Wednesday, October 20, 2010


KICHEFUCHEFU CHA HABARI KIMEANZA TANZANIA

Na Hafidh Kido

Mwaka jana nilihudhuria mdahalo wa wazi ulioandaliwa na jukwaa la majadiliano ya wanafunzi wa chuo chetu- Kampala International University (KIU Student Forum Debate), mdahalo ulihusu mswada wa uchaguzi kwa nchi za jumuia ya Afrika ya Mashariki.

“Will the proposed East African Election Bill solve the election problems in east African?” tafsiri yake “Je pendekezo la mswada wa uchaguzi kwa Afrika ya mashariki utatatua matatizo ya uchaguzi kwa nchi wanachama?” hicho ndicho kilikuwa kichwa cha habari cha mdahalo huo.

Mwanzoni mwa mwaka jana baadhi ya viongozi na wasomi kutoka nchi wanachama wa jumuia ya Afrika mashariki, walikutana jijini Kampala nchini Uganda, kujadili mswada wa uchaguzi wa pamoja kwa nchi wanachama ili kuepusha vurugu za uchaguzi, wakichukua hadhari kwa yaliyotokea Kenya mwaka 2005.

Walialikwa baadhi ya wabunge toka bunge la vijana wa Uganda, wengi walichangia kwa majibizano kama ilivyo hulka ya wabunge wetu hasa wakiwa wanatoka vyama tofauti. Lakini nilichokuja kugundua ni kuwa wote waliishia kutoa sababu zilizofanana ingawa waliamini wanatofautiana mawazo.

Mzungumzaji wa kwanza aliitwa bwana Asiimwe steven, kutoka chama tawala cha NRM (National Resistance Movement) cha bwana Museveni, Rais wa Uganda. Bwana Asiimwe, alisema kuwa ifike wakati vyama vya upinzani vikubaliane na ukweli hasa wa matokeo ili kuepusha vurugu za baada ya uchaguzi.

Alitoa kichekesho na kusema, “ ikiwa wapinzani wanadai Rais Museveni amezeeka basi na wao walete mtu mwenye sifa kama za Museveni, na si kulaumulaumu tu” alikwenda mbali zaidi pale alipowaambia wakenya “Wakenya msiwe na sifa juu ya Obama, tengenezeni Obama wenu, yule hawezi kuwa rais wa Kenya.”

Utaona maneno yake ni ya msingi kwa namna fulani, bwana huyu ingawa alimsifia kiongozi wake wa chama Generali Museveni, lakini utaona anahubiri amani. Haamini katika vurugu, ikiwa unadhani Museveni amezeeka basi mchague ‘Dk. Kizza Besiggye’ huyu ni kiongozi wa chama cha upinzani cha FDC (Forum for Democratic Change), na si kupiga kelele.

Mzunguzaji wa pili bwana Erick Sakwa, kutoka chama cha UPC (   ). Yeye anaamini katika utoaji wa taarifa sahihi. Anasema kuwa “taarifa ndiyo oxsijeni (oxygen) ya demokrasia. Hatuwezi kuanzisha jukwaa la kujadili mswada wa uchaguzi wa pamoja kwa nchi tano zenye historia tofauti za kisiasa bila ya kuzingatia viongozi wao wameingia madarakani kwa namna zipi”

Utaona hoja yake ipo kihistoria zaidi, ufinywaji wa taarifa juu ya historia za viongozi na vyama vyao ni suala la kuzingatia sana. Na hapa ndipo ninapopatia ufunguo wa mada ya makala haya. Hakika kichefuchefu kimeshaanza Tanzania, historia za viongozi wetu wanavyoingia madarakani tunajua wenyewe. Wizi, ulaghai na lawalawa kwa wananchi hushamiri katika kipindi cha uchaguzi.

