuna mwengine; makosa makubwa ajabu.
Tazama mzee aliepinda mgongo kwa kula chumvi nyingi namna anavyotamani kurudisha siku nyuma na kutenda matendo mema ili uzee wake upungue mashaka. Hudhani hata yeye alikua kijana kama wewe na sasa mate yamekuwa machungu na macho kufanya kiwi hajui tofauti ya mchana na usiku. Kama ni mwanamke zile nywele alizokuwa akizitunza kwa gharama kuu sasa ni kama mkonge uliokosa rutuba katika konde dhaifu la kichwa cha kizee huyu..
Mtu aliekuwa akiitwa na vijana wenye uchu na ubazazi kutokana na uzuri wake lakini leo hii hata kutazamwa hatamaniki; hudhani ni huzuni ya nafsi yako kuwa katika hali hii ikiwa sababu ni kuutumia vibaya ujana wako?
Jiulize ni mara ngapi umepata kukutana na mtu wa makamo mwenye umri mkubwa tofauti na muonekano wake. Jibu unalopata ni kuwa alijitunza vema alipokuwa kijana, fahari iliyoje hii. Huoni haya kujidhuru mwili kwa furaha ya muda mfupi hali utakuja kutaabika kwa muda mrefu pindi upindukapo miaka hamsini tena bila ya msaada wa ndugu wala watoto uliowazaa mwenyewe na kuwalea kwa taabu kuu.
Mawe!! Hakuna jibu muafaka la maswali yote hayo bali kuwa makini kwa kila nukta ya tamko litokalo kinywani mwako, kuzingatia kila angalio la ubaya ama uzuri kwa jirani au mtu baki, kuwa mbali na chuki na kila dhiki uzibebeshazo moyo mteke wa kiumbe cha Mungu. Hakuna tahadhari njema kama kuulinda moyo wako na mabalaa ya dunia; macho hutazama, ulimi hutamka na miguu ikafuata, ila balaa lolote litakalosababishwa na viungo vyote hivyo mbebaji ni moyo.
Chunguza kisigino kinapopata ajali ya kudungwa na nyigu au msumari, lakini maumivu hupenya mpaka kwenye moyo pakatokea mpasuko wa uchungu kama radi isiyoambatana na mvua. Moyo huzeeka haraka na ukajiinamia kutokana na rabsha za dunia wewe mmiliki uutwishwazo, ni adhabu ya kijinga uupao moyo kwa tamaa za muda mfupi na upungufu wa tahadhari.
Husemwa kwa mwerevu huenda kilio, lakini kinyume chake ni kicheko, hudhani kilio hudumu muda mwingi kuliko kicheko? Kwanini usichague kicheko ili uache kuwa na huzuni kwa muda mwingi? Maana huzuni hutafuna mwili mithili ya panzi atafunavyo jani la mbono.
Najaribu kuwavuta vijana ili wawe pamoja nami katika makala haya kwa lengo la kuondoa chuki na hashuo la kukurupuka kulaumu pasi na kuelewa mada na mwandishi kalenga nini katika maandiko yake.
Wamasai husema ‘ukiona simba kazeeka ujue amekwepa mishale mingi’ na ndivyo ilivyo kwa mwanadamu, ukiona kijana amezeeka vizuri ujue alijilinda na kukwepa majaribu mengi katika ujana wake. Huamki tu kutoka usingizini na ukajikuta u mzee wa siha na furaha nyingi, mara nyingi wazee hutuhumiwa uendawazimu na matusi kila namna kwa kuwa tu hawapendezi tena katika jamii.
Utajisikiaje leo nawe unakuwa kama Yule kizee anaepita mitaani na kopo akiomba senti ya kula huku ngozi yake imesinyaa kama dagaa la ziwani, nguo zake zimefubaa kwa kukosa maji muda mrefu huku amepinda mgogo kwa machovu. Hutumia saa nzima kukatiza uwanja wa mpira kwa namna anavyopiga hatua fupi za machozu ya mzigo wa uzee, unadhani hana ndugu?
