Na Hafidh Kido
Ni kawaida katika mahusiano kuwa na magomvi yasiyokwisha juu ya wapenzi kutoka nje ya mahusiano; si jambo la ajabu tena kwa maisha ya sasa yaliyochanganyika tamaduni na historia mbalimbali.
Kama mwandishi na mdadisi wa maisha ya kila siku yamuhusuyo mwanadamu, nimegundua sababu saba ambazo humfanya mwanamke ama mwanamme kukosa uaminifu katika mahusiano.
Nimekuwa nikijiuliza kwa muda mrefu juu ya suala hili la kukosa uaminifu katika mapenzi, kwa maana sikuona sababu ya msingi kwa mtu kutoka nje ya mahusiano.
Kipi hasa kinachomfanya mtu akakosa uaminifu juu ya mpenzi wake. Je ni starehe za kitandani? Ni starehe za maisha na raha za mahaba? Au ni tama tu za kimwili..
Lakini waswahili husema utu uzima ni dawa, ingawa sijawa mtu mzima wa hivyo kusema nimeona megi; ila maisha ya sasa hata watoto tunakutana na misukosuko inayotulazimu kukua kabla ya umri kufika.
Nitaziainisha sababu hizo saba kwa maelezo ya kutosheleza, ikibidi nitatoa mifano ya kusaidia kuelewa mada kwa utaratibi mzuri na mpangilio mwema rahisi kuelewa.
Sababu ya kwanza: ni Kupungua mapenzi; hii imekuwa ni sababu kuu ya kumfanya mtu atoke nje ya mahusiano. Kwani kawaida kuna watu hupenda kudekezwa au kupewa mapenzi motomoto bila kupungua hata chembe kwa kipindi chote cha mahusiano.
Kwa mfano; wakati penzi linapokuwa changa kuna kule kupigiana simu kila dakika, mtaongea hata upuuzi na kuchekacheka huku mkitaniana kama watoto wadogo. Ukila chakula fulani cha tunu utamwambia mpenzi wako, wakati unapika ukijikata na kisu kwa bahati mbaya utampigia simu mpenzi wako huku ukideka, na mengi kama hayo .
Mara nyingine mtatoka mandari (matembezi ya baharini au jioni), mkiwa huko baharini mtarushiana maji, mtamwagiana michanga huku mkikimbizana kwa vicheko.
Mara nyingine mnaweza kuwa mkahawani mkila ama mkinywa, mpenzi wako anaweza kukulisha ama akafanya kama anakulisha halafu anakwepesha au anakula yeye. Mradi tu mcheke ama umpige kofi kidogo la mahaba, na stihizai za kilimbukei. Lakini hayo ndo mambo ambayo wengi huwa nayo kwa kila penzi changa.
Baada ya kupita miaka miwili ama mitatu mambo kama hayo hupungua. Hamtakuwa na muda tena wa kuchezacheza namna hiyo. Inawezekana kazi zinawabana ama mwanamke anaweza kuwa amejifungua na mapenzi yote ameyahamishia kwa mtoto.
Hapo sasa mume huanza kutafuta kibinti kidogo kitakachomrudishia ile michezo ya awali aliyoizoea kutoka kwa mkewe. Unaweza kumkuta mzee wa miaka hamsini lakini wakati akiongea na kimada wake wa miaka ishirini huwezi kuamini, wanataniana na kuchekacheka kama mahantobwe au mahayawani wa mapenzi.
Kadhalika mume anaweza kubanwa na kazi, mke kila akijitahidi kupata nafasi ya kuchezacheza na mumewe huwekwa pembeni.
Anaweza kumpigia simu mumewe ofisini akaambiwa ana kazi nyingi wataongea nyumbani, akitoka kazini jioni amechoka, akishawekewa maji ya kuoga na kula huhamia mezani na ‘laptop’ yake anamalizia kazi za ofisini mpaka usiku mwingi, akitoka hapo hujiagusha kitandani na kulala, asubuhi na mapema kazini. Ikifika jumapili mama huanza kufurahia kwa kuona atakaa nyumbani na mumewe, lakini baba atasema ana semina Bagamoyo na atalala hukohuko.
