Wednesday, October 20, 2010

unaupingaje ufisadi kuanzia ngazi ya familia?


 JE? UFISADI NI IMANI KAMA ULIVYO UJAMAA

Na Hafidh Kido

Hayati mwalimu Nyerere katika maandiko yake yahusuyo ujamaa alipata kusema kuwa “ujamaa wa kweli ni mawazo ya mtu.” Akimaanisha kuwa ujamaa si kufuata sera yake au kumuonyesha mtu kuwa mimi ni mjamaa kamili, bali ni namna mtu anavyoamini na kuishi kijamaa.

Mwalimu alifafanua kuwa, “Ujamaa, kama demokrasia, ni moyoni. Katika nchi ya ujamaa kama unataka kuhakikisha kwamba watu wanajali shida za watu wengine, linalotakiwa ni mawazo ya kijamaa, wala siyo kufuatisha tu utaratibu maalum wa siasa.”

Na tunafahamu kuwa Mwalimu aliupiga vita ubepari ikiwemo rushwa kwa maisha yake yote, tangu akiwa shule, wakati wa mapambano ya kuleta uhuru, kipindi chake cha uongozi kama rais wa nchi na mwenyekiti wa chama tawala na hata alipostaafu.

 Machi 13, 1995, Mwalimu alipokuwa anazungumza na klabu ya waandishi wa habari wa Tanzania, katika hoteli ya Kilimanjaro, alipata kusema haya,“usije ukadhani kwamba wakati wa awamu ya kwanza palikuwa hapana rushwa; ilikuwapo, lakini tulikuwa wakali sana….. tulitaka watu wajue hivyo. Tulitaka watu wajue kwamba tutakuwa wakali sana na wala rushwa ndani ya serikali na wale wanaotoa rushwa.” Na hakika Mwalimu hakutania wala hakumuonea mtu haya. Aliwadhibiti wala rushwa kwa uwezo wake wote.

Yanayotokea sasa yanaweza kuzuilika ikiwa tu watanzania watamuenzi baba wa Taifa kwa vitendo, tofauti na kumuenzi kwa kunywa na kula siku ya kumbukumbu ya kifo chake. Wakati wa Mwalimu ufisadi uliweza kuzuilika kwa namna mbili.

Moja ni kwa kumdhibiti mtu anaetaka kuwa kiongozi, kwa maana aliwaandaa viongozi kuwa watumishi bora kwa wananchi. “Zamani, katika CCM na katika TANU, tunapochagua mgombea wetu, kama ana mali, tunamwambia ‘hii mali umeipata wapi?’ mali kilikuwa kigezo cha kukupotezea sifa ya kuwa mgombea.”

Jambo la pili Mwalimu alilolitumia kupiga vita rushwa kwa viongozi ni kutowaonea haya viongozi wa ngazi yoyote. Utaona kwamba mara tu baada ya kupata uhuru, waziri wa sheria wa Tanganyika alibainika kupokea rushwa, lakini Mwalimu aliacha sheria ichukue mkondo wake, hakutaka kufunikafunika wala kumung’unya maneno; alimuadhibu kama sheria ilivyotaka. Kwa kiasi utaona viongozi wote waliokuwa kipindi cha Mwalimu, kama bado wapo hai basi hawana mali nyingi kupita kiasi. Maana yake hawakula rushwa wala kujilimbikizia mali kama ilivyo sasa. 

Tunafahamu kuwa ufisadi ni ubepari uliokomaa, tena zaidi ya ubeberu. Lazima tujiulize kwa umakini kuwa huu ufisadi nao ni imani kama ulivyo ujamaa?

Sababu za msingi za kuuliza swali hili ni kutokana na kujirudiarudia kwa matukio ya kifisadi mbali ya viongozi wa dini, vyama vya siasa na vyombo vya habari kupiga kelele kila siku juu ya kukithiri kwa vitendo vya kifisadi. Lakini badala yake ndiyo vinaongezeka maradufu.

Msomi maarufu nchini na Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo kikuu cha Dar es salaam, Profesa issa Shivji, alipokuwa akiwasilisha mada inayohusu mtazamo wa Mwalimu Nyerere juu ya ujamaa, ubepari na ufisadi; katika kongamano la kumbukumbu ya miaka kumi tangu kufariki Baba wa Taifa, ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee, Oktoba 12, 2009, alikuwa na haya ya kusema.

“Kwa vyovyote vile, Mwalimu hakuamini, wala sikumbuki kwamba alisema waziwazi kwamba anaamini kwamba ubepari ni imani. Ubepari ni mfumo, si imani,” alisisitiza.

Profesa Shivji aliongeza kuwa “Ulimbikizaji mtaji ndio kiini cha mfumo wa kibepari. Uhai wa bepari kama bepari hutegemea ulimbikizaji. Bila ulimbikizaji bepari hawezi kuishi kama bepari.”

Alipokuwa akilizungumzia suala la ufisadi alisema kuwa enzi za Mwalimu ufisadi haukuwapo, ila rushwa ilikuwapo. Mwalimu mwenyewe alikuwa akirudiarudia kauli hii ‘Rushwa ni adui wa haki,’ lakini msamiati wa ufisadi haukuwa katika serikali yake.

Hii ikimaanisha kuwa ufisadi ni rushwa iliyoota mizizi na kukua kuliko kawaida. Kwa mujibu wa Mwalimu rushwa ni kishawishi unachotoa ili mpokeaji aipinde sheria au taratibu rasmi kwa kumrahisishia mambo yake mtoaji.

Kwa mfano mtu anapotoa Kitu au fedha ili mgonjwa wake asikae katika foleni ya kumuona mganga, hiyo ni rushwa, na mpokeaji ataitumia kwa matumizi yake ya lazima au ya binafsi. Kwa maana nyingine pesa hiyo itatumika kulipia kodi na itarudi kwenye mzunguko. Kutakuwa na uvunjifu wa haki na utovu wa maadili, ila uchumi wa  nchi hauwezi kuyumba kwa rushwa hiyo.

Ufisadi ni neno la Kiswahili linalotokana na lugha ya kiarabu lenye maana ya kuharibu au uharibifu. Mtu anapoitwa fisadi maana yake ni muharibifu wa jambo au kitu. Hivyo mafisadi ni waharibifu wa mali za umma na uchumi kwa ujumla. Ni wa kuogopwa.

Profesa Shivji anaamini kuwa mfumo wa uliberali mamboleo ndiwo uliozaa ufisadi. Labda utajiuliza uliberali mambo leo ndiyo nini?

Kutokana na makala yaliyochapishwa na gazeti la wiki la Raia Mwema, ukurasa wa 19, toleo namba 112 la tarehe 16 Desemba, 2009.  Profesa Shivji anaeleza kuwa: Misingi mikuu ya mfumo wa uliberali mamboleo ni:
. Ulegezaji wa masharti ya biashara ya nje na ndani, kwa maana ya kwamba serikali haidhibiti tena biashara.
. Ulegezaji wa masharti ya soko la fedha na fedha kwa ujumla, kwa maana kwamba yeyote yule anaweza akaingiza na kutoa fedha nchini bila kudhibitiwa. Kwa kifupi, kuwa na soko huria katika bidhaa na fedha.

Hayo ni masharti ya wafadhili na taasisi za kibeberu. Maana yake ni kuwa serikali inapoteza uwezo na haki yake ya kujiamulia mambo muhimu ya sera na mwelekeo wa nchi kwa faida ya watu wake kinyume na ilivyoainishwa katika katiba yetu  kuwa, “watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya Nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao”.

Katika kijitabu cha Azimio la Arusha, cha mwaka 1967 ukurasa wa 16, suala la uwekezaji linazungumziwa na Mwalimu Nyerere, kama moja ya njia za kujipatia fedha za nje, ila akasisitiza kuwa ni njia ya hatari. “Aina ya tatu, ambayo pia ni kubwa…. Ni ile ya fedha za watu au makampuni yanayotaka kuja katika nchi yetu kuanzisha shughuli mbalimbali za uchumi kwa manufaa yao wenyewe. Na sharti kubwa walitakalo jamaa hawa wenye fedha zao ni kwamba shughuli yenyewe iwe ni ya faida kwao na pia kwamba serikali iwaruhusu kuondoa faida hiyo Tanzania na kuipeleka kwao. Hupenda pia kwa jumla serikali iwe na siasa wanayokubaliana nayo au ambayo haihatarishi uchumi wao.”

Utaona kwamba hali tuliyonayo sasa ya kukithiri kwa ufisadi ni kukomaa kwa kuzoeana katika mfumo wa kiuongozi. Urafiki na kuoneana haya ndivyo vilivyozaa ufisadi.

Swali langu la msingi linarudi palepale, ufisadi nao ni imani kama ulivyo ujamaa? Maana tangu kuasisiwa kwa ujamaa miaka ya sitini mpaka sasa wapo wazee ambao huwaambii kitu kuhusu imani yao juu ya ujamaa. Ukitaka kumuudhi mzee yeyote muasisi wa TANU, basi jaribu kumwambia ujamaa haufai, anaweza hata kukuchapa bakora japo hajimudu hata kuamka.

Hali inavyobashiri miaka kumi na zaidi ijayo ufisadi nao unaweza kuwa ni imani itakayobaki vichwani mwa wazee wa baadae, na kuamini kuwa ‘kula nchi’ ndiyo malipo ya usumbufu walioupata ima kwa kugombea nafasi fulani ya uongozi au kutafuta elimu.

Maana sasa ni wazi kuwa hata wanafunzi wa vyuoni wanauzungumzia ufisadi kwa mkabala wa ushujaa. Si ajabu kumkuta mwanafunzi wa shahada ya uhasibu akikuambia, “yaani elimu ninavyoipata kwa taabu hivi halafu nisiwe fisadi? Hiyo haiwezekani” jamani hii si ni hatari?
                                                



No comments:

Post a Comment