Nani amekwambia uzee ni adhabu; hatuzeeki ili tudharaulike katika jamii wala kupoteza mazuri yote tuliyoyafanya wakati wa ujana. Bali ni sisi wenyewe ndiwo tuandaao uzee wa mashaka kwa kutojali kesho yetu. Tuache kuishi leo, tukumbuke kuwa kuna kesho na keshokutwa.
Uraibu tuutumiao sasa ni sumu ijirundikayo mwilini na huchamka pindi tuzeekapo. Ugoro, mirungi, pombe na zinaa ni sumu kali sana kwa afya za wanaadamu. Hasa vijana.
Tupunguze kulala sana kwani mwili uliozoea kukaa kaa huchoka haraka. Tuzidishe kufanya kazi ili tuwe na akiba itakayotufaa uzeeni, ndugu watuchukiao pindi tunapozeeka hali tu maskini ndiwo haohao wanaotutumia kwa ushauri na kutusikiliza kila tusemacho pindi tuzeekapo hali tuna kipato.
Hujapata kusikia watu huwaita wazee dawa? Lakini mara hiyohiyo jamii huwatusi wazee kwa kuwaambia wanazeeka vibaya na hawahitaji ushauri wao. Lakini inaaminika wazi kuwa ukiutumia vibaya ujana wako kwa matumizi yasiyo na nidhamu hakika utazeeka masikini na jamii itakosa kukuheshimu.
Kitu kingine cha kuzingatia ni aina ya vyakula tunavyokula, ni hatari sana kula sukari kwa wingi, mafuta na nyama kwa wingi huharibu siha. Kwa sasa utaona ni tamu na huleta hadhi, ila kwa baadae bohari ya maradhi utakayokutana nayo hakuna wa kumlaumu ila ni nafsi yako.
Mazoezi ni kitu muhimu sana kwa mwili wa kijana, kujibweteka tu ni mbaya sana; Misuli na moyo vinahitaji kushughulishwa ili vipate kufanya kazi kwa bidii na kuacha kufubaa.
Ushauri wa bure kwa vijana wenzangu ni kuzingatia kuwa uzee ni aibu pindi ukikujia wakati uliutumia vibaya ujana wako ima kwa kutojiandaa kifedha, kiafya na kielimu. Maana ni vema kuwa na elimu ili vijana wa baadae wapate msaada mkubwa toka kwako.
Tazama mzee alielala kitandani hana afya wala fedha, lakini ni aalimu mkubwa katika masuala ya utabibu, historia ama sanaa. Watu hupanga misururu ya mstari ili kumuona na kuvuna chochote toka kwake. Furaha iliyoje hii kuthaminika hata katika kitanda chako cha uzee unasubiri kifo.
Mfano mzuri ni hayati Mwalimu Nyerere, hakuwa na fedha wala afya katika kitanda chake cha kifo, lakini angalia msururu wa wasomi na watu wakubwa duniani namna walivyomuandama ili kupata chochote katika taaluma ya uongozi ili nao wanufaike kwacho.
Tujue ujana ni dhamana itaondoka baada ya miongo michache ya kujifaragua na majigambo. Na tutaishi katika dhiki na kukimbiwa hata na damu zetu tulizozizaa na kuzihangaikia kwa taabu nyingi. Hujasikia mtu anasuswa na watoto wake mwenyewe? Tena kwa kuitwa mzee wa nongwa……
Wednesday, November 3, 2010
fahari ya jioni inapoingia.
Na Hafidh Kido
Adhuhuri huchechemeza duara la jua na kuikaribisha alasiri yenye miali hafifu ya jua na burudiko la mchanganyiko wa joto na upepo mwanana kulingana na hali ya hewa siku hiyo.
Jioni huingia baada ya mchekecho na mabishano mafupi baina ya jua na mbingu kuwa nani atawale wakati. Na ndiyo maana jioni inapoingia mawingu hutoa kilio na kuacha uwekundu uliosababishwa na athari ya kilizi cha jua kushindwa pale linapoamua kuondoka katika upande mmoja wa dunia.