Hivyo, hayo ndiyo matatizo yanayomfanya mume au mke kuanza kutafuta mtu atakaempa furaha kama zamani. Na ndiyo maana utakuta mume au mke hayuko tayari kuharibu ndoa yake, ila hutoka nje ya ndoa. Kumbuka hajachoshwa na ndoa, bali ni vitu fulanifulani tu anavikosa na ndivyo vinavyomfanya atoke nje.
Sababu ya pili: ni tamaa ya kupata zaidi ya akipatacho katika ndoa au penzi la kawaida tu la uchumba.
Inaweza kuwa ni tamaa ya fedha au utundu wa kitandani, husemwa mapenzi si fedha, lakini watu husahau kuwa mapenzi huendeshwa kwa kutumia fedha.
Chukulia utataka kutoka mandari na mpenzi wako, lazima mtahitaji kununua juisi, soda au chakula cha jioni kitakachowafanya muwe pamoja usiku huo. Vilevile hata kama mpo katika ndoa, ni vema siku mojamoja muende mkalale hotelini ili kubadilisha mazingira ili pendo lenu lizidi kushamiri.
Tazama mambo hayo yote yanahitaji fedha, si za kumuhonga mpenzi wako la hasha, bali ni kugharamia hayo matumizi ya kuimarisha pendo na kulipalilia furaha.
Ndiyo ukaona watu wengi huamua kutafuta wanaume au wanawake watu wazima wenye kipato kizuri ili wapate fedha za kuja kufurahi na wapenzi wao wanaolingana umri.
Na mara nyingine mwanume au mwanamke anaweza kuwa na mpenzi mwenye fedha, ila bado anatoka nje; sababu huwa ni kutafuta ridhiko la kitandani.
Zingatia hili: wanaume wengi hawawaridhishi wapenzi wao, huwa na pupa ya kukimbilia tendo bila kumuandaa mpenzi wake. Matokeo ni mwanamke kukaa katika mahusiano kwa miaka miwili lakini asiridhishwe kimahaba na mpenzi wake. Hivyo huamua kutafuta shababi mmoja atakaemtimizia haja yake.
Kumbuka mwaamke hajachoshwana ndoa, bali ni mambo fulani fulani huyakosa; inawezekana anampenda mumewe kuliko hata huyu anaemridhisha, lakini huamua kutoka nje ili aendelee kuwa na huyu mumewe wakati huohuo awe anafurahia usichana wake. Sijui nimeeleweka hapa?
Ukitaka kugundua hili, mwanamke anaetoka nje ya ndoa akihisi anagundulika yupo tayari kuachana na huyo anaeiba nae na si mumewe; sasa kama ikiwa mumeo hakuridhishi si ubaki na huyu anaekuridhisha? Na si mwanamke tu, hata mwanaume anaesaliti ndoa yake akihisi anagundulika haraka huachana na hicho kibinti na kubaki na mkewe.
Ndoa zina mambo mengi, hilo ndilo jibu muafaka kwangu. Unaweza kuwauliza wanawake mia moja juu ya mahusiano katika ndoa, na ukagundua takriban wanawake thamanini hawaridhishwi na waume zao.
Kadhalika hata wanaume wapo ambao shughuli yao ni kubwa, kwa wiki anaweza kumuingilia mke wake hata mara kumi. Kwa siku tendo moja anaweza kufikia mshindo mizunguko mitatu mpaka minne. Sasa wanawake wengine ni dhaifu huchoka haraka na mara nyingine huwakatalia waume zao.
Hivyo waume namna hiyo huamua kutoka nje ya ndoa na kutafuta kahaba au janajike linaloweza shughuli anayoitaka yeye.
Haya si mambo ya kufikirika, ni vitendo ambavyo tunakutana navyo katika jamii. Na ndiyo maisha ya kila siku ya mwanaadamu, si Afirika pekee bali dunia nzima mambo haya yapo.
