Na Hafidh Kido
Viongozi wengi wa kiafrika waliokomboa nchi zao kutoka katika makucha ya wakoloni wameiaga dunia wakiwa hawana mahusiano mazuri na nchi za magharibi, ingawa nchi hizo zimekuwa msitari wa mbele kuzisaidia nchi za dunia ya tatu kujikwamua na umasikini.
Dhana hii imetokana na ukweli kwamba wakoloni walikuwa bado hawajajiridhisha na unyonyaji walioufanya barani Afrika, Asia na Latin Amerika. Hakukuwa na ubishi kwamba dunia ilishaanza kubadilika na kujitawala, ulikuwa ni ukulele usiozuilika masikioni mwao.
Wakati wakoloni wakija kupora ardhi Afrika, wajerumani walikuwa na mtu wao akiitwa Karl Peters, ni maarufu sana katika vitabu vya historia. Alikuwa ni mtu mwenye maneno matamu na muongo wa hali ya juu, alijua kucheza na akili za machifu wa kiafrika, hakika alifanikiwa hila zake na Ujerumani ikajitwalia Tanganyika katika karne ya 18.
Mwishoni mwa miaka ya hamsini Ghana ilifungua njia ya Afrika kujitawala, baada ya hapo ilikuwa ni msururu wa nchi za kiafrika kujitwalia uhuru. Mungu aliibariki Afrika rasilimali zisizokwisha, kadhalika bara Asia nalo likajaaliwa utajiri wa mafuta.
Lakini bara la Ulaya Mungu akalinyima utajiri wa ardhini, ila viumbe wale Mungu akawapa utajiri wa vichwani; fikra ama maneno ya sasa wakajaaliwa akili. Na hizo fikra ndizo zinazowafanya wakawa na mafanikio makubwa ingawa hawana chochote cha thamani.
Wataalamu wa historia wanasema bara la Ulaya katika karne ya 15 (baada ya kuzaliwa Kristo) maisha yalikuwa sawa na Afrika. Mpaka kufikia karne ya 16 ambapo waarabu wakifuatiwa na wareno walipoanza misafara yao ya biashara kuja Afrika hapo ndipo balaa lilipoanza.
Yalipokuja mapinduzi ya viwanda mwishoni mwa karne ya 17 na mwanzoni mwa karne ya 18, mambo ndipo yalipokuwa mabaya zaidi barani Afrika.
Mwenye mshale alifuma, mweye panga alirusha na mwenye uongo, busara na ulaghai aliutumia ili tu apate kupora rasilimali za bara hili. Wazungu waliajabishwa sana na vyanzo vya maji, mito, maziwa makubwa na mabwawa yasiyo mfano yatiririshayo maji mwaka mzima bila kukoma, hakuna ukame wala balaa la njaa.
Dhahabu, almasi, fedha, shaba na madini yasiyo idadi na mengine waliyaona hapa kwa mara yao ya kwanza. Ardhi yenye rutuba inayokubali kila mmea bila ya kutumia mbolea wala kuhitaji mabwana shamba wa kuelekeza upandaji bora.
Haya yote yaliwatetemesha wakoloni, hawakuamini kukuta vitu kama hivyo katika dunia ya watu wasiojua thamani yake.
Wakafanya kila hila na kuvipora vyote ambavyo walidhani vinabebeka, na ambavyo waliona hawatoweza kuvibeba kama ardhi, mito, bahari na mabwawa, walifanya namna ya kuwalazimisha wazawa wawafanyie kazi kwa niaba yao na kila kilichopatikana walibeba. Kwa lugha rahisi, waliiba.
Uroho ulipowazidi waligundua Mungu ametupatia mpaka nguvu za mwili, hivyo wakaiba mpaka wanaadamu na kuenda nao huko ulaya wakawatumikishe kwa kazi za harubu ili wawazalishie mali. Waafrika waliwapatia malighafi, waliwasaidia kusafirisha na walipofika huko walikuwa nguvu kazi ya kuzalisha walichotaka na fadhila yao ilikuwa ni kuwaita manyani au watu wasiostaarabika (uncivilized).
Walifanya haya kwa miaka zaidi ya mia moja, mpaka hao waliowapeleka huko ulaya walipoamka na kuanza kupaza sauti za kutaka warudishiwe kile walichonyimwa kwa miaka yote hiyo ndipo wasomi wa kiafrika waliobahatika kufika ulaya walipopaza sauti za madai ya kuwa huru.
Wakarudi nyumbani(Afrika) na kutoa taarifa hizo kwa ndugu na jamaa ili kufuata sauti hizo zinazowakera wazungu. Hatimae kiminyano kilipokuwa kikubwa Wamarekani ambao nao walionja ladha ya kutawaliwa waliungana na waafrika kuwaambia wazungu kuiacha huru Afrika.
