Kama tumeweza kuishi Afrika tutaishi sehemu yoyote Duniani.
Na Hafidh Kido
Mtoto wa miaka kumi anaamka asubuhi katika kitanda cha kamba, chumba hakina sakafu ni udongo, amelala na nguo alizocheza nazo kutwa siku ya jana. Chumba kidogo vitanda viwili lakini wamelala watano madirisha madogo ya kupitishia hewa ila la kushukuru hakina mlango hivyo hewa itapitia mlangoni.
Anakurupuka kitandani, mswaki upo katika kopo moja lenye miswaki ya watu kama saba, hakuna dawa ya meno anatumia mkaa, anaoga kwa kutumia viganja vyake maji ya baridi na choo ni hichohicho cha haja kubwa, ndogo na kuoga.
Hana haja ya kutafuta kaptula ya shule kwa maana ndiyo aliyokesha nayo tangu jana alipotoka shuleni, anakumbuka shati lake alivaa mdogo wake na bado amelala nalo, anamwamsha ili ampatie shati lake akamilishe sare ya shule.
Hajapiga pasi, hana viatu vya kupiga rangi wala mkoba wa vitabu.
Anakwapua madaftari yake mawili anayoyatumia kuandikia masomo saba mumo kwa mumo. Hana haja ya kuomba nauli kwa maana anatembea kwa miguu mpaka shuleni ingawa ipo umbali mrefu.
Kumbuka hajanywa chai kwa maana mama na baba ndo wamekwenda shambani kuitafuta; akifika shule amechelewa na mwalimu anamngoja kwa adhabu kwani hana fagio la kufanyia usafi na amechelewa.
Akishatandikwa bakora anaingia darasani, madawati hayatoshi anakaa chini; anakumbuka kalamu yake iliisha wino na baba alimuahidi akienda mjini kuuza mazao yake atamnunulia ila hajafanya hivyo ima kwa kusahau au hakuona umuhimu wa kununua kalamu ya mtoto na kuacha kumnunulia rafiki yake pombe kilabuni.
Mwalimu anafundisha mara anaingia mkuu wa shule anataja majina, na kusema ambae hakusikia jina lake atoke darasani kwani tangu muhula uanze hawajaleta pesa za mchango wa majengo. Hivyo waende nyumbani wakawaambie wazazi wawalipie. Badala ya kurudi nyumbani watoto wasio watiifu wanaamua kupitia maporini na kuwinda ndege ama kupopoa maembe.
Miaka saba inamkuta mtoto akimaliza elimu ya msingi kwa mtindo huo. Wachache wanafaulu na wengi wanashindwa kuendelea na elimu ya sekondari.
Waliobahatika kuchaguliwa hali wazazi wana uwezo wanaendelea na masomo, ila wenye bahati mbaya wanaishia hapo kwani wazazi hawana uwezo na serikali nayo haina uwezo kubeba mzigo wote huo ingawa ada ya mtoto mmoja kusoma sekondari ya serikali haizidi laki moja, lakini serikali inapoteza zaidi ya bilioni kadhaa kwa kutokusanya kodi, hali wabunge, mawaziri na maafisa wa serikali gharama za magari na ofisi zao ni kubwa kulingana na aina ya maisha waliyochaguliwa na serikali.
Waliobahatika kusoma mpaka kidato cha sita wengi wataishia hapo na wachache wataingia elimu ya juu, kwa mkopo wa serikali ambao unatolewa pale serikali inapojisikia tena kwa kiwango wanachojisikia. Mtoto kwa kuwa ameshazoea shida huamua kusota kwa miaka mitatu ama minne chuoni wakihemea kidogo wanachopata.
Baada ya hapo ajira huwa ni hadithi nyingine isiyosimulika, kwa maana huajiriwi mpaka uwe una ujuzi wa miaka mitatu, sasa sijui chuoni kuna ujuzi gani.
Na kwa wale wenye mawazo ya kujiajiri msingi wa kujiajiri ni mkopo wa kanzi au Bank kwa lugha ya kigeni, na huo huupati mpaka uwe na kitu kisichohamishika. Shamba la ukoo lazima litolewe sadaka.
Na kwa wale waliokomea darasa la saba ambao ni wengi kuliko hawa wa chuo kikuu huamua kujikita katika kilimo, nguvu wanazoziingiza katika kilimo hazilingani na kipato wanachostahiki. Huamua kukimbilia mjini wakabishane na maisha.
Hawana elimu, hawajui kuongea lugha ya kigeni, hawajui kuvaa makoti na tai, hivyo hawaajiriki. Wanaamua kujiajiri, lakini hawana mjomba wala baba mdogo wa kuwashika mkono, wanaamua kuuza nguo, kuuza bidhaa ndogondogo za kushika mkononi (umachinga).
