Na Hafidh kido
Urafiki ni jambo lisiloepukika katika jamii ya watu wengi; mazingira hutufanya kuwa marafiki ili tupate kusaidiana kwenye shida. Mara zote mtu asie na marafiki huonekana kioja ama mpenda kujitenga.
Huambiwa hata katika dini huruhusiwa kuwa na marafiki wa dini nyingine, mradi tu hao marafiki hulinda mipaka ya dini yako na kuiheshimu.
Na ndiyo maana hata katika Uislamu imekatazwa kukashifu dini ya mwenzako, bali hushauriwa kueleza mazuri ya dini yako ili Yule rafiki avutiwe kujiunga nawe.
Mara kwa mara binafsi nimekutana na mitihani mingi kutoka kwa marafiki wabaya ambao hupenda ulevi; mimi silewi na si tu kwakuwa dini yangu tukufu ya Uislamu imekataza ulevi, bali hata katika familia yetu nimeinukia nikiona watu wakisali na kuchukia pombe.
Hutokea nikaenda katika sherehe, vilabu vya usiku ama mikusanyiko ya unywaji, nami sijivungi na kujitenga na marafiki zangu kwakuwa tu silewi; huagiza soda ama juisi nikaburudisha nafsi. Lakini wale wasioelewa huamua kunichanganyia ulevi pindi niendapo msalani. Ninaporudi nikitaka kuendelea kunywa haraka marafiki wema huniarifu juu ya jaribio hilo baya.
Ndipo nikaamua kuwatenga marafiki wa namna hiyo wasioheshimu mipaka yangu, wasiothamini maamuzi yangu na kudharau dhamira yangu njema ya kukataa ulevi.
Lakini waswahili husema mwana akinyang’anywa kisu hupewa ubua, ndipo hupata marafiki mbadala wa kuwa nami ingawa nawo hulewa. Niwaambiapo silewi na ninahitaji soda tu katika kusanyiko hilo la walevi, basi huheshimu maamuzi yangu na kutoa taarifa kwa walevi wote kuwa bwana huyu si mlevi na naomba muheshimu maamuzi yake kama ambavyo yeye ameheshimu maamuzi yenu ya kuamua kulewa.
Nalo hilo liwe neno la leo; mtu anaposema anapenda au hapendi kitu kadha si vema kumnanga. Bali kama kuna haja mueleze madhara ya kutumia kitu hicho ama madhara ya kutotumia kitu hicho na si kumtenga au kumdharau. Unaweza kuwa na rafiki mlevi ila mwenye kuheshimu mipaka yako.
No comments:
Post a Comment