Kuna wanaadamu wa kipekee ambao hupendakufanya tendo kinyume na maumbile. Hawa hufundishwa michezo hii na wapenzi wao wa kwanza kwa kuhofia kupata mimba au kuharibu ubikira wao.
Sasa hufikia wakazoea michezo namna hiyo, pindi wakishaolewa hupata bahati mbaya wakaolewa na waume wasiopendezewa na michezo hiyo ya kuenda kinyume na maumbile. Hivyo hutafuta watu wenye kuipenda na hapo ndipo kutoka nje ya ndoa kunapoanza.
Sababu ya tatu: ni kukosa wa kukujali; na mara nyingi sababu hii huwahusu kina dada. Wanawake hupenda kujaliwa, ukimjali mwanamke na kumsikiliza kilio chake hujisikia faraja sana.
Sasa, hutokea wakaolewa ama wakapata wanaume wakatili ambao hawana muda wa kuwafuta machozi. Ndipo wanapotafuta wanaume wanaojua kubembeleza huku wakifanya zaidi ya kubembelezana. Humpa mwili wake kama zawadi ya kumjali.
Nitatoa mfano: mwanamke anaweza kuondoka nyumbani baada ya kutaka kudekezwa halafu akagundua mumewe hana muda nae bali amekazana kuangalia mpira au kuzungumza na marafiki zake huku wakinywa pombe.
Mke huamua kutoka nyumbani akatafuta mahala tulivu na kupata kinywaji kuburudisha nafsi yake, au akaenda baharini kutuliza akili kwa upepo mwanana wa bahari huku akitazama kupwa na kujaa kwa kurasa kuubwa nyeupe za maji.
Huko anaweza kukutana na mwanaume ambae ni mchangamfu, atamchekesha, atamtaniatania mwisho watakuwa marafiki na kuamua kumpa siri ya moyo wake.
Zingatia hili, wanawake hawajui kuweka kitu moyoni, hudhani akimpa kila mtu siri yake au tafrani zake ndiyo faraja asaa akapata msitiri wa kumliwaza. Na ndiyo maana wanawake waliotendwa katika mahusiano niwepesi sana kutongozeka wakati wakiwa katika kilio.
Mara nyingi wanaume wanaojua siri hizo za kinadada kwa lugha ya kimombo huitwa ‘sharp shooters.’ Hawacheleweshi, hapohapo atampa bega lake ili mwanamke apate pa kuegemea na kumaliza kilio chake.
Baada ya hapo wanaweza kupanga kukutana sehemu hiyo kila siku au kila juma, na mabadiliko ya dunia kuna simu za viganjani, watakuwa wanatumiana jumbe fupi za kuliwazana na kutakiana kheri ya usiku.
Mume ataona kero ya mkewe imepungua na kila siku ana furaha, akiombwa ruhusa ya kutoka atafurahi kwani huona atapata wasaa mzuri wa kukaa na marafiki wakitazama mpira, kumbe vyake vinaliwa.
Kwa upande mwingine hata mume hupenda kujaliwa na kuonewa wivu. Mke akijali sana watoto na mashoga akamsahau mume hilo ni kosa katika mapenzi.
Kwa mfano, mume anaweza kuwa amerudi toka kazini amechoka, mke amejitandaza upenuni anapiga soga na mashoga zake au ananyonyesha. Badala ya kumuandalia mume maji ya kuoga au dunia ya sasa hakuna kuandaliana maji ya kuoga, lakini japo ampokee mumewe mizigo, amsaidie kuvua nguo na kumkandakanda mwili kutokana na siku nzito aliyokuwa ayo kazini, lakini hayo hayafanyiki.
Mume anapoona hapewi huduma hizo huamua kutafuta mtu mwenye kuweza kutoa huduma hizo nae afaidi raha za dunia. Wewe utaona mumeo anatoka kazini kila siku amechangamka, utaona amekupunguzia mzigo kumbe mwanamke mwenzio anakusaidia.