Wajerumani, Wabelgiji, Wafaransa na Waingereza waliamua kuachia makoloni yao ingawa kwa shingo upande . Ila waliachia tu zile ambazo walidhani hazitowafaa tena.
Wareno kwao ilikuwa tabu kidogo, walikataa kuachia makoloni kwani walishajisahau na kudhani wamefika, utaona nchi nyingi zilizotawaliwa na wareno waliondoka kwa mtutu wa bunduki. Kadhalika waingereza kuna baadhi ya nchi walishapanga mikakati yao ya namna gani watarudi hivyo waliamua kuziachia kirahisi ingawa walisumbuana kidogo na wadai uhuru mpaka kufikia kuwatia ndani kwa kesi za uongo alimuradi tu kuwavuja moyo wabadili nia.
Nchi kama Kenya, South Africa, Zimbabwe na baadhi ya hizo ilikuwa tabu kidogo kuachiwa na waingereza, maana zilikuwa na mashamba makubwa ambayo ndiyo yaliyokuwa yakilisha ulaya nzima. Walifadhaika sana kuona sasa tutakuwa ombaomba wa Afrika ikiwa tutawapatia uhuru wote.
Lakini kama nilipozungumza awali, wazungu Mungu aliwanyima rasilimali, lakini aliwajaalia uwezo mkubwa wa kufikiri. Walijua namna ya kucheza na akili za waafrika. Wale ambao walipewa uhuru mikononi kama kina Nyerere, kwame Nkurumah na Kenyata walikuwa ni wagumu kidogo kuhadaiwa, ila wakaamua kukaa chini kama umoja wao na kuunda umoja wa Mataifa (UN) mwanzo ilianza League of Nations, na kubadilishwa kuwa (UN).
Kumbe hapo ndipo balaa lilipoanza, wazungu walicheza na akili zetu kwa kuunda mashirika mengi ambayo yalikuwa chini ya umoja wa mataifa, ambayo yataweza kupenya katika ngome za mataifa ya kiafrika kirahisi na kuchota kila kinachofaa kwa kutumia waafrika wasio na uzalendo.
Kazi ya kwanza ya umoja wa mataifa ilikuwa ni kuvuruga amani duniani, ili mashirika yaundwe haraka haraka na kutuliza amani wakati huohuo nafasi itumiwe kuleta vibaraka watakaochota utajiri uliobakishwa na wakoloni.
Kazi ya pili ya umoja wa mataifa ilikuwa ni kuhakikisha USSR (Union of Soviet Socialist Republics) inapotea kabisa sambamba na Usoshalist duniani. Maana nchi nyingi za kiafrika walishaanza kuvutiwa na ujamaa, nchi kama Cuba, China, Urusi na Ujerumani ya Mashariki, walikuwa wakitoa msaada mkubwa kwa nchi masikini. Hii ilisababisha malengo ya kuwafanya waafrika wawe tegemezi yafifie.
Maana wazungu walitaka waafrika wawe tegemezi na mwisho tukubali kuwaita warudi kututawala. Na ndiyo maana vijana wa mitaani waliokata tamaa ya maisha utawasikia wakisema “ni heri wazungu wasingeondoka, ili waendelee kututawala labda maisha yangekuwa mazuri,” au utasikia kijana anasema “ni heri ningezaliwa paka au mbwa ulaya kuliko nilivyozaliwa binaadamu Afrika.”
Si maneno ya kuyapuuzia hata kidogo, utegemezi ni ndoto ya muda mrefu ya mataifa ya ulaya ili tuwaite wenyewe ingawa sisi ndiwo tuliowafukuza. Inakuwa sawa na kuramba matapishi yetu.
Uchina, Urusi, Ujerumani ya mashariki na Cuba, zilikuwa mwiba kwa nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani, Uingereza, na Ufaransa. Hawakupenda namna Afrika ilivyokuwa ikisaidiwa na nchi hizo za kijamaa.
Chini ya mfumo wa kijamaa waafrika wengi walipata nafasi za kuenda kusoma nje, walikuja wataalamu kuwafundisha namna ya kuunda baadhi ya vitu, waafrika walifudishwa mbinu za kijeshi, walifundishwa namna ya kujitegemea na misaada lukuki ililetwa bila ya masharti magumu. Hilo liliwaudhi mabepari.
Mbinu zikaundwa kuua umoja wa kisovieti, mabeberu wakaitawala dunia; waliojidai vichwa ngumu kama kina Nyerere na ujamaa wao waliadabishwa na kubaki kujutia kwanini walikumbatia ujamaa.
