Na Hafidh Kido (Kampala Uganda) 16th October, 2010 Saturday.
Wanafunzi wa Kampala International University (KIU) main campus cha jijini Kampala Uganda, jana usiku walifanya vurugu kupinga ongezeko la faini katika ada yao.
Vurugu hizo zilikuja baada ya wanafunzi wenye hasira kali kukusanyika katika viwanja vya chuo wakisubiri kuisha kwa kikao cha bodi ya wakurugenzi ambapo Rais na spika wa bunge la wanafunzi waliwawakilisha wanafunzi wenzao katika kikao hicho kilichofanyika jana mchana tarehe 15 mwezi huu.
Akizungumza na wanafunzi baada ya kutoka katika kikao Rais huyo wa wanafunzi chuoni hapo bwana Ignatius Muhatia, mwanafunzi kutoka Kenya alisema chuo hakizingatii utoaji elimu na badala yake wanafanya biashara huku wakiwaminya wanafunzi kwa kuwatoza faini kubwa.
“Ikiwa mwanafunzi ameshindwa kulipa ada yake ndani ya muda uliopangwa vipi ataweza kulipa faini ya dola 150 za kimarekani ambayo ni karibu asilimia thalathini ya ada,” alihoji Muhatia.
Wanafunzi hawakuishia hapo bali walikwenda mbali zaidi na kumtaka mmiliki wa chuo ambae ni mfanyabiashara maarufu nchini Uganda bwana Hassan Bassajabalaba, kuongea nao na si askari wala viongozi wa wanafunzi.
Hali ilipofikia hapo mmiliki huyo wa chuo alijaribu kuingia ndani ya gari na kuondoka eneo la chuo lakini wanafunzi walilala chini kwa lengo la kumzuia asitoke, baada ya kuona hivyo bwana Bassajabalaba aliwataka askari polisi wamchukue Rais wa wanafunzi na kumuingiza katika ofisi yake kwa madai anataka kuzungumza nae.
Hapo ndipo vurugu zilipoanza kwa kuanza kurusha mawe katika vioo vya jengo la utawala, huku wanafunzi wengine wakiimba kwa sauti kuwa wanataka kiongozi wao aachiwe.
Nae spika wa bunge la wanafunzi Thon Michael mwanafunzi kutoka Sudani alisema walijaribu kuwatuliza wanafunzi ili wasifanye uharibifu lakini walishindwa kwa maana kila mtu alishachoshwa na vitendo vya chuo kuwadharau na kuona kama wao hawawezi kudai haki zao. Na kudai mmiliki huyo amewadharau kwa kuwaambia hawawezi kufanya lolote kwani analindwa na serikali ya Uganda.
“Tumejaribu kutumia nafasi zetu kuwatuliza wanafunzi, lakini tumeshindwa kwa maana walisisitiza kutaka kuongea na mmiliki mwenyewe wa chuo,” alisema spika huyo.
Jitihada za kumpata mmiliki wa chuo zilishindikana kwani simu yake ilikuwa haipatikani, na polisi hawakuruhusu mtu yeyote kusogea zilipo ofisi za mmiliki huyo.
Baada ya wanafunzi kufukuzwa eneo la chuo waliamua kuzagaa mitaani na kupora maduka, katika migahawa ya jirani kama krunchy Bite na Chicken Tonight ambapo walikula vyakula na kuvunja baadhi ya vifaa vya migahawa. Baadhi ya wanafunzi walisikika wakisema kuwa hiyo ndiyo siku yao kuingia humo kwani ni migahawa ghali sana na wasingeweza kuingia tena.
“Nisipoingia leo Chicken Tonight siwezi kuingia tena mpaka namaliza chuo, kila siku naiona kwa nje tu wacha leo nikale kuku wa bure,” alisikika mwanafunzi mmoja huku akiingia na wenzie mgahawani humo.
Hata hivyo mpaka kufikia saa moja ya usiku askari wa kutuliza ghasia walifika eneo la chuo na kuanza kutawanya wanafunzi waliokuwa na hasira kali, baada ya askari polisi takriban hamsini kushindwa kuwamiliki wanafunzi hao. Vurugu zilizidi kuwa kali na baadhi ya wanafunzi walitiwa nguvuni, wengine kujeruhiwa na mmoja kukimbizwa hospitali baada ya kupigwa risasi ya plastiki kichwani.
Askari wa kutuliza ghasia hawakuishia hapo tu, bali waliingia hostel za wasichana zenye jina la aliekuwa Rais wa Sudan ya Kusini John Garang, na kuanza kuwatoa wasichana wote wengine wakiwa nusu uchi huku wamenyooshewa mitutu ya bunduki na mabomu ya machozi.
Hatua hiyo iliwaudhi wanafunzi wa kiume na kurudi tena eneo la chuo kwa madai ni uonevu kuwatoa wakinadada hali walikuwa wamejifungia na hawajihusishi na vurugu hizo. Hali hiyo iliongeza vurugu na kuanza kuwafukuza wanafunzi mpaka katika makazi ya watu katika eneo maarufu liitwalo Nabutiti eneo ambalo wanafunzi wengi wamepanga vyumba.
Magari yaliyokuwa yakipita karibu na chuo yalitupiwa mawe na kila aliepita aliingizwa katika mkumbo kwa kuchapwa viboko na askari wa kutuliza ghasia.
Moshi wa mabomu ya machozi ulisambaa kote na milio ya risasi ilisikika hewani hali iliyofanya biashara zote kufungwa na watu kujifungia ndani. Barabara maarufu ya Ggaba ilifungwa na hakuna magari kupita mpaka saa tatu na nusu ya usiku kuanzia saa kumi na moja ya jioni.
Chanzo cha vurugu hizo ilikuwa ni mgomo wa kuhudhuria darasani uliofanyika wiki mbili zilizopita, mgomo huo ulikuwa unautaka uongozi wa chuo kuangalia mambo manne muhimu. Moja ni kuondolewa kwa faini, pili ni kufunguliwa kwa mageti yote ya chuo, kwa maana kwa sasa yanatumika mageti mawili tu katika matano wakidai lengo ni kuimarisha ulinzi baada ya tukio la alshabab.
Lakini kulikuwa na tukio la kudhalilishwa kwa akina dada wa kiislamu baada ya kupekuliwa na askari wa kiume na kuwashika sehemu nyeti, na wanafunzi kulalamika kupanga mistari mirefu kusubiri kupekuliwa hayo yote yalikuwa katika mambo muhimu yaliyosababisha mgomo wa masomo uliodumu kwa siku nne.
Kadhalika jambo la tatu lilikuwa ni kuongezeka kwa ada ya mahafali, ambapo kila mwaka inaongezeka asilimia Fulani.
“Mfano mahafali ya mwezi ujao kila muhitimu anapaswa kulipa ada ya dola 180, lakini katika dola zote hizo guo la kuhitimu unanunua mwenyewe, booklet la majina ya wahitimu unanunua na hakuna chakula cha jioni wala nini zaidi ya chupa ya soda au maji. Sasa fedha zote hizo zinakwenda wapi, Ikiwa wanahitimu takriban wanafunzi elfu tano jumlisha dola 180, je si ni wizi huo,” alihoji mwanafunzi mmoja anaesubiri kuhitimu.
Suala la mwisho lililosababisha mgomo wa wiki mbili zilizopita lilikuwa ni kupotea kwa mitihani, kukosa matokeo ya mitihani kwa waliofanya mitihani na kukamilisha kila kitu pamoja na kukosa usahihi wa matokeo ya jumla kwa kila mwanafunzi. Suala hilo ni tatizo la muda mrefu ambalo linafanya wanafunzi kukosa utulivu na kupata taabu wakati wa kukusanya matokeo yote wakati wa kuhitimu.
Baada ya mgomo huo wa siku nne kuombwa kusitishwa ili kusubiri kikao cha tarehe kumi na tano mwezi oktoba mwaka huu siku ya ijumaa, ndipo wanafunzi walipoamua kuchukua sheria mkononi baada ya mambo waliyoomba kutupwa kapuni na kikao hicho cha bodi, na kauli iliyosambaa chuoni kutoka kwa mmiliki wa chuo kuwa ‘wanafunzi hawawezi kufanya chochote kwa maana serikali inanilinda na hiki ni chuo changu wafanye wanavyotaka nitawadhibiti’ ndiyo iliyosababisha yote haya.
MWISHO
No comments:
Post a Comment