Nipo mbali na nyumbani lakini si haba wa taarifa za kila linalojiri huko, nasikia viongozi wetu wameoa wake watatu- siasa, dini na taaluma ya uandishi wa habari. Kitakachofuata ni kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo. Maana watoto watakuwa wa baba mmoja ila hawapatani, ya Rwanda, Kenya, Burundi na Uganda kidogokidogo sasa yatahamia Tanzania.

Waswahili wana usemi wao kuwa mtu akiwa na tabia nzuri tangu utotoni na kuharibikiwa ukubwani huyo hufananishwa na mung’unya. Hivyo Tanzania yetu kisiwa cha amani imegeuka mung’unya kuharibikia ukubwani.

Katika mjadala ule kila nchi ilitoa sababu zake ni kwanini mswada huo wa uchaguzi wa pamoja hautoweza kutatua matatizo ya uchaguzi katika nchi tano hizi.

Wakenya walizungumzia  ukabila kuwa ndiyo sumu, maana kila kabila linataka mtu wao ndie aongoze nchi, na wakikuyu bado wanataka kuitawala Kenya- ukiangalia tangu baba wa taifa la Kenya Mzee Kenyatta, Moi na Kibaki, wote ni wakikuyu, hivyo hawataki kuiachia hiyo kamba.

Waganda wao walizungumzia ukabila na ujeshijeshi uliotawala Uganda. Maana Uganda mpaka sasa inatawaliwa kijeshi tangu mapinduzi ya mwaka 1986, yaliyomng’oa madarakani Tito Okello, nae alimtoa Milton Obote, mwaka 1985, Obote aliingia kwa uchaguzi mwaka 1980, ambapo kabla ya hapo alikuwapo Paulo Muwanya, aliekuwa mwenyekiti wa tume ya kijeshi iliyomtoa madarakani Godfrey Binaisa, 1979.

Binaisa yeye alimng’oa Yusuf Lule, aliewekwa na Mwalimu Nyerere baada ya kuondolewa Nduli Idi Amin Dada, mwaka 1979. Nae Idi Amin, alimtoa madarakani kijeshi Milton Obote, mwaka 1971, na Obote nae akisaidiwa na Idi Amin walimtoa Kabaka Muteesa, ambae alipokea uhuru mwaka 1962 kutoka kwa waingereza akisaidiwa na Benedicto Kiwanuka, ambae alishinda uchaguzi wa March 1,1961, chini ya chama cha Democratic Party (DP), na kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Uganda huru.

 Lakini baadae walipoamua kuunganisha vyama vya DP cha Benedicto Kiwanuka na UPC cha Milton Obote, ndipo Obote akawa waziri mkuu wa pili chini ya Kabaka Muteesa, kama rais na mfalme wa Buganda Kingdom.

Utaona tangu Uganda ipate uhuru hali haikuwa nzuri, Museveni ndie rais wa kwanza kukaa madarakani kwa muda mrefu.

Kingine kinachoitafuna nchi ya Uganda ni ukabila, mpaka sasa Buganda Kingdom wanadai madaraka yao waliyonyang’anywa na Obote kutoka kwa Kabaka Muteesa, ambae alikuwa mfalme wa Buganda Kingdom na rais wa kwanza wa Uganda huru. Na mpaka sasa Buganda Kingdom wanataka Federal Government (Serikali ya majimbo) kama ilivyo Marekani.

Uganda kila kabila linaongozwa na mfalme, ina maana Museven ni kama anaongoza Serikali kuu akiwa Kampala tu, lakini kila kabila lina kiongozi wake wanawaheshimu kuliko rais wa nchi.

Na hapo palipo na Ikulu Kampala, ni eneo la Buganda Kingdom, serikali inatakiwa ilipe kodi kwa Buganda Kingdom, yaani kuna fungu linaingia kila mwaka katika serikali ya Buganda Kingdom na wana bunge lao linaitwa Lukiiko na wana waziri mkuu wao anaitwa Katikkiro kwa cheo, na jina lake ni J.B.Walusimbi. Mfalme wao wa sasa anaitwa Kabaka kicheo, jina lake halisi ni Ronald Mutebi, inakanganya eeenh!.

