Wednesday, October 20, 2010

woga ndicho kisababishi cha kuonewa katika jamii


Tujijue tuna michango gani ktk jamii tusiishi tu


Na Hafidh Kido

Katika maisha ni jambo jema sana kujijua unasimamia nini, ni ubaghili wa urithi kwa kizazi kijacho kusema mimi siamini kitu na wala sina upande wowote ninaosimamia. Ni vema kueleza msimamo wako kwa njia moja ya nyingi zilizotumiwa na wapigania haki.
Rais wa kwanza wa India Mahatma Gandhi, ni mmoja ya viongozi wanoheshimika sana duniani, alianzisha utaratibu wa kudai haki bila vurugu. Kwa kikoloni iliitwa ‘non violence agitation’ au mwenyewe kwa kihindi aliita {ganda satraha}, utaona ni namna Fulani hivi ya kiyonge ya kudai haki lakini imeleta mvuto na mwamko mkubwa katika dunia mpaka mpigania haki za weusi nchini Marekani Martin Luther King Jr nae aliiga mfumo huo wa kudai haki pasi na vurugu.
Lengo la kusema haya ni kutaka kuieleza dunia kuwa kudai haki ni haki ya kila mwanaadamu anaechukizwa na mfumo Fulani wa kiutawala au namna yoyote ya maisha isiyompendezea.
Lakini cha ajabu wapo watu ambao hubaki mfu huku wakiugulia moyoni, wato namna hiyo hata Mungu huwadharau. Ndiyo! hata Mungu huchukizwa na mtu anaedhulumiwa na asipaze sauti kudai haki yake. Ni ujinga ulioje kunyamazia upuuzi wa mtu mmoja aikoseaje jamii ya watu wapatao maelfu mengi, ni udhalili ulioje kujikunyata kwa hofu kwa kitu kikuyimacho uhuru wa kuabudu, kuamini au kuishi kwa amani kwa maisha uyalipiayo gharama kubwa. Hilo halivumiliki.
Jamii za kiafrika ziliishi katika unyonge kwa karne nyingi zilizokuwa chini ya ukoloni. Walitumishwa na kufanyishwa kazi ngumu ambazo hata hao waliowatumisha wasingeweza kufanya hata robo yake. Mababu zetu walijenga reli kwa kubeba vyuma vya reli katika migongo yao; jaribu leo hii kuyanyua chuma kimoja cha reli na ukibebe japo mita mia moja tu. Lakini chuma hicho hicho kilibebwa na mababu zetu kwa maili elfu bila ya kuchoka huku wakichapwa bakora. Na kila alieonyesha udhaifu aliuwawa kikatili. Udhalili ulioje huu.
Kina Mkwawa wa Uhehe walipojitokeza kudai haki za waafrika wenzao walitokea waafrika wasio na fikra na kuiba siri za viongozi wa kiafrika na kuzipeleka kwa wakoloni ili wapate ngawira kidogo ambazo hazikuwafaa chochote. Haiingii akilini kamwe.
Hata wakati wa kudai uhuru kina Kwame Nkurumah. Nyerere, Kenyata na wengi wengineo kama Robert Mugabe na Nelson Mandela walipata upinzani mkali kutoka kwa waafrika wenzao ambao walikuwa na nyoyo za woga. Ni dhuluma ya nafsi yako kuogopa kuomba haki.
Munaweza kupanga kugomea kuingia darasani ili chuo, shule au taasisi yoyote ipewa haki, lakini unakuta wapo wenzenu ambao wataendele kuingia darasani au kuenda kazini kama kawaida mradi tu wanaogopa kudai haki zao. Hakika inaudhi.
Mara nyingi watu namna hiyo husimamia ukweli kuwa hawataki fujo, lakini kidhati unapopingana na wenzako inaonyesha ni kiasi gani hujui kusimamia unachoamini. Unadhani kizazi kijacho kitanufaika vipi ikiwa wewe uliishi katika unyonge? Unadhani mwanao atanufaika vipi na utu bora ikiwa wewe uliishi katika kupinga mabadiliko? Unadhani mjukuu wako atajinasibisha vipi na wewe ikiwa muda wako wote wa maisha uliutumia katika hofu na kujificha? Unadhani baada ya miaka mia moja utaendelea kutajika ikiwa tu katika uhai wako hukuacha chachu yoyote au alama yoyote ya mabadiliko kwa hiyo miaka mia moja ijayo? Sidhani mtu muoga anayo majibu muafaka kwa maswali hayo. Hakuna  halitokuwapo.
Tunaishi katika dunia ya mashindano, kila mmoja anataka kuvutia upande wake kama muwamba ngoma. Lakini kikubwa ni kujitambua upo kundi gani ili uepukane na matatizo. Maana hatua ya kwanza ya kuepuka tabu ni kukubaliana na hali halisi.
Dunia ina watu wenye kujua mambo lakini wenyewe hawajui, hujiona ni watu wa kawaida sana lakini kauli zao hufuatwa na wanajamii kama nyuki afuatavyo maua.
Cha kushangaza watu namna hiyo hutumia vipawa vyao kuwaogofya watu na kuwakatisha tamaa. La busara ni kuwaamsha watu hao ili wafanye kitu wakijuacho kwa manufaa ya wengi.
Lakini kuna watu ambao hawajui na hawajui kuwa hawajui, ila tatizo lake ni kuwa wabishi wa kuonyeshwa njia. Huamini kila wakisikiacho na ni wakaidi wa kufuata waambiwacho. Mmmhhhh…. Watu namna hiyo ni bomu linalosubiri kulipuka, hutumia nusu ya maisha yao kuamini kisicho kweli. Ni vema kuwaepuka watu namna hiyo ili kusaidia wenye haja. Wadigo wana methali yao isemayo ‘mwana hukanywa akiuya’ maana yake mtoto mkaidi huambiwa ajirekebishe pale anapokubali kuwa alichofanya si sahihi na limeshampata la kumpata.
Kadhalika jamii imejaa watu wasiojua chochote katika maisha, lakini ni wepesi kuuliza kila wanaposhindwa kuelewa. Hao ni waja wema ambao wamesifiwa mpaka na Muumba mbingu na ardhi. Ni vema kuwaonyesha njia na kuwaelimisha, watu hao huwa waongofu kila waonapo ukweli na ni wepesi kuelimisha wenzao kila inapohitajika.
Jamii vilevile imezungukwa na watu wajuvi na wanajua kuwa wao ni wajuvi wa mambo kadha yasumbuayo watu katika jamii wanazoishi. Ni vema kuwa wafuasi wa watu namna hiyo. Wana mambo mengi ya kuturithisha kwa faida ya kizazi kijacho. Kuwaepuka ni sawa na kujaribu kuziba jua kwa kutumia sepetu, bila kudhani kuwa miale ya jua hupenya kila penye nukta ya upenyo.
Kifupi nilichotaka kuieleza jamii ni kusimamia haki zetu, tusiwe waoga kwa kusimamia ukweli. Kuwa msaliti wa nafsi yako ni kosa kubwa sana litakaloisababishia dunia kuangamia. Watu waoga ndiwo wasababishao mambo kuenda mrama, vita, taabu na maonevu huletwa kwa kuwa dunia inashikiliwa na watu waoga.
Acha uoga simamia haki yako, kuna manufaa makubwa kwa kizazi kijacho.

No comments:

Post a Comment