Hali hiyo ya mabishano hutoa faraja kubwa kwa mwanadamu anaefuatilia kwa makini kitali hicho; hakika ni burudani isiyo kifani kushuhudia kuzama kwa jua. Macho hufanya nuru inayoakisiwa kutoka katika mbingu; rangi ya samawati iliyochanganyika na zari ipendezayo angani humaanisha kuisha kwa siku.
Waumini wa dini ya kiislamu wakati huo hushughulika kushika udhu ili kuingia katika sala ya magharibi kwa kumtukuza Muumba wa maajabu yote hayo. Shukurani nyingi humuendea muandisi wa ajabu hiyo ya kupendeza.
Mara nyingine watu hutoa viti vya uvivu nje wakiwa na vikombe vya kahawa wakishuhudia mandhari hayo mazuri ya kupendeza macho na kupumbaza akili, baada ya hangaiko la siku nzima katika jua kali la kutesa ngozi. Huwa ni kama sherehe ya kuliaga jua ili kuukaribisha mwezi na nyota zake wakia pulizo la upepo likizidisha raha hiyo ya magharibi.
Magharibi ni wakati muafaka kwa wapendanao kuandaa mandari yao au kwa wanagenzi wa mambo ya mahaba kuomba kutoka kwa kinywaji au mlo wa pamoja na wawapendao. Nyakati hizi huwa kama uchawi namna zinavyopumbaza akili za watu. Maajabu mengi hutendeka.
Magharibi huvuta watu katika migahawa na masikani zenye mwanga hafifu mfano wa sumaku ivutavyo uchafu wa chuma na vitu namna hiyo. Utaona watu wamesimama wawiliwawili katika vipembe vya mitaa na viguzo vya umeme au visiki vya miti; hilo hudhihirisha ni namna gani wanadamu hunufaika na kiza. Maana mengi yashindikanayo kufanyika mchana huvugumizwa katika nyakati hizi.
Fahari ya magharibu hudhihirika pale mwanadamu anapozigugumia pesa zake alizozivuna kwa siku nzima. Wengine hunena ‘ponda mali kufa kwaja,’ lakini itaonekana ni msemo wa kipumbavu kabisa ikiwa unatumia usichoweza kukiingiza; ama unatumia nusu na robo ya ulichokichuma hali saa chache kutakucha na misukosuko ya kilimwengu itaanza upya usahau kama kulikuwa na magharibi usiku wa jana.
Ni jambo la kuchunga sana namna tuitazamavyo magharibi, maana ni wakati wenye ghiliba nyingi na vishawishi vya ajabu sana. Mara zote huwafanya watu wajute saa chache baada ya kuitumia vibaya magharibi yao; ujukuu wa majuto hudhihirika pale tu uamkapo kitandani huna senti hata moja hali mchana wa jana ulihangaika chini ya jua ukiitafuta hiyo shilingi kwa matusi, kedi na kila namna ya dharau za waajiri wabaya.
Chumo bora hupaswa kutumika vema na kwa uangalifu mzuri sana, ni faraja na fahari iliyoje kuweka akiba yako kwa manufaa ya baadae. Ni ushujaa mkuu kuipitisha magharibi kwa kinywaji kidogo ima ukiwa na familia au wenza wema watakaokushauri kurudi nyumbani kupumzika baada ya kukuona umeanza kupoteza utimamu katika maamuzi. Ama ni vema kuipitisha magharibi ukiwa nyumbani huku umeshikilia kikombe cha chai ukizungumza na mtoto wako mkiulizana habari za masomo na kumsaidia kazi za shule.
Ni ushujaa ulioje kuipitisha magharibi yako ukiwa jikoni na mumeo ama mkeo huku mkisaidiana kuandaa chajio kwa furaha na vicheko mkitaniana. Huoni ni jambo jema kuonekana na watoto wenu mkiwa pamoja mkifurahi, maana hata wao hufarijika kuwaona wazazi wao katika hali hiyo.