Mwaka jana jijini Kampala kulikuwa na vurugu baina ya Buganda Kingdom na Museveni, Kabaka Mutebi alikuwa anataka kuwatembelea watu wake sehemu fulani, lakini Museveni akataka kuonyesha yeye ni zaidi akamkatalia, kilichotokea ni wabaganda kulala barabarani, wakatumwa askari pamoja na wanajeshi kuwatawanya, ila kilichofuata ni mapigano, vita hasa.

Sisi hatukutoka kuenda mjini wala sokoni ni ndani tu, watu waliuwawa, wengine walipoteza viungo, redio za Buganda kingdom zilifungwa na baadhi ya wabaganda mpaka sasa wapo rumande wanasubiri kusomewa mashtaka.

Tanzania kukitokea vurugu huletwa FFU, lakini Uganda wanaletwa wanajeshi na vifaru, mabomu na kila silaha nzitonzito, ukiwanyooshea kidole tu umeumia.

Burundi na Rwanda hakukuwa na wachangiaji, lakini tunafahamu ingawa hali kwa sasa imetulia lakini ukabila na ujeshijeshi bado kuisha katika nchi hizo.

Tanzania mimi ndie nilechangia mada, lakini kabla sijasimama wachangiaji walionitangulia waliisifia nchi yetu kwa amani na utulivu. Wakasema Tanzania hakuna vurugu za baada ya uchaguzi, na nchi yetu ina amani na utulivu kiasi wao wanapaswa kuiga kwetu. Nilichekea kiganjani.

Sikutaka kuharibu jina la nchi yetu, lakini yaliyo moyoni Mungu mwenyewe ndie anaejua, maana huwa tunalazimishwa kujiua wenyewe, amani aliyoiacha Mwalimu Nyerere imeshapotea, siku hizi sauti za mabomu, milio ya risasi tumeshavizoea. Lakini hayo yote wenzetu hawayajui.

Nilichofanya ni kuwazindua kuwa ni kweli vurugu hakuna maana viongozi wetu wameshajua pa kutukamatia siku hizi, ni pahali padogo sana, ni kiasi cha kudhibiti imani mbili, ya dunia na akhera.

Imani ya dunia ni kudhibiti waandishi wa habari, ima kwa kuwatisha au kuwanunua, na imani ya akhera ni kuwadanganya waumini wa dini mbili kuu, uislamu na ukristo. Nakumbuka wakati Rais Kikwete anaomba kura mwaka 2005, aliitwa chaguo la Mungu na viongozi wa kikatoliki, na akapewa biblia ili imlinde.

Hakuishia hapo, akawaahidi waislamu kuwa atawaletea Kadhi ili aweze kutatua matatizo yao madogomadogo, lakini mpaka sasa ni wimbo. Hivyo mada yangu kuu ilikuwa ni kuwazindua wana Afrika mashariki wenzangu kuwa si kuwa Tanzania kuna amani ila tumetiwa mtungini sauti zetu hazitoki. Na uoga unatunyima kutukutika.

Hivyo naomba niseme kuwa kwa kuwa uchaguzi umebakia siku chache utaona ziara za viongozi wote lazima zitabeba waandishi wa habari. Bahasha zitakuwa nyingi na ziara za kutembelea vyombo vya habari hazitokwisha. Misikiti itapata mabusati mapya na kupakwa rangi, makanisa yatapata wageni rasmi wengi katika harambee za ujenzi wa majengo ya kanisa.

Harufu mbaya imeshaanza kusikika, kichefuchefu kitatusababishia kutapikia viatu vya wajumbe wa usimamizi wa zoezi la upigaji kura. Watakimbia kutoa taarifa za uongo, kumbe wanaepuka harufu ya matapishi. Naomba kuwasilisha.





No comments:

Post a Comment