Na Hafidh Kido
Kila ifikapo tarehe kenda ya mwezi Disemba, tunasherehekea uhuru wa Tanganyika, uliopatikanwa mwaka 1961, kutoka kwa waingereza.
Wengi tuliozaliwa baada ya uhuru tumekosa dhana ya kupiganiwa uhuru, hatulewi maana ya uhuru, hatujui thamani yake. Kifupi wengine hutamani ukoloni ungerudi.
Nadhani hii hutokana na madhila ya maisha mabaya yanayodhaniwa kuwepo baada ya wazungu kuihama ardhi yetu takatifu. Elimu duni, huduma mbaya za afya sambamba na maradhi yasiyoisha bila kusahau umasikini uliokithiri.
Utaona ni afadhali tungeendelea kutawaliwa. Ila hilo ni wazo la kijinga kabisa kwa mwenye akili, laiti ungepata bahati ya kuzaliwa miaka mia moja iliyopita na kuona namna waafrika walivyonyanyasika katika ardhi yao sijui kama mawazo yako yangefanana na ya sasa. Sijui kama ungetamani hata kuwaona hawa watu weupe na macho yao makali kama mwanga wa tochi; hawakuwa na huruma hata kidogo.
Nakumbuka bibi yangu aliefariki miaka ishirini iliyopita mimi nikiwa mdogo, ukitaja wazungu hasa wajerumani, alificha kichwa chake kifuani huku akilaani kwa lahaja yake ya kimtang’ata ‘kawatajwa hao jamani msiwatajeeee!! Kwani mwawataja kina kingi joji?’ alilaani vikali.
Unadhani ni nini kilichomfanya kulaani na kuogopa? Ni namna wazungu walivyowanyanyasa waafrika katika ardhi yao wenyewe. Hakika hata mimi sitamani wazungu warudi tena ingawa nimezaliwa miaka ya thamanini.
Mwalimu wangu wa ‘Photo Journalism’ Ramadhan Tonge, alipata kuniasa nisiwe na mawazo kama hayo ya kutamani uhuru usingepatikana. Alinambia kipindi chao huduma muhimu kama elimu, afya lishe na usafiri zilitolewa kwa ubaguzi. Kuna baadhi ya maeneo nchini ambayo wazungu walikaa, waafrika hawakuruhusiwa kufika; ukipita tu unakamatwa ama kufunguliwa mbwa.
Sasa kijana mwenzangu tafakari, ndani ya nchi yako mgeni anakuchagulia maeneo ya kupita, darasa la kukaa, zahanati ya kuenda ama huduma nyingine muhimu? Mgeni akuamulie mustakabali wa maisha halafu unasema bora hivyo wazungu wangekuwapo kuliko sasa tupo huru, lazima kichwani kutakuwa na mushkeli.
Turudi katika historia kidogo, bwana C.M.F Lwoga, katika kitabu ‘Uhuru wa bendera,’ ukurasa wa saba anasema, “Ukoloni ambao ni utawala wa mabavu ulioikumba Afrika…. Kiini chake kilikuwa ni ubeberu wa mataifa ya Ulaya.”
Mwandishi anaendelea kueleza “Kuvamiwa na kutawaliwa kwa nchi za kikoloni kulitokana na nchi hizo za Ulaya kutafuta malighafi kwa ajili ya viwanda vyao. Vilevile makoloni yalikuwa ni masoko ya kuuzia bidhaa zilizokuwa zikitengenezwa katika viwanda vyao nchi hizo za Ulaya.”
Hapa muandishi anajaribu kufichua siri ya ukoloni, kwa wale waliosoma historia hawapati tabu kuling’amua hili. Kwa maana wazungu walikuwa masikini na sisi matajiri, tatizo hatukuwa tukijua kuutumia utajiri wetu; na hata sasa hivyo ndivyo ilivyo. Walichofanya ni kuja kutughilibu na kufanya mabadilishano. Sasa sisi tunaonekana masikini na wao matajiri.
Badala ya kuamua inatosha kunyanyasika na tuwawajibishe viongozi walafi wanaoturudisha nyuma, Mtanzania mwenye shahada ya chuo kikuu anatamani kutawaliwa na mzungu. Hataki kuwa huru. Hapa pana shaka.
Nchi yetu ni ya kijamaa, na katiba inatamka hivyo; kwanini tusitumie Azimio la Arusha kuwabana viongozi wetu ili tufaidi matunda ya uhuru badala ya kuendelea kutamani kutawaliwa na wazungu huku tukiubeza UHURU?
Hayati Mwalimu Nyerere, alipokuwa akizungumzia Ujamaa na dhana ya uhuru aliandika “Wakati tunapoyakataa mawazo ya kibepari yaliyoletwa katika Afrika na ukoloni, lazima vilevile tukatae na utaratibu wa kibepari ulioleta mawazo hayo……… sisi waafrika ardhi siku zote ilijulikana kuwa mali ya umma.
“Kila mtu katika kijiji alikuwa na haki ya kutumia ardhi, maana bila ya hivyo hakuwa na njia ya kupata riziki yake; na haiwezekani mtu awe na haki ya kuishi bila ya kuwa na haki ya kupata njia za kutafuta riziki.” (Ujamaa, Julius K. Nyerere, uk 6-7).
Hapa Mwalimu, alikuwa anajaribu kuwafungua masikio vijana wasomi na viongozi waliokuwa wakiukumbatia ubepari ambao ni moja ya mazao ya ukoloni. Uhuru wetu uliandamana na misemo mingi, miongoni mwao ni ‘Uhuru na kazi’. Vijana wa sasa wanalalamika sana kuwa uhuru haujawanufaisha lakini ukiwauliza wamezifanyia nini nafsi zao, si nchi! maana watakujibu si kazi yao; nafsi yake tu ameshindwa kuitendea haki. Sasa utamsaidiaje mtu huyo?
Mwalimu anaendelea kuasa katika kitabu cha Ujamaa, ukurasa wa 3-4, “Ujamaa ni kuhakikisha kwamba wale wanaopanda wanavuna mavuno ya haki ya yale wanayopanda.”
“kujilimbikizia mali kwa sababu ya kujipatia mamlaka au hadhi si mawazo ya ujamaa. Katika nchi ya namna hiyo mali inawaharibu mioyo wale wanaoipata. Mali inawapa hamu ya kuishi kwa raha zaidi kuliko wenzao,” anasisitiza.
Lazima viongozi wetu wafuate ahadi za viapo vyao vya kuilinda katiba ambayo ndani yake inaamini katika ujamaa. Hii itasaidia nchi yetu kufaidi utajiri tulionao na kurudisha imani ya vijana ambao walio wengi hawajui taabu na matatizo waliyopata mababu zetu kwa kutawaliwa. Ni hali mbaya sana kufikia mwanaadamu kutamani kutawaliwa.
Jambo muhimu katika suala la mabepari kutafuta mali ghafi katika makoloni ieleweke kuwa mali ghafi hiyo ilibidi ipatikane kwa gharama ndogo ili kuwawezesha kujipatia faida kubwa. Waafrika walilazimishwa kufanya kazi kwa mabepari wakilipwa ujira mdogo, au kuwalazimisha walime mazao ya biashara ambayo yalinunuliwa kwa bei ndogo.
Kwa maana nyingine sisi tulinyonywa, hatukupewa elimu, huduma za afya wala miundo mbinu kwa faida yetu kama Tanganyika huru ifanyavyo sasa. Ingawa maisha ni mabaya, lakini tupo huru. Usipofanya kazi huli; ila kipindi cha ukoloni usipofanya kazi unakamatwa kwa kutolipa kodi ya kichwa.
Barabara, reli na bandari vilijengwa ili kupata urahisi wa kusafirisha malighafi ulaya, na wao kupata urahisi wa kuitembea Tanganyika. Huduma za kiafya hazikuwa za kutunufaisha sisi, bali ni wao wenyewe; utakumbuka hata wale manamba waliokuwa wakilima mikonge walipoumia kazini hawakupelekwa kwenye hospitali za wazungu.
Huduma za elimu zilitolewa kwa lengo la kumfanya mwafrika ajue kuandika na kusoma; haikuwa kumwamsha toka ujingani.Na ndiyo maana majengo ya shule yalitofautiana. Shule na Hospitali ziligaiwa wazungu peke yao, wahindi peke yao na waafrika waliwekwa na waarabu. Matabaka haya tutayakubali sisi tunaokebehi uhuru?
Mwandishi Lwoga,wa kitabu ‘Uhuru wa bendera’ anaeleza, “Matokeo ya kuvamiwa kwa nchi na kutawaliwa na wakoloni ni kuwa nchi hizo zilizotawaliwa zilipoteza kitu muhimu sana katika historia ya maendeleo ya binadamu. Kitu hicho ni UHURU.” Uk. 6.
Sasa ninachojaribu kuieleza jamii ni kuwa, hapa hatutetei serikali za kiafrika kwa unyonge wanaowasababishia wananchi wake mpaka wakatamani kutawaliwa na weupe. Ila ni kutaka kuiondoa ile dhana ya kuwa uhuru hauna faida yoyote, hakika hiyo ni laana na kukosa hekima. Ni sawa na mfungwa anaeachiwa huru na kuamua kuwaaga wafungwa wenzie kuwa ‘kirago hiki asilalie mtu nitarudi muda si mrefu’ na kweli baada ya wiki anaiba tena anarudishwa gerezani.
Haipendezi kuwa na fikra mgando namna hiyo, lazima ionekane tofauti ya binaadamu na mnyama. Tufikiri kuwa huru, na baada ya hapo tutafute namna za kutoa huduma katika nchi yetu ili uhuru ulete maana.
Tufahamu kuwa hata hizi fikra tulizonazo za kusema heri tusingepata uhuru, au mtu anasema tunashereheKea uhuru gani hali nchi ipo gizani, maji ya taabu na mafisadi wamejaa. Lakini haya yote ni mazao ya kutawaliwa, hatujiamini tena ule ukomavu waliokuwa nao mababu zetu kama kinjekitile Ngwale, chifu Mkwawa na chifu wa Kiyao, Machemba aliewaandikia barua wajerumani kuwajibu ujinga wao, ushujaa huo hatunao tena. Bali tunalalamika tu, madomo kaya.
Chifu Machemba, wa Uyao mnamo mwaka 1899 alimwandikia barua Wissman, aliekuwa Gavana wa Ujerumani, Tanganyika. Alimjibu baada ya Wissman kumtaka Machemba ajisalimishe kwa utawala wa kijerumani.
Majibu ya Chifu Machemba yalikuwa kama ifuatavyo:
“Sioni sababu yoyote ile ya kukutii wewe. Iwapo nia yako ni kutaka urafiki, vema niko tayari, leo na siku zote. Lakini kamwe sikubali kuwa chini ya himaya yako. Iwapo nia yako ni kupigana, vema pia, niko tayari. Lakini siwezi kamwe kuwa raia wako. Mimi ni Sultani katika nchi yangu hii, na wewe ni Sultani huko kwenu ulikotoka. Lakini sijakuambia kuwa unitii mimi, kwa sababu nafahamu kuwa wewe ni mtu huru. Sitakuja huko, kama una nguvu, hebu njoo basi unichukue.”
Hayo ni majibu ya mwafrika halisi mwenye fahari ya kuwa huru na kuwa tayari kuulinda uhuru hata mbele ya silaha kali. Lakini sisi tunataka kujirudisha katika ukoloni kilaini kama mbuzi amuonapo chatu.
Hivyo kama hukuchangia kupatikana kwa uhuru, tafadhali ulinde uhuru wako kwa vitendo na maneno ya kishujaa. Tusibweteke kwa kulalamika, tufanye kazi ili kuonyesha nia ya kuendelea. Wazungu hawana nia ya kutusaidia bali wanataka kutunyonya tena. Wanatutamani kutupata kama leo.
No comments:
Post a Comment