Akili ya kawaida tu inatosha kufahamu kuwa mchana ulipita nyumba ikiwa tupu na kimya kama ganjo wakati wewe ukiwa kazini na watoto wakiwa shuleni; magharibi ama jioni imefanya tas-hila na msaada mkubwa kuweza kuwaweka pamoja watoto na wazazi, hivyo si busara baba kuiacha familia yako ikiwa pweke nawe ukatokomea kusikojulikana halafu baada ya saa nyingi unarejea nyumbai ukiwa umelewa, watoto wameshalala, mama amechoka kwa kukusubiri, chakula kimepoa na nyumba imepoteza nuru ya mkusanyiko wa familia. Si hali nzuri, hakika husikitisha.
Muumba ardhi na mbingu amezigawa nyakati na matukio ili iwe rahisi kwa wanaadamu kufanya mambo yao kwa ufanisi na utaratibu mkuu.
Asubuhi ni ya kujiandaa kulijenga taifa na watoto huenda shule ili kujizoeza kutenda matendo bora ya baadae na kujua mambo mapya ambayo ima walikuwa wakiyasikia lakini hawana uhakika nayo au ni mapya kwa maana ya upya, huyajua kwa mara ya kwanza ili yaje kuwasaidia katika umri uliobakia.
Mchana huwa ni wa kupumzisha akili baada ya kuisumbua kuanzia asubuhi ima kwa kazi ngumu au masomo yanayohitaji akili imara. Na ifikapo alasiri huwa ni wakati wa kurudi nyumbani na kuandaa ya magharibi.
Wengi huitumia alasiri kwa kusoma majarida, vitabu, kutembelea wagonjwa, ndugu au jamaa waliopotelewa na mtu kwa kuifariki dunia. Vijana wengi huenda pwani ya mito au bahari ili kuikabili kurasa nyeupe ya maji yaliyotuama. Ama hutembelea mabustani ya maua yenye harufu nzuri na laini kwa nyoyo zilizokufa; Kufanya hivyo huwaburudisha nafsi na kupata akili mpya.
Magharibi huwa ni wakati wa kurudi yumbani na kukaa na familia, kula au kunywa pamoja huku mkitazama luninga. Wengine ambao hawana familia huitumia magharibi kwa kutembelea sehemu za burudani ama hukaa tu na marafiki wakipiga soga.
Usiku unapoifunika dunia ni wakati wa kulala na kupata nguvu mpya ya kuikabili asubuhi yenye mikiki na vishindo vingi vya walimwengu.
Ni busara sana kulala mapema na kuamka mapema, na ni ukatili wa afya yako kuchelewa kulala na kuchelewa kuamka ama kuchelewa kulala na kuwahi kuamka. Kwa maana mwanaadamu amepangiwa saa za kila shughuli anayoifanya katika siku yake. Na kulala kumetengewa saa kumi katika saa ishirini na nne za siku nzima.
Maana ikiwa tunashauriwa kulala mchana kwa saa mbili, na usiku kuanzia saa nne tuwe tumeshalala na asubihi ikifika saa kumi na mbili tuwe tumeshaamka. Sasa ukichanganya utagundua katika saa 24 tunapaswa kulala saa kumi. Na hizo saa kumi na nne zilizobaki tunatakiwa kuzitumia kwa ibada, kazi na kukutana na jamaa ima kwa kutembelea wagonjwa au kusaidia wahitajio msaada au kufunza na kujifunza vitu vipya katika dunia.
hasira na hasara zake.
Na Hafidh Kido
Unapotaja neno hasira kitu kinachokuja kwanza katika fikira ni maudhi na ukakasi wa hali awayo mtu anapokarahishwa na tukio, neno au hali fulani katika maisha tuishiyo ya karaha taabu na raha kidogo.
Hufurahisha kuona mtu anaweza kuhimili hasira zake, lakini pia simlaumu mtu anaeshindwa kuzuia hasira zake bali humuhurumia mtu namna hiyo. Kwa maana mpaka mja huamsha hisia zake za hasira inaonyesha ni namna gani ameshindwa kuvumilia kwa alilolishuhudia ama kulisikia dhidi yake.
Lakini husemwa jemedari ni Yule awezae kushinda kitali cha kupigana na moyo wake dhidi ya maudhi ya wanaadamu. Ikumbukwe kuwa tunaishi katika dunia ya mchanganyiko wa tabia na historia tofauti za maisha; hivyo kuudhiwa ama kutoelewana katika dunia ni kitu cha kawaida sana haifai kubeba kila uonacho na kukihifadhi moyoni kwa chuki na maudhiko.