Maana mpaka leo ujamaa wa Tanzania ni mdahalo usio na majibu muafaka nani hasa aliuua Ujamaa; Mwalimu mpaka anakufa wapo wanaosema alikubali kuwa ujamaa haufai na wapo wanaosadiki kuwa Mwalimu alifariki akiamini ujamaa unafaa hata sasa.
Ikaja benki ya Dunia, hicho ni kichefuchefu nadhani hata kilisababisha kumuua Mwalimu Nyerere, kwa namna alivyokuwa anawachukia viumbe hawa wa benki ya Dunia. Maana ni kirusi kilicholetwa kudumaza fikra za viongozi wa kiafrika. Wanatoa misaada ya uongo na kuweka masharti magumu yasiyotekelezeka.
Kwa mfano wanaweza kukupa msaada wa shilingi mia, lakini wakakuambia uongeze mishahara ya wafanyakazi, uongeze wawekezaji wa kizungu na kupunguza mrahaba wa wawekezaji katika sekta ya madini, hoteli kubwa, mashamba ama viwanda, ukubali thamani ya pesa yako ishuke katika soko la Dunia na bei ya bidhaa unazokwenda kuuza katika soko la Dunia wapangaji wa bei wawe wao. Sasa kuna kuendelea hapo?
Pesa wanazokupa ni nyingi ambazo wanajua huna uwezo wa kuzilipa na pia huna uwezo wa kuzikataa, sasa njia rahisi ya kukubali kusamehewa madeni ni kuwa mtoto mtiifu ufuate masharti yao ili usamehewe.
Na mbaya zaidi masharti nayo yanakuwa magumu ila inatumika ile methali ya ‘heri lawama kuliko fedheha,’ ‘funika kombe mwanaharamu apite,’ au ‘mtumikie kafiri upate muradi wako,’ mpaka lini?
Sasa wamekuja na mbinu mpya; na hii ndiyo kiboko yao: kuvamia kijeshi kwa kila kiongozi ambae anakataa kufuata masharti yao baada ya kuona vikwazo vya kiuchumi vinagoma, hutaki kuchukua mkopo benki ya Dunia ama huchekicheki nao.
Watakuundia kesi mwisho Dunia nzima itakuona hufai, kifuatacho wanakaa mabwana wakubwa wanapiga kura ya VETO, halafu hawasubiri kura hiyo ifikie nusu wala robo tatu ya wajumbe, wanakuvamia wanakutoa katika kiti na kukuua au kukupeleka katika limahakama lao na kutafuta mtu mtiifu atakaechukua nafasi yako kuwafurahisha wao.
Na hapo ndipo makala yetu inapoanzia, vuguvugu la Dunia ya kiarabu matajiri wa mafuta na uvamizi wa Uingereza, Marekani na Ufaransa nchini Libya.
Vita ya muungano wa Marekani Ufaransa na Uingereza dhidi ya Libya ina mfanano mkubwa na vita ya Iraq. Kumbukumbu zinasema April mwaka 1986 ndege za kivita za kimarekani zilivamia Libya kwa madai Gaddafi alihusika na ugaidi uliotokea West Berlin siku kumi nyuma, na taarifa hizo zililetwa na ‘strong force US intelligence’.
Rais Ronald Reagan, alivamia mji wa Tripoli na Benghazi(mji tajiri wa mafuta) kwa mizinga iliyotupwa na ndege za kivita.
April 16, 1986 Marekani walianza mashambulizi saa mbili ya asubuhi, ndani ya dakika 12 walitupa mizinga ya tani 60 na hawakupata upinzani wowote toka majeshi ya Libya ambayo hayakuwa hata na ndege moja ya kijeshi kujitetea. Utaona nguvu iliyotumika ilikuwa ni kubwa kuliko ilivyostahili.
Madai makubwa ya Marekani kuivamia Libya mwaka 1986 ni kuwa Muammar Gaddafi alikuwa akitumia utajiri wa mafuta kudhamini ugaidi. Uvamizi huo uliopewa jina la (Operation El Dorado Canyon) ulihusisha zaidi ya ndege 100 za Kimarekani wakisaidiwa na Waingereza ingawa wafaransa walikataa kushiriki na hilo liliwakera sana Wamarekani.
“watu wa Libya lazima walindwe na kwa kukosekana kuisha kwa haraka vurugu dhidi ya wananchi, muungano wetu umejiandaa kuchukua hatua na tutachukua hatua kwa umuhimu wake.” Barack Obama.
Lakini maneno haya yana utata, ikiwa wameungana ili kunusuru maisha ya walibya, mbona wanaangusha mabomu mazito yanayoangamiza makazi na hata wananchi wenyewe?
Na je, wanabariki uasi unaotokea Libya au wanaziba masikio yao kwa manufaa binafsi ya kutaka kuiba mafuta ya walibya kama walivyofanya Iraq?
Kwa maana ikiwa wananchi wataandamana kutaka madai ni lazima wawe waandamanaji na si vinginevyo. Pengine wawe wanapindua nchi, na wakishidwa kupindua nchi huwa inaitwa ‘attempt coup d’état’.
Lakini waandamanaji hawa wanabeba silaha nzito, na cha kushangaza ukisoma na kusikiliza vyombo vya habari vya kimataifa hawawaiti waandamanaji tena, bali ‘waasi.’ Sasa tuulizane mimi na wewe, je Barrack Obama, ameamua kubariki waasi na kuwalinda?
Majibu ya Gaddafi baada ya uvamizi huo wa ndege za kifaransa yalikuwa ni: “hatutaacha mafuta yetu kwa wamarekani, ufaransa, uingereza wala maadui wa mataifa ya kikristo ambayo yanaungana kutupinga,” alisema.
“hatutoiacha ardhi yetu. Tutapigana kwa kila inchi ya ardhi yetu na tutakomboa kila inchi ya ardhi hiyo.” Aliongeza Gaddafi.
Tukio jingine la kushangaza ni kuonekana kwa wananchi watiifu kwa Gaddafi wakiwa wamebeba mabango yanayosema : "Colonialism will never be back again in Libya." (Ukoloni hautorejea tena Libya)
Muunganiko wa matukio ni kuwa mwezi kama huu wa Machi mwaka 2003, Marekani ilitangaza vita dhidi ya Iraq wakisaidiwa na Waingereza, kwa madai Saddam Hussein Rais wa Iraq, ana mabomu ya maangamizi yasiyofaa.
Lakini cha kushangaza vita hiyo haikupata baraka za umoja wa mataifa wala baraza la usalama la umoja huo halikutumia sheria ya kulinda raia ya mwaka 1973, iweze kufanya kazi kulinda raia wa Iraq kama ambavyo imelazimishwa kufanya kazi kulinda raia wa Libya.
Kwani September 16, 2004 aliekuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan, alitangaza kuwa uvamizi huo haukuwa na baraka ya umoja wa mataifa, na kwa mtazamo wa umoja wa mataifa uvamizi haukuwa wa halali.
Tarehe 18 November 2002, waangalizi wa silaha kutoka umoja wa mataifa (United Nations Monitoring, Verification and Inspection Commission) walirudi Iraq kwa mara nyingine na Hans Blix, aliekuwa kiongozi wa tume hiyo na Mohamed ElBaradei, kiongozi wa wakala wa kimataifa wa nishati ya Atomic (International Atomic Energy Agency), walifanya uchunguzi bila ya kutoa majibu yoyote mpaka walipoondolewa siku chache kabla ya majeshi ya George Bush na Tony Blair kuivamia Iraq kimabavu.
Has Blix, anadai mpaka sasa Marekani na Uingereza hawajatoa ushahidi unaokubalika juu ya madai yao kuwa Iraq ilikuwa ikimiliki silaha za maangamizi ingawa walilazimishwa kupekua mpaka kwenye nyumba za wanasayansi wa kiiraki.
Kinachotokea sasa katika Dunia ya waarabu ni kuvuruga utawala ambao upo madarakani kwa muda mrefu na haujawanufaisha chochote mabwana wakubwa.
Wataondolewa ili wawekwe wengine ambao watakubali kuendeshwa na mataifa ya kimagharibi ili wanyonye mafuta.
Hakuna tofauti na ukoloni ulioondoka mwishoni mwa 1950 na mwanzoni mwa 1960.
Wakoloni walikuja kutunyonya kwa kuwa viwanda vilihitaji malighafi na ardhi ya kupandia malighafi hizo, na sasa wamehamia nchi za kiarabu tajiri kwa mafuta kwani magari, mashine na vifaa vingi vinatumia mafuta kujiendesha na wao hawana. Wanaishia kuyanunua kwa bei ya juu toka kwa waarabu na kuwatajirisha ambapo kwao ni kosa la jinai kumtajirisha mtu anaetoka dunia ya tatu.
Watayapataje, lazima watumie mabavu kwa maana zamani waafrika tulihadaiwa kwa vitu vidogo kwa maana tulikuwa wajinga hatuna elimu, ila sasa dunia nzima ina elimu. Mwenye nguvu ndie atakaeitawala dunia.