Duniani kwa sasa huduma hizi hutolewa kama biashara, kuna wanawake mahsusi wanawafanyia wanaume ‘massage’ na wanalipwa fedha nyingi. Kifupi mwanaadamu hupenda kukandwakandwa mwili wake baada ya kufanya shughuli ngumu ya kutumia nguvu au akili.
Sasa inapofikia wakati mwanaume anavua nguo ili akandwe na jinsia ya kike tena si mkewe, sidhani kama hapo kuna usalama. Lakini ikiwa mke atampa mumewe huduma hiyo ni salama zaidi katika kudumisha mahusiano.
Vilevile mume au mke anaweza kuwa na gubu au kelele kila wakati; mara amembwatukia jirani, mara kamchapa mtoto, mara kamfokea mfanyakazi za nyumbani. Alimuradi mume hana amani katika nyumba.
Akili yake imechoka anahitaji kupumzika au kufanya kazi zake za ofisini nyumbani, matokeo yake huamua kutafuta sehemu kama baa au hoteli iliyotulia ili afanye kazi zake huku anashushia kinywaji. Na baada ya hapo anaweza kukutana na mijanajike inayosaka waume za watu na kuanza uhusiano. Mke hapo inakuwa huna chako tena.
Sababu ya nne: ni mwanaume au mwanamke kutaka kutimiza ndoto yake katika ujana. Tunafahamu vijana wanakuwa na ahadi nyingi, nyingine za kipuuzi na nyingine za maana.
Sasa msichana ama mvulana anaweza kuweka ahadi ni lazima atatembea na mtu fulani kimapenzi.
Mfano, binti anaweza kusoma shule moja na kijana ambae alikuwa akimpenda kwa roho yake yote, ila alikuwa akiogopa kumwambia.
Hutokea miaka ikapita na wote wameshakuwa watu wazima, na mara nyingine keshaolewa na kusahau hata hiyo ahadi aliyoweka.
Inatokea bahati tu siku anakweda kazini au sokoni akakutana na huyo kijana, bado ni mzuri vilevile na mikogo yake ya shule na muonekano vipo vilevile au vimezidi maradufu.
Hapo tena ile ahadi inamjia na pendo linaanza upya, husemwa mtu mzima hana maya. Yaani watu wazima huambizana kiutu uzima. Si kama watoto mpaka wazunguke, wajing’ate vidole au waanza kukunjakunja nguo.
Hapana, watu wazima wao huambiana kitu kilekile kilicho moyoni. Hapo mapenzi huanza na labda kutokana na kumtamani siku nyingi mke hugundua alikuwa akikosa vitamu kutoka kwa huyo kaka. Hapo tena balaa linaanza la kutoka nje ya ndoa.
Hata mwanaume anaweza kuwemo katika kundi hilo la kuweka ahadi kuwa mwanamke fulani ni lazima nimpate, lakini labda wakati anaweka ahadi hiyo alikuwa kijana mdogo na hana pesa za kumghilibu au hana maneno matamu ya kumhadaa.
Hivyo anapopata kazi na kuoa, mara nyingine nae alishamsahau msichana huyo, wakikutana maofisini au njiani ndipo hukumbukana na kijana huamua kutimiza ahadi yake, bila ya kujijua kuwa tayari yumo katika mkataba wa ndoa na mwanamke mwengine.
Na wanaadamu wa siku hizi unaweza kumwambia nimeshaoa ama nimeshaolewa na pete ya ndoa unayo, lakini bado hujisikia raha kufanya machafu na wewe.
Sababu ya tano: ni kuficha udhaifu wako katika jamii inayokuzunguka. Na hii inawahusu sana wakina baba.
Inaweza kutokea mwanaume ni mtanashati sana, awapo ofisini au nyumbani huvaa nadhifu, afanyapo kazi zake huwa makini. Anapoijali familia yake hataki mchezo; kifupi ni mfano wa kuigwa na shujaa.
