Tuesday, October 19, 2010

Barua kwa marehemu baba

Na Hafidh Kido


Kwako baba

Ama baada ya salam natumai huko uliko unaendelea kufaidi thawabu za utu bora na ibada njema ulizokuwa ukizifanya huku duniani. Sisi huku ni wazima, tangu uondoke miaka sita sasa imefika lakini  familia yako bado tunakukumbuka.

Mimi nimefanikiwa kuingia chuoni, Juma ameamua kuenda ughaibuni kutafuta maisha bora kwa kila mtanzania baada ya aliyoahidiwa hapa Tanzania kutotimia, Meddy maisha ya Afrika ya kusini yalimshinda ameenda kwa wazungu kubahatisha tena kama mkimbizi, Nafisa bado yupo sekondari na mama yupo nyumbani tu maisha yamekuwa magumu.

Zile kashata, mikate ya kumimina na biashara ndogondogo alizokuwa akifanya kwa sasa bwana dakitari amemkataza kufanya maana moto hauwezi tena, baada ya kuzifanya biashara hizo kwa miaka kumi na tano bila mafanikio kwa sasa anaishi kwa rehema ya Mungu tu kama lilivyo jina lake Rehema binti katani. Ila tunamshukuru Mungu kwa kuendelea kumpa umri kaka yetu mkubwa Abdul alie ughaibuni, maana ndie anaenisomesha na kuisukuma familia kila anapopata nafasi.

Lengo la barua hii si kukuelezea namna familia yako inavyoishi tangu uifariki dunia, ila ni kutimiza ile ahadi tuliyowekeana kuwa nikuandikie barua kila ninapopatwa na matatizo yasiyo ya kawaida. Ingawa nilikutupa lakini barua hii inaweza kukutoa machozi, sijui kama huko kuzimu bado mnalia.

Tatizo lenyewe linahusu elimu, kitu ulichoniusia nisikipuuze, na kuwa ndiwo utakuwa ufunguo wangu wa kuingia katika chumba cha maisha pindi nitakapokuwa tayari.

Nipo Kampala nchini Uganda, nafanya masomo ya mawasiliano ya umma ngazi ya shahada. Lakini maisha ya kiuanafunzi yamekuwa magumu kuanzia ada, fedha za kujikimu na utanzania wangu. Usishangae, utanzania wangu pia umekuwa kikwazo katika nchi hii ya Uganda ambayo ulinambia muliikomboa kutoka katika mikono dhalimu ya nduli iddi Amin dada, chini ya amri ya amiri jeshi mkuu Mwalimu Nyerere ambae upo nae huko.

Maisha si kama nilivyoyatarajia, tunanyanyasika kwa utaifa wetu. Hapa chuoni kwetu wageni tunalipishwa ada kwa pesa za kikoloni au unaweza kuita dola, lakini wenyeji  kwa maana ya waganda wanalipa ada kwa kutumia pesa za matoke au shilingi. Inasikitisha kidogo, maana wanalipa karibu nusu ya tunavyolipa. Lakini tunakaa darasa moja na kupata elimu sawa bila kupunjwa, duka moja bidhaa moja ila bei mbalimbali. 

Elimu ni biashara sasa baba, tofauti na ulivyokuwa ukinielezea kuwa hata kipindi chenu vyuo vikuu vilipatikana Kenya na Uganda. Lakini wewe kule Kenya ulisoma kwa raha bila ya kubaguliwa wala kunyanyaswa. Mlilipa pesa sawa na kila kilichohusu kutoa fedha hakikutolewa kwa matabaka. Na nakumbuka ulinambia wakati huo jumuia ya Afrika ya mashariki ilikuwa bado kuanzishwa, baada ya ile ya mkoloni kuvunjika.

Hapa ninapokuandikia barua hii nipo katika chumba kidogo kama kile choo chetu pale kijitonyama, ndiyo baba sijakosea najua kulinganisha ukubwa wa chumba changu sasa, kwani nimeshakua mkubwa. Kama hujaelewa vizuri chumba kina urefu wa futi kumi na upana wa futi nane, ninakilipia dola mia mbili na thalathini au shilingi laki nne na nusu za Uganda sawa na laki tatu na kiasi za kitanzania kwa miezi mitano au minne kulingana na urefu wa muhula wa masomo. Wakati kwetu Tanzania ninapata chumba na sebule kwa pesa hiyo.

Chuoni wageni wote tunalipa kwa mfumo wa dola na ukichelewa kumaliza ada yako mwezi mmoja tu baada ya kuanza muhula unatakiwa ulipe faini ya asilimia thalathini ya ada yako, baada ya wiki mbili inazidi na kuwa asilimia sitini ya ada yako, wiki mbili tena unalipa dola thalathini wiki mbili tena unalipia dola sitini, inakwenda hivyo mpaka ikikaribia mitihani unalipia ada yote ukiambatanisha na asilimia sitini ya ada yako bila kusahau faini ya dola mia na ishirini. 

Ngoja nikupe mfano kama hujaelewa, mfano mimi ada yangu kwa muhula ni dola mia nane na hamsini, nikichelewa natakiwa nilipe asilimia thalathini ya ada ambayo ni dola mia mbili hamsini na tano, baada ya wiki mbili ni asilimia sitini ya ada ambayo inakuwa ni dola mia tano na kumi. Na ikiwa hujalipa mpaka karibu na mitihani unalipia dola mia nane hamsini ambayo ni ada jumlisha mia tano na hamsini ambayo ni faini ya awali bila ya kusahau dola mia na ishirini faini ya pili. Unyonge ulioje huu. 

Najua utakuwa hujaelewa kwa maana ulikuwa hupendi mahesabu ya fedha, hakika yanakanganya hasa fedha zenyewe ukiwa unadaiwa. Kifupi nilichotaka kukuambia ni kuwa kwa sasa hatuedi chuoni kwa maana wanafunzi tumeitisha mgomo kupinga hizi faini zisizo na tija. Maana maprofesa wa chuo wamefikia ukomo wa kufikiri, ikiwa nilishindwa kulipa ada yenyewe kwa muda, vipi nitaweza kulipa faini inayokaribia sawa na ada yenyewe? Nini kama si kukosa akili.

Unakumbuka zile vurugu zilizotokea chuo kikuu cha Dar es salaam mwaka 1966? Ulinambia wakati huo ulikuwa Shinyanga au sijui ni Nairobi bado unasoma, sikumbuki vizuri lakini wewe ndie ulienielezea vurugu zile kuwa wanafunzi walikuwa wakidai haki zao. Walikuwa wanapinga kupelekwa jeshini na kukatwa pesa zao za kujikimu hali ‘wabenzi’ wakina Kambona walikuwa wanapata mishahara minono.

Sasa mgomo wetu ni kupinga kulipishwa ada mara mbili hali elimu na huduma tunayopata hailingani na tunacholipia. Kuna mitihani mingi ya wanafunzi imepotea bila ya kusahihishwa, waalimu hawaingii madarasani kama ipasavyo, huduma za afya chuoni ni mbovu, na waliofanya mitihani baadhi matokeo yao hayaoekani. Lakini hayo yote hayashughulikiwi mwenye chuo anajali ada yake tu na faini.

Mfano mzuri ni mimi mwanao, mwaka jana nililipa ada yangu mapema kabisa bila ya kukatwa faini, nilikuwa mtoto mwema. Nikahudhuria darasani kwa zaidi ya asilimia tisini, nikapongezwa na wakufunzi wangu, na nikafaulu majaribio ya darasani, nikakaa kweye mtihani wangu wa mwisho kama inavyotakiwa. Lakini baada ya matokeo kutoka, wenzangu matokeo yao wa liyapata  ila mimi  yakwangu hayakutoka, nilipouliza nikaambiwa sikulipa ada. Nilitaka kuzirai kwa kiwewe.

Nilifuatilia ofisi za fedha nikakuta nimelipa ila jina langu halikuwa limeingizwa katika mfumo wa kumpyuta nakumbuka baba kompyuta ulikuwa ukiita ‘dubwana’ au kinakilishi. Kumbe ni mchezo wao, usipofuatilia pesa zako zinakuwa zimeliwa na wajanja halafu ukilalamika sana wanakuita mkorofi na wanakufukuza chuo na unabaki mtaani kama mtoto wa Yule mzee pale mtaani ambae ulikuwa unasema laiti ungepata  fedha ungemsomesha, utafikiri wewe ndie rais wa nchi. Baba nae ulikuwa unapenda sifa..

Basi baada ya kufuatilia nilipata baadhi ya matokeo yangu, ila somo moja la ‘modern and classical political thought’ niliambiwa na mkufunzi wa somo hilo kuwa mtihani wangu hajauona, hali nilisaini katika orodha ya waliofanya mtihani na katika chumba cha mtihani mkufunzi aliniona. 

Sikuridhika na jibu hilo nilifuatilia kila idara kwa makini, jibu nililopata ni kuwa nirudie somo hilo tena kwa kuhudhuria vipindi vyote, ninunue upya vitini vya masomo ambavyo  ni ghali sana, na kama hiyo haitoshi nilipie dola kumi kama gharama za mtihani. Kwa maana nyingine mtihani niliokwisha kuusoma, kuulipia, kuukalia darasani na kupoteza muda, sasa niulipie tena. Hali makosa ni yao kwa kutofanya kazi kiumakini, nililipa ada yangu mapema kuepuka usumbufu na risiti niliwaonyesha ila hilo walidai haliwahusu. Hivi ndivyo tunavyosoma Kampala International University, Uganda.

Nakumbuka wakati nikifanya mazoezi ya uandishi wa habari pale New Habari cooperation, kuna mzee mmoja anaita Kakoloboji Mwandaji, aliniuliza “kwanini umeamua kuenda kusoma Uganda wakati hapa Tanzania tunavyo vyuo vizuri tu vya shahada ya mawasiliano ya umma?”

Nilikosa jibu la kumpa lakini nilidanganya ati wewe ndie ulienishauri, wakati najua fika wewe hukuwa duniani wakati mimi najiunga na chuo huku Kampala. Hivyo kimbelembele changu cha kusikia mambo nikadakia sasa kinaniponza.

Wiki iliyopita chuoni kulitokea maandamano ya kudai haki, lakini mmiliki wa chuo aliyaita vurugu na kuita askari wa kutuliza ghasia. Lakini cha kushangaza askari hao walishindwa kutuliza ghasia na badala yake waliongeza ghasia kwa kuwasulubu hata wasio na hatia.
Waliingia katika hosteli za kina dada na kuwaadhiri, wengine walikuwa wanatoka msalani waliwavua nguo, waliwapiga na kuwatoa katika vyumba vyao huku wakiwadhalilisha bila ya kosa lolote. Maana wao walikimbilia vyumbani mwao na kujifungia ili kulinda maisha yao, lakini askari hao waliona haitoshi, maana waliwaingilia humohumo vyumbani na kuvunja milango yao, fedheha iliyoje hii.

Kwa leo sina mengi, ila nilitaka kukuambia tu kuwa usishangae kusikia lolote baya limetutokea wanafunzi wa Kampala International University, maana tupo katika kipindi kigumu, mgomo baridi unaendelea lakini sioni ukiisha salama. Maana bado kuna wanafunzi ambao wanaingia madarasani, na kuna wanaopanga kuwaadhibu hao wanaotusaliti tuliogomea masomo. Na hapo ndipo vurugu zitakapoanza.

Nimesikia chuoni kuna askari maalum takriban hamsini wameletwa, wana silaha nzito na wameambiwa waue kila atakaethubutu kufanya vurugu chuoni hapo. Mimi sijagusa mlango wa chuo wiki inafika sasa.

Maana Uganda ni nchi ya jeshi, kuuana si jambo la ajabu, na kufuatia kulipuliwa kwa mabomu na Al Shabab kumewafanya askari wawe makini na kila vurugu ianzishwayo. Alaa kumbe baba huna taarifa za Al shabab, hawa ni wanamgambo wa kikundi cha kigaidi cha kisomali, kinahusishwa na milipuko miwili ya mabomu iliyoua watu karibu elfu moja na wengine kujeruhiwa katika ukumbi wa Ethiopian Village uliopo karibu na chuo chetu, na mlipuko mwingine ulitokea katika uwanja wa gofu hapahapa kampala.

Jambo jingine linalofanya nihofie maisha yangu ni kuwa sasa Uganda ipo katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge. sasa vurugu zozote zinahusishwa na siasa chafu, hivyo serikali hutumia kila namna au mbinu kuzuia machafuko kwa kutoa mfano kwa wale wanaojaribu kuvuruga amani.

Sina mengi, wako umpendae kwa dhati niendelezae wajihi wako na kipaji chako cha uandishi wa mashairi. Maana kila anaeniona anasema ati nimefanana na wewe. Watu bwana wambea kweli.
                                                                 Hafidh A. Kido
                                                                        Wakatabahu.


No comments:

Post a Comment