Serikali inaona aibu kwa wageni na wafadhili wanaokuja nchini hasa ikizingatiwa jiji la Dar es salaam ndipo kilipo kiwanja kikuu cha kupokelea wageni. Kwa lugha rahisi ndipo ilipo sebule ya nchi, napo ndipo wamachinga walipojaa. Inaamua kuwafukuza, haiwataki, wanawanyang’anya bidhaa zao. Mtaji unarudi sifuri.
Kwa wale walioamua kujifichaficha wanapata vijisenti, wanapanga chumba, lakini inabidi apange chumba nje ya mji kwani katikatika ya mji ni ghali sana. Anapata chumba kitunda, kwa mwezi ni shilingi elfu kumi na tano, chumba hakina umeme. Kwa kuwa ameshakuwa barobaro inampasa aoe, anaagiza mchumba wake wa kijijini aletewe.
Mke kwa kuwa ameshazoea kufanya kazi hataki kuwa mama wa nyumbani anaamua kupika chakula ili auze. Mume kutoka nyumbani mpaka mjini kila siku kwenda na kurudi anatumia shilingi elfu moja ya nauli, akila chakula cha mchana na chai ni shilingi elfu mbili, ukichangaya na nauli jumla inakuwa shilingi elfu tatu kila siku.
Mapato yake ya biashara kwa siku ni shilingi elfu kumi, akitoa pesa ya mtaji elfu tano inabaki elfu tano. Akitoa matumizi ya kila siku elfu tatu maana yake anabakiwa na elfu mbili. Kila siku, kwa wiki anapata elfu kumi na mbili kwa kuwa jumapili hafanyi kazi watu hawaji mjini.
Kwa mwezi anapata shilingi elfu arobaini na nane. Hapo hajalipia kodi ya chumba elfu kumi, hajanunua mahitaji ya nyumbani, hajamtumia mzazi wake hela ya mafuta ya taa kijijini, yeye, mkewe na watoto hawajaugua wakajitibu.
Bila ya kusahau biashara haiwi nzuri kila siku, kuna faida na hasara, mama lishe ambae ndie mkewe hajatupiwa chakula chake na askari wa jiji, yeye mwenyewe kama machinga hajatupiwa bidhaa zake na askari wa jiji. Hajakutana na vibaka njiani wakampora kila alichokuwa nacho. Hapajatokea michango ya misiba, harusi au rafiki kumtaka msaada tu wa kifedha.
Kumbuka nimetoa mfano wa Tanzaia, lakini nchi nyingi za kiafrika kama siyo zote hayo ndiyo maisha halisi wanayoishi ama tunayoishi.
Utaona kwamba maisha ya mwanaadamu anaeishi Afrika ni magumu sana, yanakufunza mambo mengi kiasi unaweza kuishi mahala popote duniani hutojali utakutana na mabalaa gani.
Wazungu na ukichaa wao wote ulaya wanapokutana na waafrika wanafanya kazi ngumu katika mazingira hatarishi huwa wanashangaa mambo haya tunayaweza vipi.
Wapi tulipokosea, nini cha kufanya au nani wa kumshika ili aturekebishie haya.
Viongozi tukiwachagua wanajali familia zao tu, mtu anapoingia madarakani anafikiria atumie njia gani abaki madarakani, na si kuwa atumie njia gani kututoa katika huu umasikini wa kutupwa.
Si tu masikini ndiwo wanaopata taabu hizi na mateso; Hata walio katika hali nzuri kifedha, bado wanakutana na changamoto nyingi za kimaisha.
Umeme, maji na barabara bado ni tatizo, umeamua kurudi nyumbani ili umalizie kazi za kiofisi, foleni ya magari inakuchelewesha, unafika nyumbani umechoka unataka uoge na ulale kidogo ili ufanye kazi za ofisi kesho bosi anazitaka. Unakuta maji yamekatika, kutoka nyumbani mpaka maji yanapotoka ni mbali si haba.
Unaaamua kulala hivyohivyo.. unaamka unawasha mashine yako unaanza kufanya kazi, umefika katikati ya kazi umeme unakatika unarudi baada ya saa sita. Umeshakata tamaa na akili haikuruhusu kufanya kazi na kesho bosi anaitaka asubuhi na mapema.
Unaamua kulala ili kesho uamke mapema uwahi ofisini ukaimalizie huko, unaamka mapema kweli lakini kupata daladala ya ofisini ni kwa kugombania, unakaa kituoni nusu saa ndipo unapata gari, njiani unakutana na foleni isiyotembea, unafika ofisini bado umewahiwahi, unafungua kazi unakuta imeliwa na virusi ama umeme umekatika. Je kwa hali hiyo tutafika?
Naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment