Saturday, December 11, 2010

Hatutakua huru mpaka siku moja tutakapoamua kuwa huru.


 
Na Hafidh kido

Taaluma ya uandishi wa habari ni kama dini mpya inayojiamualia mambo yake na kuishi katika dunia watu waso fikira njema kutofika. Yanaweza kuwa ni maneno mabaya lakini yana maana kubwa kwa wale waliopata kuhudhuria darasa la taaluma ya uandishi wa habari.

Huo ndiwo msingi wake, unapoamua kuwa mwandishi hasa wa habari ni lazima ujivue katika imani yoyote; ikibidi hata familia yako uikane pale panapostahiki kuandikwa ukweli kuhusu jambo fulani.

Na ndiyo maana katika taaluma hii kuna neno la kimombo linasemwa ‘ethical dilemma’ au ‘conflict of interest;’ hivi ni vitu vinavyoogopwa sana na mwandishi aliekula kiapo kuwa msafi.

Kwa muda mrefu tangu kuingia mfumo wa vyama vingi ile ladha ya uandishi wa hakika imeonekana kupungua nchini. Waandishi shupavu na wanaosimamia haki wamepungua ama hawapo tena. Na hata aina ya magazeti tuliyonayo hayana hadhi ya kuitwa magazeti yenye kupasha habari. Unafiki mtupu.

Najua nitapata taabu nyingi baada ya kuandika haya, maneno kama ‘silijui nilitendalo, sijakomaa katika taaluma ya habari ama nimetumwa,’ yatakuwa mengi sana. Ni bora nikose kupendwa lakini niandike kile ninachoamini; ili siku nikifa nisigeukegeuke kaburini kwa kutamani kurudi duniani kufanya hiki nikifanyacho sasa. Kuandika ukweli.

Inahitaji muhariri mwenye moyo wa kutojali mwajiri wake atasema nini ili kuweza kuruhusu makala kama haya kuchapwa katika kurasa zake. Lakini hilo si lengo la makala haya, tujali kilichotuleta humu.

Mimi nipo Uganda kimasomo, lakini taaluma yangu ya uandishi haikomi kwa kuwa nje ya mipaka ya nchi yangu, ule udakuzi wa kutaka kujua kila kinachotokea nyumbani umenifanya kusoma mengi na kuona vita vingi vya waandishi wakongwe wenye kutajika katika tasnia ya habari hapa nchini.  

Kwa kipindi fulani nimekuwa nikifuatilia mabishano hayo, na mengi yalikuwa yakitoka nje ya taaluma hii, taaluma iliyotokea kuogopewa sana na jamii bila kuheshimiwa. 

Ndiyo! Tunaogopewa kwa maana kila tunapoona jambo limeenda mrama tunasema, na hatuheshimiwi kwa kuwa tukinunuliwa kidogo tunafunga midomo yetu na kalamu zinakoma kuandika.

Nimeliona hilo, japo ni mchanga katika taaluma: haimithiliki kwa muandishi kuchagua gazeti la kupeleka habari yake baada ya kuiandika. Maneno kama ‘aahahaa usipeleke makala hayo katika gazeti fulani, hawatoitoa,’ ni aibu sana kufikia hapo.

Kwa maana taaluma ya uandishi habari imekuwa inabadilika misingi na maadili yake kila unapotoka gazeti moja kwenda jingine. Kifupi uandishi wa habari umekuwa ni biashara za kulinda maovu ya watu fulani na kuwakomoa watu fulani kwa sababu tu mmiliki wa gazeti lako haivi na mtu huyo.

Mwandishi wa habari hawakilishi mawazo yake, ni kinyume na mafundisho kutumia neno ‘mimi.’ Bali huandika alichokiona na chenye ukweli, hakandamizwi mtu bali dunia hutaka kujua kinachoendelea kiwe kibaya ama kizuri. Lakini lazima ufuate taratibu.

Kama mtu amekwenda kinyume na maadili fanya nae mahojiano, sikiliza upande wa pili unasema nini, oanisha na tazama haki iko wapi. Usiandike habari kumkomoa mtu, bali toa taarifa kwa manufaa ya umma. Lakini wakati huohuo mhariri hana haki kuzuia habari kwa kuwa tu alieandikwa ana maslahi nae, ni shoga yake ama ndie anaemuweka mjini, ingawa ni kweli amekosa.

Kuna muhariri nguli wa gazeti maarufu nchini, baada ya kutokea sakata fulani la kiuandishi (mgogoro wa kupinga kutaka kuteuliwa waziri fulani wa zamani) alitoa maneno mazuri ambayo nimeyapenda na nikaamua kuyaandikia makala haya unayosoma. Alisema ‘hatutakuwa huru mpaka siku moja tutakapoamua kuwa huru.’ 

Ni kweli waandishi hawataki kuwa huru? Hiyo siku ya kuamuwa kuwa huru itakuja lini kama wasipoamua sasa. Tambua mwandishi unalalamika huthaminiwi katika jamii, lakini huwezi kuthaminika mpaka uanze kujithamini mwenyewe kwanza. 

Mfano ulio hai waandishi wengi wanaishi bila ya mishahara, wanalipwa posho kwa jina la ‘retainer’ ni vibarua, mwajiri ‘atakuretain’ mpaka lini? Waandishi wengi hawana ajira kwa miaka hata kumi katika kampuni na bado wanaendelea kuinufaisha kampuni. 

Tena ukimkuta katika kusaka habari ndani ya gari la kampuni ameweka sambusa (kisugudi) nje, tabasamu kuubwa. Unafurahia nini, au kuwapo mmoja wa vibarua wa gazeti fulani? Inasikitisha.
Lakini akisikia kuna wafanyakazi katika taasisi fulani wamegoma kwa mshahara kiduchu, au wanataka ajira wamechoka kuwa vibarua; waandishi ndiyo wa kwanza kukimbilia na vikamera vyao, hao hao mbio mbio kuandika makala nzito nzito na habari ‘front page.’ 

Ila akirudi ofisini hana mshahara mpaka ‘stori’ yake itoke apewe elfu tatu au tano, au makala apewe elfu kumi au elfu kumi na tano.  Mpaka lini?

Na hautosikia muandishi anaandika makala au habari inayohusu waandishi wenzie kuwatetea haki zao. Anaogopa makala hayo yakionekana kitumbua chake kitaingia mchanga. Tunakwenda wapi na tutafika lini..

Kuna dhana kuwa viongozi wengi wa vyama si CCM, CHADEMA na CUF  tu, bali vyama vyote vya siasa, asilimia kubwa wanamiliki vyombo vya habari, au kuna chombo cha habari wana mkono wao. Lengo likiwa ni kuficha maovu yao na kulipua maovu ya wapinzani wao kisiasa ama kiitikadi. Lakini ikumbukwe si wao wanaoandika habari hizo, bali ni waandishi wa habari ndiwo watumikao kama mbuzi wa sadaka kutimiza malengo ya mabwana wakubwa.

Kuuza taaluma ni sawa na kuuza utu wako, hilo halihitaji shahada ya chuo kikuu kulitambua. Lakini leo hii wafufuke wale waandishi wa zamani waliopata kubobea katika fani hii, na waulize ‘uwapi ule ujasiri waliokuwa nao waandishi wa zamani’ mtajibu nini?

Hatutakuwa huru mpaka siku moja tutakapoamua kuwa huru. 

Angalia ujanja wa walanguzi wa taaluma za watu, kibopa baada ya kukwapua fedha za umma anaanzisha gazeti ama redio, ananunua kampuni kubwa iliyokuwa imara katika kutoa habari zenye hoja nzito. Makampuni ya habari yaliyokuwa mwiba kwa mafisadi na wakengeuka maadili katika jamii.

Baada ya kununua kampuni haishii hapo, ananunua na waandishi. Kichekesho: ati muandishi nae ananunuliwa, na baada ya muandishi kununuliwa nae anajiuza kwa bei rahisi kwa kuandika anachoambiwa na si anachoona.

Mwandishi anaweza kuulizwa na mwajiri wake, ‘tazama pale unaona nini?’ Atajibu ‘nimeona pikipiki inapita,’ basi ataambiwa ‘sasa nakutaka uandike ni gari ndiyo iliyokuwa inapita sawa?’ nae ataandika vilevile alivyoambiwa na bwana mkubwa, ingawa bwana mkubwa huyo hajui hata kuandika ‘lead’ ya habari. Ama hajui hata ‘5W na 1H’ zina maana gani katika habari.

Hajui hata ‘balanced story’ ni kidubwasha gani katika taaluma ya habari. Na bado anakuamulia cha kuandika, huoni haya?
Ifike wakati waandishi nao wanapoingia katika shughuli maalum waheshimike, watambulike uwepo wao. Wajulikane tena kwa majina kama wanavyotambulika madakitari, wahandisi na wanasheria.

Lakini hawawezi kufika huko mpaka jamii iwathamini kutokana na kazi zao zenye haki, mnapoandika kitu kiwe na maslahi katika jamii. Kisilenge kumchafua mtu wala kufurahisha kundi fulani katika jamii au serikali.

Elimu nayo hurudisha nyuma waandishi, hawasomi mpaka wawekewe sheria kwamba mwandishi haajiriwi mpaka awe na shahada. Ni aibu mwandishi una stashahada ama astashahada halafu unafanya mahojiano na mtu mwenye shahada ya uzamivu (Phd) au ni profesa.

Utaona tu hamlingani katika mawazo na aina ya maswali unayouliza hayatokuwa na mantiki wala kuhitaji majibu ya kiuchambuzi.

Na ndiyo maana Rais mstaafu Benjamin Mkapa, amenukuliwa mara kwa mara akiwaponda waandishi wa habari wa Tanzania. Hata mwaka jana  katika maadhimisho ya miaka hamsini ya kampuni kubwa ya habari Afrika Mashariki ‘National Media Group’ jijini Nairobi Kenya, alirudia maneno yake kuwa haturuhusu mwandishi asie na shahada kufanya nae mahojiano.

Hapa naomba niweke wazi, hoja yangu sisemi kuwa waandishi wasio na elimu si waandishi, la hasha. Tena unaweza ukakuta mwandishi ana cheti tu, lakini anaweza kukuandikia habari mpaka ukasikia raha, na mwandishi mwenye shahada akashindwa hata kuandika ‘lead’ au anaweza kuingia chumba cha habari kutoka mtaani lakini hata hajui ‘source’ wake alizungumza nini ambacho ni habari.

Lakini tutambue dunia ya sasa inabadilika, kusoma ni kila kitu. Ukiwa na elimu utajua mambo mengi, na hata ukikutana na watu wenye maringo kwa kuwa tu wamesoma wakigundua wewe umesoma zaidi yao au una uelewa mpana kuliko wao, hakika watakuheshimu na wataufyata mkia.

Cha ajabu mwandishi akishaamua kusoma akipata shahada yake iwe ya siasa, uongozi ama uchumi, basi huihama taaluma na kutafuta kazi mahala kwegine. Kwanini usiendelee kuwa mwandishi uliebobea katika masuala ya uchumi, siasa au jamii kulingana na shahada yako? 

Kwa kuikimbia taaluma yako kisa u msomi tafsiri yake ni kuwa uandishi habari ni wa ‘vilaza’ watu wasiosoma. Kamwe hilo sikubaliani nalo, tubadilike.

Hatutakuwa huru mpaka siku moja tutakapoamua kuwa huru. Nalo liwe neno la leo.
mwisho

Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi wa shahada ya mawasiliano ya umma. Kampala International University. Kampala Uganda. hafidhkido@yahoo.com +256 791848055 au +255 713593894.


No comments:

Post a Comment