Wanawake wengi hupenda wanaume mashujaa, wanaojali kazi na familia zao bila ya kujisahau wao wenyewe. Maana wapo wanaume hujali kazi kiasi hawakumbuki familia zao wala miili yao.
Hivyo kwa minajili ya kuwa shujaa katika jamii wanawake wengi hutokea kujigonga kwa baba huyo; baba atajaribu kujiheshimu na kuamua kuwakatalia, ima kwa wazi wakitumia neno ‘sitaki, nina familia’ au kwa kutumia matendo tu; kama kutotimiza miadi ya mualiko wa chakula cha mchana au usiku. Kukataa kahawa au maua anayoletewa ofisini na msichana huyo au hao.
Lakini jamii inayomzuguka baba huyo itaanza kudadisi mienendo yake na wanawake hao. Maneno kama ‘anatupa bahati, au hana nguvu za kiume ndo mana anakataa wanawake wazuriwazuri,’ yatakuwa mengi sana.
Na wanawake wakishasikia minongono kama hiyo ndipo watakapozidisha vituko na kujionyesha wazi wazi kama mwanaume huyo haonyeshi kuwajali ingawa wao ni wazuri na kila mwanaume angetamani kuwa nao.
Kama mwanaume huyo hatokuwa jasiri hapo sasa atataka kulinda hadhi yake katika jamii na kuanza kusaliti ndoa yake. Huo huwa mwanzo wa kutoka nje ya mahusiano.
Kadhalika hata mwanamke inaweza kumtokea hali namna hiyo; anaweza kuwa ofisini bosi akawa anamtamani kimahaba. Atamuongeza mshahara, atampa safari za kikazi ulaya na sehemu nzurinzuri. Lakini ataombwa mapenzi na ahadi nyingi zaidi ya alivyopata ambavyo wafanyakazi wenzie hawana.
Atakapokataa kwa kutaka kulinda ndoa, wafanyakazi wenzie wa kike wataanza kumuandama kwa maneno, ‘wewe huyo mumeo atakupa nini, unaacha bahati kama hii, looohh shoga huna akili unaokota kopo la dhahabu mtaa wa kongo unakataa kulichukua.’ Na maneno mengi namna hiyo.
Mwanamke ataona aibu kwa kutazama hali mbaya ya nyumbani, mara nyingine labda ametishiwa kufutwa kazi na bosi kwa kukataa ombi lake ovu. Hivyo huamua kusaliti ndoa yake si kwa kuwa hampendi mumewe, bali ni kukabiliana na mitihani ya maisha iliyo migumu.
Sababu ya sita: ni msukumo kutoka kwa wazazi, mara nyingi hii huwaathiri wanaume. Inafahamika sana wazazi hasa wa kike hupenda kuwachagulia watoto wao wa kiume wake wa kuoa.
Na hii husababisha mikanganyiko ya mawazo kwa watoto wa wa kiume mpaka kufikia kutoka nje ya ndoa ili kuwaridhisha mama zao. Kwani hali huwa mbaya kiasi mama huamua kumtafutia mwanae wa kiume mwanamke mwengine ili kumkomoa mkwe wake.
Sitoiongelea sana sababu hii, kwani inajulikana sana katika jamii; kisaikolojia wazazi wa kike huwa na wivu sana kwa watoto wao wa kiume. Hutamani wasiondoke nyumbani na ikiwa wataondoka basi waende kwa wake ambao watawachagulia wao, na ikiwa hawajawachagulia basi wake watakaoolewa na wanaume namna hiyo basi wajipange na mashambulizi toka kwa mama wakwe wao.
Mama anaweza kutafuta mtoto wa shoga yake na kumtambulisha kwa mwanae wa kiume huku akijua tayari ni mume wa mtu; kinachotokea hapo ni urafiki wa kiwizi au kihawara mradi tu amfurahishe mama yake.
Lakini ikumbukwe ndoa si kitu cha kukiteganisha hivihivi tu, kwa maana labda wameshazaa, ama wameshakaa katika mahusiano kwa muda mrefu na jamii imeshawazoea kuwaona hivyo. Kutengana na mkewe linakuwa jambo gumu lakini ataamua kumfurahisha mama yake.