Mara nyingine watu huona raha tu kukujaribu na kuona ni namna gani unaweza kughilibika na nafsi yako dhidi ya utani mdogo tu unaokera moyo; ni kawaida ya wanaadamu kufurahishwa na sura ya kutisha ya mtu alieudhika.
Ni busara kuhimili hasira zako ili watu wasione udhaifu ulionao pindi uudhikapo, nasema hivi kwa maana hasira humfanya mtu mwenye hadhi kuongea maneno mabaya yaliyo nje ya maadili mema katika jamii na kuiharibu heshima aliyoihangaikia kwa miaka mingi; pengine nusu ya maisha yake.
Marehemu Shaaban Bin Robert, alipata kusema kuwa ‘mtu anapoudhiwa ni vema ahesabu moja mpaka kumi,’ maana ya usemi huu ni kuwa unapoudhiwa usifanye papara ya kuwajibu wabaya wako au kutaka kuwaonyesha kuwa wewe ni nani kwao. Bali vuta subira. Na mara nyingi hasira ina tabia ya kupungua ipitapo kipindi fulani bila ya kutamka ama kutenda kitu.
Mambo mengi huharibika kwa kutendwa huku mtendaji akiongozwa na hasira ama chuki dhini ya nafsi yake. Ndiyo! mtu mwenye chuki hachukii ila huichukia nafsi yake.
Wanaadamu tumejiaminisha kuwa tunawachukia waliotutedea kinyume na tupendavyo, lakini bila kufahamu tunaudhika kiasi tunajidhuru wenyewe kwa kupata maradhi ya moyo; je huoni kuwa unaemchukia unazidi kumpa ushindi badala ya kumfanya ajutie alichotenda dhidi yako?
Angalia dereva alieudhiwa na mke wake nyumbani, huamua kuendesha kwa fujo akidhani anamkomoa aliemuudhi; matokeo yake huishia kuangusha gari ama kumpiga dafrau mpita njia na kupata hasara ya kumlipa mpita njia huyo. Badala ya kutatua tatizo moja bila ya kufahamu anaongeza matatizi juu ya tatizo moja ambalo lingemalizwa kwa kukaa chini na mkewe kumweleza namna alivyomkosea na kumtaka asirudie makosa hayo kwa maana hapendezewi nayo.
Naona unajiuliza ni namna gani utaweza kukaa mbali na hasira; ni rahisi.
Baada ya kuudhiwa na mtu awaye yeyote mdogo, mkubwa, rafiki au mtu baki, kitu cha kwanza kufanya ni kujiuliza kwa kuudhiwa huko maisha yako yatabadilika namna gani? Kitu gani kitapungua katika kipato, heshima au ukaribu na mtu aliekuudhi. Ukiona kipo kitakachopungua hakuna haja ya kumghadhibikia mja huyo bali ni busara kumuuliza ni kwanini ameamua kukufanyia hivyo hali anajua si jambo jema kwenu nyote.
Akikosa jibu muafaka la kukupa na bado akisisitiza kuwa alichotenda ni sahihi, basi kitu chema kufanya ni kutafuta watu ambao muovu huyo anawaheshimu ima kwa kuwa ni wakubwa wake kiumri au kicheo. Kwa kufanya hivyo utamsaidia yeye kujirekebisha ikiwa ni muungwana.
Lakini ukiona maudhi utakayopata hayatokuwa na madhara yoyote kwako ni vema kumuepuka muovu huyo kwa maana hakuna badiliko lolote litakalokupata kwa kumuepuka mtu huyo aso maana.
Waungwana husema ukimya ni silaha ishindayo mara zote. Hivyo inashauriwa kuitumia silaha hiyo mara nyingi iwezekanavyo.
Hivyo ni vema kujiweka mbali na hasira, kwa maana hakuna tunachonufaika kutokana nazo zaidi ya hasara ya kuharibu mahusiano na kazi zetu ama kudharaulika katika jamii.
Subscribe to:
Posts (Atom)