Kwa upande wa mwanamke inaweza kuwa tofauti kidogo, familia za kitajiri huwa hawapendi kuwaozesha watoto wao kwa familia za kimaskini. Hivyo hutokea binti akalazimisha kuolewa na mume anaemchagua, lakini katikati ya safari maisha yakawa magumu.
Anapoamua kurudi kwao, familia humtenga na kumwambia ‘tulikuonya usiolewe na huyo mume.’ Matokeo yake mwanamke huamua kutaka kuwaridhisha wazazi wake kwa kutembea na mwanaume mwenye kipato, ingawa mume wake wa awali hajaachana nae.
Maana hutokea ikawa ni ngumu kuachana nae kwani wameshazaa na mara nyingine wameshazoeana.
Sababu ya saba: na ya mwisho kwangu si kwa kila mtu, nasisitiza si kwa kila mtu kwa maana kila mtu atakuwa na sababu zake za kwanini mtu anatoka nje ya ndoa. Sababu hiyo ya saba inatoakna na kufufua penzi lililositishwa na hali ya maisha au mazingira.
Hapa nazungumzia utoto, fedha au jamii inayowazunguka ilivyokua ikiwachukulia. Inawezekana mlipokuwa vijana mlikuwa katika penzi motomoto, lakini kwa kuwa familia zenu zilikuwa na ugomvi wa muda mrefu hivyo haikuwezekana kuoana, ama dini zilikinzana hivyo ukaamua kuoa au kuolewa na mtu mwingine na kumsahau kabisa mtu Yule uliekuwa ukimpenda sana.
Lakini kwa muda fulani mlikosana na mwenza wako Yule wa awali, ukakaa na mume au mke wako mpya hata kwa miaka kumi, ingawa ulikuwa humpendi mume au mke huyo mpya lakini mmeshazaa na inawezekana umeshamsahau mweza Yule wa awali.
Bila ya kutegemea unakuja kukutana na Yule mpenzi wako wa zamani, ambae labda ndie aliekutoa ubikira au kama ni mwanaume ndie aliekufungulia kitabu cha mapezi; kifupi ndie mpenzi wako wa kwanza kabisa katika maisha yako.
Namna hiyo mara nyingi penzi huweza kuchipua upya bila ya kujijua; ile nguvu ya penzi la dhati mlilokuwa nayo inaweza kuwafaya mkumbushie ya zamani.
Kidogokidogo bila ya kujijua mnaweza kujikuta mnachipua penzi lililolala siku nyingi kwani mlitenganishwa tu na mazingira na si ridhaa yenu. Ni hatari sana kuoa au kuolewa na mtu ambae alilazimishwa kuachana na mpenzi wake aliekuwa akimpenda kuliko chochote.
Hivyo sababu zote saba ni vema kuziangalia kwa makini na kujiuliza wewe umeangukia wapi. Usilaumu wala kujilaumu ikiwa unaoa mpenzi wako anatoka nje ya ndoa na kukosa uaminifu, ni vema kukaa nae chini kwa umakini na kumuuliza sababu za kufanya hivyo; kukiwa na sababu za kuachana nae ni vema kuachana kwa wema.
Nasema hivi kwa kuwa wapo watu ambao huwa katika ndoa ambazo hawana furaha, bali hufanya hivyo kwa kuwa tu wana watoto, jamii inawasukuma au familia ndiyo inayolazimisha watu hao kuwa katika ndoa.
Hivyo unapogundua mwenza wako amebadilisha mwenendo wake ni vema mkakaa chini na kuzungumza kuhusu mustakabali wa ndoa yenu badala ya kugombana bila ya kujua tatizo.
Kwa maana kuna mambo katika mahusiano huwa yanamalizwa kwa mazungumzo na si kugombana, hili litasaidia kuepusha matatizo ya kiafya na kiakili yanayoletwa na majuto baada ya talaka za kulazimisha.
Naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment